• Umegharimu bilioni 216 za Tanzania
  • Umetekelezwa kwa ushirikiano wa Tanzania na Sweden
  • Utaokoa bilioni 9.8 kila mwaka
  • JPM, Balozi wa Sweden waipongeza Wizara ya Nishati
  • Waziri Kalemani asema ukatikaji umeme Ruvuma sasa basi

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, amezindua mradi mkubwa wa njia ya usafirishaji umeme wa kilovoti 220 kutoka Makambako mkoani Njombe hadi Songea mkoani Ruvuma.

Alizindua mradi huo Aprili 6, 2019  katika kituo cha kupoza na kusambaza  umeme kilichopo Unangwa, Songea Mjini; ambacho ni kimojawapo kati ya vituo vitatu vya Mradi huo; vingine vikiwa ni vya Madaba na Makambako.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na wananchi katika uzinduzi wa mradi wa Ujenzi wa njia kuu ya kusafirisha umeme KV 220 kutoka Makambako hadi Songea pamoja na vituo vya kupooza umeme KV 220/33 katika sherehe zilizofanyika Songea mkoani Ruvuma.

Akizungumza katika hafla hiyo iliyoshirikisha viongozi mbalimbali wa serikali na wananchi; Rais Magufuli aliishukuru serikali ya Sweden kwa kuchangia fedha zilizowezesha kutekeleza mradi husika.

Aidha, aliwataka wananchi katika maeneo ambako mradi umepita, zaidi ya kilomita 250 kutoka Njombe hadi Ruvuma,  kuutunza na kuulinda kwani ni mkombozi wao kimaendeleo.

“Kwa mujibu wa utafiti uliowahi kufanywa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), takribani watu 600,000 hupoteza maisha kwa sababu ya matatizo yanayohusiana na matumizi ya mafuta ya taa, mkaa au kuni,” alisema Rais na kuongeza kuwa ni kwa kutambua hilo, yeyé binafsi amefarijika sana kuzindua mradi huo wa kusafirisha umeme utakaovinufaisha vijiji zaidi ya 122.

Rais Magufuli alisema mojawapo ya faida kubwa za mradi huo ni kusaidia kutatua changamoto ya umeme iliyokuwepo katika mikoa ya Njombe na Ruvuma na kuokoa kiasi cha shilingi bilioni 9.8 kwa mwaka, zilizokuwa zikitumika kulipia gharama za uzalishaji wa umeme wa mafuta.

“Napenda kutumia fursa hii kuipongeza Wizara ya Nishati kwa kusimamia utekelezaji wa mradi huu. Nawapongeza sana. Aidha, nawapongeza watanzania kwa kufanikisha ujenzi wa mradi huu.”

Akieleza zaidi kuhusu mikakati ya serikali anayoiongoza, Rais Magufuli alisema kuwa azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuipatia Tanzania umeme wa kutosha, wenye uhakika na wa gharama nafuu.

Akizungumzia athari za ukosefu wa umeme kwa Tanzania, Rais alisema kila mwaka, nchi yetu hupoteza takribani ekari 400,000 za miti kwa ajili ya mkaa na kuni, hali inayochangia uharibifu mkubwa wa mazingira.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akimshukuru Balozi wa Sweden hapa nchini Anders Sjoberg mara baada ya uzinduzi wa mradi wa Ujenzi wa njia kuu wa umeme KV 220 kutoka Makambako hadi Songea pamoja na vituo vya kupooza umeme KV 220/33 katika sherehe zilizofanyika Songea mkoani Ruvuma.

Alisema, ni ukweli usiopingika kwamba uharibifu huo hauwezi kuisha endapo serikali isipotafuta suluhisho kwa kuwapa wananchi wanaotegemea nishati ya kuni na mkaa, njia mbadala ili waache kukata miti.

Akifafanua zaidi, alisema ni kwa sababu hiyo, serikali imeamua kutekeleza mradi wa umeme wa Rufiji ambao ukikamilika utakuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 2100 za umeme; ambazo ni zaidi ya umeme wote tulionao sasa.

“Kwa sasa tuna megawati 1,560; ule utatoa megawati 2,100. Tunataka katika miaka kadhaa, tuwe na megawati zaidi ya 5,000 ili viwanda vyetu viendeshwe vizuri,” alieleza.

Alisema, Mradi wa Umeme wa Rufiji ni muhimu sana kwa kutunza mazingira kwani usipotekelezwa wananchi watavamia pori la Selous na kukata miti kwa ajili ya matumizi ya kuni na mkaa na kwamba serikali haiwezi kuwazuia.

“Siwezi kupanga askari kuzuia watanzania wasiende kwenye pori kukata miti wakati hawana umeme,” alisisitiza Rais.

Alizitaka Jumuiya mbalimbali za kimataifa kuelewa kuwa watanzania ni watunzaji wazuri wa mazingira kuliko nchi nyingi duniani na hivyo wasizuiliwe kutekeleza mradi ambao utasaidia kuendelea kutunza mazingira.

Rais alitoa wito kwa watendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kuendelea kuulinda na kuutunza mradi wa umeme wa Makambako – Songea pamoja na miradi mingine mbalimbali ya umeme kwa manufaa ya watanzania na Taifa kwa ujumla.

