NISHATI YAJIVUNIA MAFANIKIO MIAKA MINNE YA SERIKALI YA AWAMU YA TANO

 •  Ongezeko la megawati 480 za umeme katika gridi ya Taifa
 • Bilioni 138 zimeokolewa kwa kuachana na matumizi ya mitambo mikubwa ya kufua umeme wa mafuta
 • Uwepo wa ziada ya umeme usiopungua megawati 280 kwa siku
 • Kusitisha uagizaji vifaa vya umeme nje ya nchi
 • TANESCO – kutoka kampuni inayopata hasara na kuwa inayotengeneza faida na kujiendesha pasipo ruzuku
 • Ongezeko la asilimia 400 uunganishaji umeme vijijini
 • Gesi asilia imefikia futi za ujazo trilioni 57.54
 • Uwepo wa mafuta yanayotosheleza mahitaji pamoja na akiba

 Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani amefanya mkutano na waandishi wa habari na kueleza mafanikio ya sekta ya nishati, yaliyopatikana katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Tano.

Mkutano huo ulifanyika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam, Februari 2, 2020 na kuhudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu, Naibu Katibu Mkuu Mhandisi Leonard Masanja, pamoja na viongozi mbalimbali wa Wizara na Taasisi zilizo chini yake.

Akielezea mafanikio hayo, Waziri Kalemani aliyagawa katika sehemu nne ambazo ni hali ya upatikanaji umeme nchini, usambazaji umeme vijijini, matumizi ya rasilimali ya gesi asilia pamoja na hali ya upatikanaji mafuta nchini.

Yafuatayo, ndiyo aliyoyaeleza Waziri kwa kila sehemu:

Hali ya upatikanaji umeme nchini

 • Hali ya upatikanaji umeme nchini imeendelea kuimarika siku hadi siku. Tunao umeme wa kutosha kwa sasa. Mwaka 2015 tulikuwa na megawati 1,038 za umeme katika gridi ya Taifa. Leo hii tuna jumla ya megawati 1,602.34. Tumeongeza zaidi ya megawati 480 mpya na tumekuwa na ziada ya umeme usiopungua megawati 280 kila siku.
 • Tumeimarisha miundombinu ya uzalishaji umeme kwa kuongeza njia kuu za kusafirisha umeme ambazo hazikuwepo huko nyuma. Mwaka 2016 tulikamilisha mradi wa kusafirisha umeme mkubwa wa kilovoti 400, umbali wa kilomita 670 kutoka Iringa kupitia Dodoma – Singida hadi Shinyanga.
 • Pia, tulikamilisha mradi wa kusafirisha umeme mkubwa wa kilovoti 220 kutoka Makambako kupitia Madaba hadi Songea, umbali wa kilomita 250.
 • Tumeendelea kujenga njia za kusafirisha umeme (kilovoti 132) mahala ambapo hazikuwepo kabisa mathalani kutoka Mbagala – Mkuranga – Nanjilinji Mtwara kupitia Lindi, umbali wa kilomita 5.2.
 • Tumeendelea kuunganisha maeneo mengi ambayo hayakuwa kwenye gridi ya Taifa, hasa yaliyokuwa yanatumia mashine za kufua umeme wa mafuta.
 • Tumeondoa takribani vituo 12 vilivyokuwa vikitumia mafuta ambavyo baadhi yake ni Ngara, Biharamulo, Songea, Mbinga, Namtumbo, Ludewa na Nyakato. Tumeokoa pesa nyingi ambazo zilikuwa zinatumika kwa ajili ya kununua mafuta katika maeneo hayo.
 •  Pia, tumeondoa mitambo mikubwa ya IPTL (megawati 103), Aggreko (megawati 48) na Symbion (megawati 120-129) ambapo tumeokoa takribani shilingi bilioni 138. Tulipoondoa mitambo hiyo, tuliweza kuokoa kwa mwezi shilingi bilioni 6.9 zilizokuwa zinatumika kwa ajili ya uendeshaji wake.
 •  Vilevile, tumeendelea kuunganisha maeneo mbalimbali katika gridi ya Taifa na kuokoa shilingi bilioni 121. Maeneo hayo ni Tunduru, Mnazimmoja mkoani Lindi kuelekea Luangwa, umbali wa takribani kilomita 80 (kilovoti 132), Liwale, Masasi na Nanyumbu.
 •  Mwaka 2015, transfoma zilizokuwa zimefungwa nchini kote zilikuwa 12,000.2 lakini leo hii, jumla ya transfoma 23,000.56 zimefungwa nchini sawa na ongezeko la zaidi ya asilimia 100) Pia, tumeendelea na ukarabati wa transfoma zilizokuwa mbovu.
 •  Mwaka 2015, tulikuwa na nguzo za umeme zilizojengwa nchini milioni 1.1. Leo, tuna zaidi ya nguzo milioni 3.7 zilizotumika hivyo tumeongeza usambazaji umeme katika maeneo mengi hivyo kuimarisha kabisa hali ya upatikanaji wau meme nchini.
 •  Mwaka 2017 tuliweka mkakati wa kiserikali kuhakikisha kwamba shughuli zote za usambazaji na ujenzi wa kupeleka umeme kwa wananchi, zinafanyika kwa haraka. Njia pekee ilikuwa ni kuhakikisha vifaa vinapatikana ndani ya nchi hivyo tulisitisha rasmi uagizaji vifaa hivyo kutoka nje ya nchi.
 •  Wakati huo tulikuwa na kiwanda kimoja cha kuzalisha transfoma, sasa viko vinne. Uwezo wetu wa ndani ilikuwa ni transfoma 97, leo hii ni 21,000 ingawa mahitaji yetu ni 14,000 kwa sasa. Kwahiyo transfoma zilizopo ni nyingi hadi zinabaki ziada.
 •  Pia, mwaka 2017 tulisitisha uagizaji wa nguzo kutoka nje ya nchi. Wakati huo, mahitaji yetu ya nguzo yalikuwa milioni 1.2 na uwezo wetu wa ndani ulikuwa 800,000 hivyo zilikuwa hazitoshi. Leo, tuna viwanda 10 ambavyo vinazalisha nguzo zaidi ya milioni 2.5 wakati mahitaji yetu ni chini ya milioni 2 kwa mwaka.
 •  Hii imesaidia sana kutengeneza ajira kwa watanzania. Zaidi ya watanzania 3,000 wameajiriwa kutokana na uwepo wa viwanda hivi vipya. Aidha, tumeokoa shilingi bilioni 162.23 kwa kutumia nguzo za ndani ya nchi.
 •  Kwa upande wa mita za LUKU, awali hatukuwa na viwanda hapa nchini. Mwaka 2017 tulisitisha kuagiza mita hizo kutoka nje ya nchi. Kwas asa tuna viwanda vikubwa vitatu vya kuzalisha mita za LUKU. Mahitaji yetu ni mita milioni 1.56 wakati uwezo wa kuzalisha ni zaidi ya mita milioni 2.5.
 •  Aidha, tulikuwa na kiwanda kimoja cha nyaya za umeme. Leo tunavyo zaidi ya vinne. Mahitaji yetu ni kilomita 149,000 kwa mwaka wakati uwezo wa kuzalisha ni kilomita 250,000.
 • Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) lilikuwa linapata hasara wakati ule kiasi cha shilingi milioni 439 lakini leo shirika halina hasara na linatengeneza faida. Kwa mwaka huu wa fedha, shirika limelipa gawio kwa serikali kiasi cha shilingi bilioni 1.43.Usambazaji umeme vijijini
  • Usambazaji umeme vijijini umeenda kwa kasi kubwa sana. Mwaka 2010, vijiji vilivyokuwa na umeme ni 562, mwaka 2015 vijiji 2,018 na leo hii tumefikia vijiji 8,517 kati ya 12, 268 vilivyopo nchini. Vijiji takribani 7,000 vimepelekewa umeme ndani ya miaka minne ambapo ni sawa na ongezeko la asilimia 400.
  • Baada ya Juni mwaka huu, tunatarajia vitabaki vijiji 1,822 tu ambayo ni sawa na chini ya asilimia 15 ya vijiji vyote nchini. Ifikapo Juni 31, 2021 hakutakuwa na kijiji ambacho hakijafikiwa na umeme.
  • Aidha, mwaka 2015 hatukuwa na Wilaya iliyokamilika kuunganishiwa umeme katika vijiji vyake vyote. Leo hii tunazo jumla ya Wilaya 34 nchini ambazo vijiji vyake vyote vimepata umeme.
  • Mwaka 2015, Taasisi za Umma zilizokuwa zimefikiwa na umeme zilikuwa 3,200 lakini leo idadi ya taasisi hizo imefikia 11,070 sawa na ongezeko la asilimia 500.
  • Kwa nchi za Afrika Mashariki, Tanzania inaongoza kwa kupeleka umeme vijijini kuliko nchi nyingine.

