Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amezindua rasmi biashara ya kuuza na kusambaza mafuta kwa Serikali nchini kwa kufungua   kituo cha kwanza cha kuuza mafuta ya Petroli na Dizeli kitakachosimamiwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kupitia Kampuni yake Tanzu ya Mafuta (TANOIL).

Dkt. Kalemani alisema kuwa kuzinduliwa na kufunguliwa kwa biashara hiyo ni kutimiza azma na nia njema ya Serikali ya kuboresha shirika lake la TPDC, kuwapatia na kuwasogezea karibu wananchi wake huduma ya kupata mafuta yenye viwango vya ubora unaotakiwa, bei nafuu, na yatakayopatikana kwa wingi muda wote.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, akizungumza na wakazi wa Mkoa wa Mara wakati akifungua rasmi kituo cha kuuza mafuta ya dizeli na petroli cha serikali (TANOIL) Juni 06, 2020, wilayani Musoma mkoani Mara.

Alifanya uzinduzi huo pamoja na kufungua kituo hicho wilayani Musoma, mkoani Mara  Juni 6, 2020, wakati wa ziara yake ya kikazi  katika Mkoa huo, akiwa ameambatana na  Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu, Katibu Mkuu Mhandisi Zena Said pamoja na viongozi wengine waandamizi wa wizara na taasisi zilizo chini yake.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akizungumza na wakazi wa Mkoa wa Mara wakati wa ufunguzi wa kituo cha kuuza mafuta ya dizeli na petroli cha serikali (TANOIL). Kituo hicho kilifunguliwa rasmi na Waziri wa Nishati, Dkt. Kalemani, Juni 6, 2020, wilayani Musoma mkoani humo.

Alisema baada ya kuanza rasmi kwa biashara hiyo, TPDC kupitia TANOIL itashirikiana na Halmashauri zote nchini kuhakikisha inafanikisha azma ya Serikali ya kufungua na kuweka vituo vya kuuza na kusambaza mafuta katika kila halmashauri nchini pamoja na miundombinu ya kuhifadhi na kusafirisha mafuta.

Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Zena Said akizungumza na wakazi wa Mkoa wa Mara wakati wa ufunguzi wa kituo cha kuuza mafuta ya dizeli na petroli cha serikali (TANOIL). Kituo hicho kilifunguliwa rasmi na Waziri wa Nishati, Dkt. Kalemani, Juni 6, 2020, wilayani Musoma mkoani humo.

“Tumeshaanza biashara ya kuwauzia wananchi wetu mafuta, sitegemei kusikia mafuta yanauzwa kwa bei ghali katika vituo vya serikali. TPDC na TANOIL mnielewe vizuri hapa!  Lengo letu sisi serikali ni kuhakikisha kuwa wananchi wanapata bidhaa bora za mafuta kwa kiwango kinachotakiwa, kwa bei nafuu na kwa wingi, wakati wote,” alisema Dkt. Kalemani.

Mwonekano wa Kituo cha kuuza mafuta ya petroli na dizeli cha serikali (TANOIL) kitakachosimamiwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kupitia Kampuni ya Mafuta ya TANOIL, kilichofunguliwa na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, Juni 06, 2020 wilayani Musoma mkoani Mara.

Aidha, alibainisha kuwa TPDC na TANOIL watashiriki katika biashara ya uagizaji na usambazaji mafuta kama zinavyofanya kampuni nyingine za mafuta nchini ili kuongeza ushindani na kutanua wigo wa kampuni za kizalendo kushiriki  katika biashara ya mafuta, ambayo kwa sasa inafanywa na  makampuni kutoka nje ya nchi tu.

Alisema kuwa Serikali kupitia TPDC itajenga vituo 100 kwa kipindi cha miaka mitano ijayo, ambapo tayari baadhi ya Halmashauri zimeanza kutenga maeneo yatakayojengwa vituo hivyo. Aidha, Serikali itahakikisha kuwa nusu ya mafuta yote yanayoingizwa nchini yanasimamiwa TPDC.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (kushoto) na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima wakijadiliana jambo wakati wa ufunguzi wa kituo cha kuuza mafuta ya dizeli na petroli cha serikali (TANOIL). Dkt. Kalemani alifungua kituo hicho Juni 06, 2020, wilayani Musoma mkoani Mara.

“Watanzania tutembee kifua mbele na kujivunia vilivyo vya kwetu. Uzinduzi wa biashara hii ya mafuta hapa Musoma leo unaofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano, ya Uongozi wa Rais Dkt. John Magufuli, ni kutambua juhudi na mchango mkubwa wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika kuimarisha sekta ya Umma ya kukuza uchumi.”

Alisema Watanzania hawana budi kutambua mchango wa Mwalimu kuanzisha TPDC mwaka 1969 pamoja na kiwanda cha kusafisha mafuta cha TIPER mwaka huohuo, ambapo TPDC ilimiliki kiwanda hicho kwa asilimia 50%. “Mwalimu aliona na kuwaza mbali sana, yote ikiwa ni katika dhana ya kujitegemea kiuchumi,” alisisitiza Dkt. Kalemani.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Dkt. James Mataragio akizungumza na wakazi wa Mkoa wa Mara wakati wa ufunguzi wa kituo cha kuuza mafuta ya dizeli na petroli cha serikali (TANOIL). Kituo hicho kilifunguliwa rasmi na Waziri wa Nishati, Dkt. Kalemani, Juni 6, 2020, wilayani Musoma mkoani humo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dkt. James Mataragio alisema kuwa katika kutekeleza azma hiyo ya serikali, kuanzia mwaka wa fedha 2020/2021, TPDC imetenga fedha za kutosha kwa ajili ya mtaji wa kugharamia shughuli za uagizaji, usambazaji na usimamizi wa mauzo ya mafuta nchini kote.

