Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani ametoa siku tano kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kulipa fidia kwa wananchi wa Kidahwe, Kigoma Vijijini, mkoani Kigoma, waliopisha ujenzi wa kituo cha kupoza umeme.

Alitoa agizo hilo Juni 27, 2020, wakati akizindua kuanza malipo kwa wananchi ambao wameridhia kutoa ardhi yao kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho cha kupoza umeme cha Kidahwe.

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kidahwe, Kigoma Vijijini, mkoani Kigoma, akiwa kwenye uzinduzi wa kuanza malipo kwa wananchi ambao wameridhia kutoa ardhi yao kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha Kupoza umeme cha Kidahwe, Juni 27, 2020.

Akizungumza kwenye tukio hilo, Waziri alisema kuwa, zaidi ya shilingi milioni 700 zipo tayari kwa ajili ya malipo ya wananchi 411 na kuitaka TANESCO kuanza mara moja kuwalipa wananchi hao.

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (kushoto) akiwa pamoja na Uongozi wa Mkoa wa Kigoma na baadhi ya wananchi wa kijiji cha Kidahwe, wakiwa wameshika mfano wa hundi itakayolipwa kwa wananchi wa kijiji hicho kilichopo kata ya Kidahwe, Kigoma Vijijini, Juni 27, 2020. Malipo hayo ni kufuatia kutoa ardhi walizokuwa wakimiliki ili kupisha ujenzi wa kituo cha kupoza umeme Kidahwe.

“Niliacha maelekezo kwa waatalamu wetu kufanya kazi mbili, kazi ya kwanza ilikuwa kuhakikisha wananchi ambao wanapitiwa na mradi, wafanyiwe tathmini na kulipwa fidia zao. Jambo hili tayari limeanza kufanyiwa kazi. La pili ni kuanza matayarisho ya ujenzi wa mradi huu mkubwa,” alisema Dkt Kalemani.

Aidha, Waziri aliwashukuru wananchi wa eneo hilo kwa kutoa maeneo yao kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho kikubwa  chenye uwezo wa kuzalisha umeme wa kilovoti 400, ambao  unatarajiwa kuondoa kero ya upatikanaji wa umeme mkoani humo.

Aliwataka wananchi watakaolipwa fidia hiyo kuzitumia vizuri fedha zao kwa kununua maeneo mengine na kujiendeleza kiuchumi.

“Mtakaolipwa fedha zenu, msije mkazitumia vibaya halafu mkarudi tena TANESCO kudai hela nyingine. Hakuna hela nyingine. Ni hiyohiyo mtakayolipwa,” alisema.

Vilevile, alilitaka shirika hilo la ugavi wa umeme, kuanzia Julai 5 mwaka huu, lianze mara moja ujenzi wa kituo hicho, ili wananchi wa Kigoma waanze kupata umeme wa uhakika ambao utawasaidia kujenga uchumi wa Mkoa huo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Emmanuel Maganga, aliwashukuru wananchi wote waliotoa maeneo yao kwa ajili ya maendeleo ya Mkoa huo na aliwahakikishia kuwa pesa za malipo yao ziko tayari.

Pia, aliwatahadharisha wale wote watakaolipwa fidia kuwa hawataruhusiwa kuyatumia tena maeneo hayo kwani yatakuwa ni mali ya Serikali.

Katika ziara hiyo, Waziri Kalemani pia alikagua kituo cha kupoza umeme cha Nguruka kilichopo katika kijiji cha Mganza na kuielekeza TANESCO kumaliza ujenzi wa kituo hicho Julai mwaka huu.

Hafsa Omar – Kigoma