  Matumizi ya gesi asilia

  • Tunayo gesi ya kutosha nchini. Jumla ya gesi tuliyonayo ni futi za ujazo trilioni 57.54. Mwaka 2010 mahitaji yetu ya gesi yalikuwa futi za ujazo milioni 40. Mwaka 2019 mahitaji yetu yalikuwa futi za ujazo milioni 80 na sasa mahitaji yetu ni futi za ujazo milioni 200 kwa siku.
  • Kati ya hizo, futi za ujazo milioni 135 zinatumika kuzalisha umeme na zilizobaki zinatumika katika viwanda na matumizi mengine ya ndani.
  • Tumeunganisha viwanda vikubwa zaidi ya 48 katika mtandao wa gesi na zoezi linaendelea. Aidha, magari zaidi ya 250 kwa sasa yanatumia gesi nchini na wananchi zaidi ya 500 wanatumia gesi asili kupikia.

  Upatikanaji wa mafuta nchini

  • Hali ya upatikanaji wa mafuta nchini inaimarika siku hadi siku. Mwaka 2014 tulikuwa na utaratibu wa kuingiza mafuta kibinafsi. Serikali ikaanzisha Wakala wa Kuingiza Mafuta kwa Pamoja (PBPA).
  • Mwaka 2015, uwezo wetu wa Bandari kupakua mafuta ulikuwa tani 165,000 na tulikuwa na bandari moja tu. Baada ya miaka miwili, tukaongeza bandari mbili zenye uwezo wa kupakua mafuta tani 45,000 kila moja.
  • Hiyo imefanya kwa ujumla wake, bandaro zetu kuwa na uwezo wa kupakua mafuta tani 255,000.
  • Tuna akiba ya mafuta kiasi cha kutosha ambapo kwa upande wa dizeli akiba tuliyonayo leo ni lita milioni 197.21 inayoweza kutosheleza mahitaji kwa zaidi ya siku 26. Petroli ziada ya lita milioni 97.2 inayotosheleza mahitaji ya zaidi ya siku 38, mafuta ya ndege ziada ya lita 30.18 yanayotosha kwa siku 58 na mafuta ya taa lita laki 6.6
  • Vifaa vyetu vya kuhifadhi mafuta nchini kwa sasa vina uwezo wa kuhifadhi lita bilioni 1.3 kutoka uwezo wa zamani wa lita milioni 900.

Na Veronica Simba