Alisema kwamba TANOIL imejipanga kuhakikisha kunakuwa na usalama wa usambazaji mafuta nchini, kunapatikana takwimu sahihi za mafuta, bei na viwango stahiki vya ubora pamoja na uelewa mzuri na mpana wa biashara ya mafuta nchini.

“Nina furaha sana leo TPDC inaandika historia mpya na kubwa sana katika nchi yetu. Tunaungana na wakazi wa Mkoa wa Mara, kwa niaba ya Watanzania wote kuonesha furaha yetu katika kuandika historia hii mpya ya kwamba shirika letu linarudi kwa kishindo katika biashara ya kuuza na kusambaza mafuta na bidhaa zake kwa maslahi yetu sote na taifa kwa ujumla.

Alieleza zaidi kuwa mwaka 2000, Serikali ilifanya maamuzi ya kuendesha biashara ya mafuta nchini kwa mfumo wa soko huria, hivyo TPDC ikaunda kampuni tanzu ya COPEC kuweza kuingia katika mfumo huo na kushiriki katika soko la ushindani katika biashara hiyo.

TPDC ilinunua na kujenga vituo mbali mbali nchini vikiwemo Segera na Muheza Mkoani Tanga, Makuyuni na Makumira Mkoani Arusha, Singida, Geita pamoja na Mara ambapo vilinunuliwa vituo viwili tu cha Musoma na Tarime. Alisema vituo vyote hivyo vinamilikiwa na TPDC kwa asilimia 100.

Alizidi kufafanua kuwa TPDC ilishiriki katika biashara hiyo kupitia katika vituo hivyo lakini kukosekana kwa sheria madhubuti ya Mafuta/Petroli, kulififisha ushiriki wake katika soko lenye ushindani mkubwa.

Alisema, baada ya kufanyika michakato na mapitio ya rejea na maboresho mbalimbali ya shirika hilo kumewezesha uwepo wa sheria madhubuti, pamoja na usimamizi wa kanuni mbalimbali, ambazo sasa zinaiwezesha TPDC kuingia katika soko kwa ufanisi zaidi.

Mataragio alieleza kuwa katika mwaka huu wa fedha, TPDC itakamilisha ujenzi wa vituo viwili katika Mkoa wa Singida na Mkoa wa Geita. Aidha, alisema kuwa shirika hilo linaendelea na mkakati wa kutwaa ardhi katika mikoa ya Dar es salaam, Tanga, Dodoma na Morogoro kwa ajili ya kuendeshea biashara hiyo.

“Natumia fursa hii kwa niaba ya TPDC kutoa shukrani zetu za dhati kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Nishati unayoiongoza wewe Dkt. Kalemani kwa umahiri, kwa maelekezo na rasilimali fedha zinazoiwezesha TPDC sasa kuingia katika biashara hii.”

Pia, alitoa shukrani kwa uongozi wa Serikali ya Mkoa wa Mara kwa ushirikiano waliotoa katika kipindi chote tangu enzi za COPEC hadi sasa TANOIL na kufungua ukurasa mpya wa mafanikio ya uzinduzi wa biashara ya mafuta.

Naye Mkuu wa Mkoa, Adam Malima, aliwaasa wakazi, wafanyabiashara na watumiaji wa mafuta ya Petroli na Dizeli kuunga mkono juhudi za serikali za kuanzisha bishara ya mafuta kwa kununua mafuta katika vituo vya serikali.

Sambamba na hilo, alisema kuwa kutokana na mikakati iliyowekwa na Serikali kupitia Wizara ya Nishati kufikisha huduma ya mafuta hayo karibu na wananchi, kutawaweka katika mazingiza salama na rafiki watumiaji wa mafuta hayo hasa waendesha bodaboda na wafanyabiashara wadogo.

“Wafanyabiashara wadogo wanaowauzia waendesha bodabora na vyombo vingine vidogo vinavyotumia mafuta hayo, wamekuwa wakihifadhi bidhaa hiyo katika hatari kubwa ya kupoteza maisha na mali zao, wanatumia vifungashio duni kama galoni na chupa za maji. Hii itaondoa kabisa hatari iliyopo katika jamii yetu hasa vijijini,” alisema Malima.

Historia inatuonesha kwamba katika miaka ya 80 hadi kufikia Mwaka 2000, TPDC licha ya biashara yake kuu ya utafutaji, uchimbaji, uendelezaji na usambazaji wa gesi asilia, ilikuwa muagizaji, muingizaji na msambazaji mkuu wa mafuta yote yaliyotumika nchini.

TPDC iliingiza mafuta ghafi nchini na kuyasafisha, na pia uingizaji wa ziada ya mafuta yaliyosafishwa na kutosheleza mahitaji ya mafuta nchini.

Pia TPDC ilibeba jukumu hilo kwa ufanisi na uzalendo wa hali ya juu, ikiwemo kuwa msambazaji pekee aliyesambaza mafuta mstari wa mbele wakati wa vita vya Kagera kati ya Mwaka 1977/78 baada ya kampuni binafsi kugoma kupeleka mafuta Kagera.

Zuena Msuya – Mara