Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amesema Serikali itawachukulia hatua kali wafanyabiashara wa mafuta nchini, wanaoficha bidhaa hiyo ili wayauze kwa bei kubwa hapo baadaye, hali inayosababisha usumbufu mkubwa kwa watumiaji wake.

Alitoa kauli hiyo Juni 15, 2020 jijini Dodoma, katika mkutano wake na waandishi wa habari.

Alisema, kumekuwepo na taarifa za baadhi ya wafanyabiashara wakubwa wa mafuta kutotaka kuuza bidhaa hiyo kwa sababu bei elekezi ziko chini kwa sasa, wakisubiri bei zipande ili wapandishe bei na kuwaumiza Watanzania. Waziri amesisitiza kuwa kamwe Serikali haitaruhusu jambo hilo.

“Natoa rai kwa wafanyabiashara wa mafuta ya aina zote nchini ikiwemo petroli, dizeli na mafuta ya taa waache kuficha mafuta. Yeyote tutakayemkamata akificha mafuta, tutamchukulia hatua kali sana za kisheria na kiutawala,” alisisitiza.

Katika kuhakikisha hatua stahiki zinachukuliwa, Waziri alitoa maelekezo kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) pamoja na Wakala wa Uagizaji Mafuta Kwa Pamoja (PBPA), kuendesha msako kwa wote wanaoficha mafuta ili kuwabaini na kuwachukulia hatua chini ya Sheria ya EWURA.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) katika ofisi za Wizara Dodoma, akiwaonya baadhi ya wafanyabiashara wa mafuta ya Petroli, Dizeli na Taa, kuacha tabia ya kuficha bidhaa hiyo. Mkutano huo ulifanyika Juni 15, 2020.

Akifafanua, alisema Sheria ya EWURA imeainisha adhabu za aina mbili kwa watakaobainika kutenda kosa la aina hiyo, akizitaja kuwa faini isiyopungua shilingi milioni 100 pamoja na muhusika kufungiwa biashara yake.

Alitoa tahadhari kwa wafanyabiashara wa mafuta akiwataka wakumbuke kuwa wanatoa huduma kwa wananchi, hivyo ni lazima wazingatie masharti ya leseni zao.

“Nawataka watoe huduma na kufanya biashara pasipo kuathiri mapato ya Serikali wala kuathiri upatikanaji wa mafuta kwa walaji.”

Katika hatua nyingine, Waziri aliwataka wafanyabiashara hao kuendelea kuleta mafuta huku akiwataka wananchi kuondoa shaka juu ya kiwango cha akiba ya bidhaa hiyo kilichopo nchini, akisema ni toshelevu.

“Tunayo akiba kubwa sana ya matanki yetu hapa nchini inayoweza kufikia lita bilioni 1.2 na tunaweza kuitumia kwa muda wa miezi mitatu ijayo. Mahitaji yetu kwa muda huohuo ni lita milioni 750 tu, kwahiyo uwezo wetu wa kuhifadhi mafuta ni mkubwa kuliko mahitaji yetu,” alifafanua.

Akizungumzia mchango wa Bandari zilizopo nchini katika suala hilo, Dkt Kalemani alisema kuwa lengo la kuanzishwa kwa Bandari hizo zilizopo Dar es Salaam, Tanga na Mtwara ni pamoja na kusogeza huduma kwa wananchi ili kila kona ya nchi iweze kupata huduma husika kwa urahisi, kwa haraka na gharama nafuu.

Alitoa wito kwa wafanyabiashara na wenye matumizi ya bandari, kuhakikisha wanatumia utaratibu wa bei linganifu ili wananchi pia wafaidi uwepo wa bandari hizo nchini.

Alisema rai hiyo inakwenda sambamba na agizo kwa wafanyabiashara wote wa mafuta, kuhakikisha bei ya mafuta kwa watumiaji inaendelea kushuka kwani katika Soko la Dunia, bei ingali inashuka.

“EWURA lazima mzingatie hili. Akipatikana mfanyabiashara wa kituo cha mafuta anauza bei tofauti na bei elekezi ya Serikali, huyo akamatwe mara moja. Lazima tuhakikishe kushuka kwa bei kunawanufaisha Watanzania.”

Aidha, Waziri alizungumzia suala la upelekaji nishati vijijini, akisisitiza kwamba kwa upande wa umeme, Serikali imepata mafanikio makubwa kiasi cha kushika nafasi ya kwanza Afrika kwa usambazaji umeme vijijini.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (katikati), akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) katika ofisi za Wizara Dodoma, akiwaonya baadhi ya wafanyabiashara wa mafuta ya Petroli, Dizeli na Taa, kuacha tabia ya kuficha bidhaa hiyo. Mkutano huo ulifanyika Juni 15, 2020. Kulia ni Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu na kushoto ni Naibu Katibu Mkuu, Mhandisi Leonard Masanja.

Hata hivyo, alitanabaisha kuwa, nishati siyo umeme peke yake, hivyo akatoa msukumo kwa Mamlaka zinazohusika kuhakikisha mafuta na gesi pia zinafikishwa kwa wananchi walioko vijijini.

Alisema kwa upande wa gesi, tayari zoezi la kupeleka vijijini limeanza kwa kufikisha nishati hiyo Lindi vijijini na kwa upande wa mafuta, alisema EWURA wanakamilisha taratibu za kuanzisha Mradi wa Kielelezo unaolenga kuanzisha vituo vya mafuta vya gharama nafuu vijijini.

Aliitaka EWURA kuhakikisha ndani ya miezi sita Mradi huo uwe umeanza kutekelezwa kwa kuanza kuruhusu ufunguzi wa vituo vidogo vidogo na huduma tembezi za kuuza mafuta vijijini ili wananchi wa maeneo hayo wanufaike.

Akifafanua zaidi, Waziri alisema endapo Mradi huo wa Kielelezo utaonesha mafanikio, Serikali itaanzisha miradi ya aina hiyo katika maeneo mengi zaidi lakini ikijikita katika maeneo yasiyofikika kwa urahisi kutokana na miundombinu isiyo rafiki, visiwani na katika maeneo tengefu.

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, Naibu Katibu Mkuu Mhandisi Leonard Masanja, Kamishna wa Petroli na Gesi, Adam Zuberi pamoja na viongozi waandamizi kutoka EWURA.

Veronica Simba na Zuena Msuya – Dodoma