Awali, akiwasilisha taarifa fupi kuhusu mradi husika, Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani alisema changamoto ya kukatika-katika kwa umeme iliyokuwepo katika Mkoa wa Ruvuma, imepata suluhisho kutokana na uwepo wa mradi huo.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa pamoja na Balozi wa Sweden hapa nchini Anders Sjoberg na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, wakimsikiliza Meneja wa Mradi wa Umeme wa Makambako – Songea, Mhandisi Didas Lyamuya alipokuwa akiwaelezea mradi huo utakavyosambaza umeme katika maeneo mbalimbali kutoka Makambako hadi Songea.

Hata hivyo, alisema changamoto iliyopo sasa ni uwepo wa umeme mwingi unaozidi matumizi ya wananchi hali inayosababisha kuungua kwa baadhi ya vifaa vya wateja.

“Mahitaji ya umeme kwa sasa katika Mkoa wa Ruvuma ni megawati 12.5 na kwa Songea Mjini ni megawati 9.7 tu. Umeme uliokuja sasa ni megawati 48. Matokeo yake umeme umekuwa ukimiminika kwa kasi wakati mahitaji ni madogo,” alisema.

Waziri alisema serikali inafanya utaratibu wa kutatua changamoto hiyo kwa kufunga kifaa kitakachodhibiti umeme uendane na mahitaji ya wananchi.

Pia, alitoa wito kwa wananchi wa Ruvuma kuutumia umeme kwa wingi ikiwemo kuanzisha viwanda na biashara mbalimbali.

Aidha, Waziri alieleza kuwa, katika maeneo ambako Mradi unapita, jumla ya vijiji 122 vitasambaziwa umeme na kuunganisha wateja takribani 22,700. Alisema hadi sasa tayari vijiji 110 na taasisi za umma 114 zimeshaunganishwa na zoezi bado linaendelea.

Akizungumzia umeme vijijini, Dkt. Kalemani alibainisha kuwa hadi sasa vijiji zaidi ya 6,464 vimekwishapelekewa umeme kati ya vijiji 12,268 vilivyopo nchi nzima.

Alipongeza jitihada za serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais Magufuli kwa namna inavyotekeleza mikakati mbalimbali ya kusambaza nishati ya umeme kwa wananchi.

“Mheshimiwa Rais, wakati unaingia madarakani, ulitukuta tuna umeme katika vijiji 2,018. Leo hii tumepeleka umeme katika vijiji 6,414 katika kipindi chako cha miaka mitatu tu.”

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Balozi wa Sweden hapa nchini Anders Sjoberg na Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani, wakielekea eneo la uzinduzi wa mradi wa Ujenzi wa njia kuu wa umeme KV 220 kutoka Makambako hadi Songea pamoja na vituo vya kupooza umeme KV 220/33 katika sherehe zilizofanyika Songea mkoani Ruvuma.

 

Waziri aliwaambia wana-Ruvuma kuwa kupitia mpango wa umeme vijijini, vijiji vyote mkoani humo vitapelekewa umeme na kwamba hadi sasa wakandarasi wameshawasha umeme katika vijiji 56. Alisema vijiji 132 vilivyosalia vitaunganishiwa ndani ya kipindi cha miezi 18 ya mradi iliyosalia.

Kwa upande wake, Balozi wa Sweden hapa nchini, Anders Sjoberg, alieleza kwamba, Mkataba kati ya Serikali za Tanzania na Sweden kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi husika, ulisainiwa mwaka 2008 ambapo Sweden ilitoa Krona milioni 700 sawa na shilingi za kitanzania bilioni 165.

“Tunapoona matokeo haya; tunaweza kuhitimisha kwamba, haya ni mafanikio makubwa, ni uwekezaji mkubwa,” alisema Mheshimiwa Balozi.

Balozi Sjoberg aliipongeza Wizara ya Nishati, TANESCO, REA, Timu ya Ubalozi iliyopo nchini Tanzania pamoja na wahandisi washauri kwa kazi kubwa iliyofanyika.

“Ninajua yote yaliyofanyika ili kukamilisha Mradi huu, yanatufanya tuwe na fahari kubwa.”

Vilevile, Balozi alisema ni matumaini ya Serikali ya Sweden kuwa, ushirikiano kati yake na Tanzania katika kutekeleza Mradi husika, utawezesha wananchi wa Tanzania hasa Ruvuna na Njombe, kufanya kazi kwa bidii na kutumia umeme huo katika kujiletea maendeleo.

Gharama za Mradi wa Umeme wa Makambako – Songea ni sawa na bilioni 216 za kitanzania, ambapo umetekelezwa kwa ushirikiano wa Serikali ya Tanzania na ya Sweden kupitia Shirika la Maendeleo la Sweden (SIDA).

Ilielezwa kuwa kukamilika kwa Mradi huo, kumesaidia kuongeza uwezo wa njia za usafirishaji umeme na kuimarisha hali ya upatikanaji umeme kwa Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kupitia Gridi ya Taifa.

Pia, Mradi umesaidia kupunguza gharama za uendeshaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) baada ya kuzimwa kwa mitambo yote ya mafuta na kuweza kuokoa kiasi cha shilingi bilioni 9.8 kwa mwaka.

Na Veronica Simba – Ruvuma