SERIKALI YAJIPANGA KUHAKIKISHA NISHATI YA MAFUTA INAPATIKANA MUDA WOTE

Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani, amekutana na kufanya mazungumzo na wadau wa mafuta nchini kujadili hatua ambazo nchi itazichukua endapo uhaba wa mafuta utajitokeza katika kipindi hiki cha mlipuko wa maradhi ya Virusi vya Corona.

Mazungumzo hayo yalifanyika Machi 17, 2020 jijini Dar es Salaam, katika ofisi za Wakala wa Uagizaji Mafuta Kwa Pamoja ( PBPA)  na kuhudhuriwa na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Mhandisi Zena Said, Naibu Katibu Mkuu Mhandisi, Leonard Masanja, Kamishina wa Petroli na Gesi, Adam Zuberi, viongozi mbalimbali wa Taasisi za Wizara ya Nishati na wadau mbalimbali wa mafuta nchini.

Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Zena Said,  akizungumza kwenye kikao kati ya Waziri wa Nishati na wadau mbalimbali wa Mafuta nchini, kilichofanyika jijini Dar es Salaam, Machi 17,2020. Kulia ni Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani, na kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Mhandisi Leonard Masanja.

Waziri wa Nishati alisema kuwa, Serikali ilipanga kukutana na wadau hao ili kuona namna bora ya kuhakikisha mafuta yatapatikana muda wote kulingana na mahitaji ya nchi, endapo itatokea dharura yoyote kwenye nchi ambazo wafanyabiashara wananunulia mafuta..

“ Sisi kama Serikali pamoja na wadau ni jukumu letu kuhakikisha kwamba mafuta yanapatikana muda wote tena ya kutosha kuendesha shughuli zenu wafanyabiashara lakini na kuendesha shughuli za Serikali pamoja na shughuli za kijamii.” Alisema

Aliongeza kuwa, nchi inajenga miradi mingi mikubwa ya kimaendeleo na kiasi kikubwa miradi hiyo inategemea sana uwepo wa mafuta katika utekelezaji wake.

Aliongeza kuwa, nchi ambazo Tanzania inanunua mafuta, mpaka sasa bado wanaendelea na uzalishaji  wa mafuta na bado hawajafunga mipaka yao, lakini kwa upande wa Serikali lazima ichukue  hatua madhubuti kwa kushirikiana na wadau wake ili kuweza kujihakikishia mafuta ya kutosha nchini.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (wa kwanza kushoto), Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Mhandisi Zena Said (katikati) na Naibu Katibu Mkuu, Mhandisi Leonard Masanja wakiwa pamoja na wadau mbalimbali wa mafuta (hawapo pichani) kujadili hatua ambazo nchi itazichukua endapo uhaba wa mafuta utajitokeza katika kipindi cha mlipuko wa maradhi ya Virusi vya Corona, jijini Dar es Saalam, Machi 17, 2020.

Dkt. Kalemani aliwatoa wasiwasi watanzania na kueleza kwamba mafuta yapo ya kutosha ambayo yatatosheleza mpaka miezi miwili ijayo na Serikali  itajipanga zaidi ili kuwa na mafuta ya siku nyingi zaidi.

Nao, wadau wa mafuta nchini, waliipongeza Serikali kwa kitendo cha kuwaita ili kuzungumzia suala hilo ambalo limejikita katika kuchukua tahadhari katika kipindi ambacho dharura itajitokeza na kuahidi kuwa wapo tayari kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha mafuta nchini yanapatikana muda wote.

Hafsa Omar- Dar es Salaam