Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Zena Said amewataka watu wote wanaomiliki mali za serikali kiujanjaunja na kinyume cha sharia na utaratibu wazirudishe katika mamlaka husika ili ziwanufaishe watanzania wote na serikali kwa ujumla.

Mhandisi Zena alisema hayo, June 02, 2020, wakati wa makabidhiano ya Maghala( Godown) matatu kwa Shiriki la Maenedeleo ya Petroli ( TPDC) yaliokuwa yametwaliwa na kumilikiwa kinyume cha utaratibu na kampina ya SACCOSSA kuanzia mwaka 2006.

Mhandisi Zena alisema hayo ni matokeo ya Tume iiliyoundwa na TPDC kuhakiki mali zake pia ni muendelezo wa zoezi la kurudisha mali za serikali zilizotwaaliwa au kumilikiwa kiujanja ujanja na  kinyume na utaratibu wa Kisheria ili zirudishwe serikalini katika mamlaka husika.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Zena Said, akizungumza na vyombo vya habari, Juni 2, 2020, wakati wa kukabidhi maghala ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini, (TPDC) yaliyokuwa yametwaaliwa na kampuni ya SACCOSSA tangu 2006.

Maghala hayo yaliorudishwa kwa TPDC, yapo katika eneo la Mikocheni Jijini Dar es salaam, ambapo Kampuni ya SACCOSSA awali waliingia makubalino na TPDC ya kuyatumia maghala hayo katika shughuli zake, baadaye kampuni hiyo ilienda kinyume cha makubaliano ya mkataba kwa kutokulipa fedha ya pango huku ikiendelea kuyamiliki na kuyatumia majengo hayo pasipo kunufaisha mamlaka husika na Serikali kwa ujumla.

“Baadhi ya watu kujimilikisha mali za serikali kiujanjaujanja kwa muda mrefu huku serikali ikiwa haifaidiki, sasa kuna haja ya kurudisha mali hizo serikalini moja baada ya nyingine, jana tu tumeshuhudia mali za mkonge zikirudishwa kule Tanga, sisi leo tunarudisha hizi za TPDC na si hizi tu, tutarudisha mali zote za Wizara ya Nishati na Taasisi zilizo chini zake, natoa wito kwa yeyote anayemiliki mali kinyume na taratibu aanze kuzirejesha mwenyewe”, Alisema Mhandisi Zena.

Akizungumzia makubalino katika ya TPDC na SACCOSSA, Mhandisi Zena alisema kuwa kampuni ya SACCOSSA ilikuwa mpangaji katika majengo hayo kuanzia miaka ya 2000 na walikuwa wakilipa pango vizuri kwa muibu wa mkataba, ilipofika mwaka 2006, kampuni hiyo iliacha kulipa fedha hiyo ya pango huku wakiendelea kuyamiliki na kuyatumia bila kulipa chochote kwa zaidi ya miaka kumi hivyo kuleta mgogoro baina yao.

Alifafanua kuwa baada ya usuluhishi wa mgogoro huo, na TPDC kushinda kesi, SACCOSSA iliamuliwa kurejesha majengo hayo ili yatumie na mamlaka husika, Hata hivyo, Katibu Mkuu huyo aliiagiza kampuni hiyo ya SACCOSSA kulipa fedha za pango walizokuwa hawalipi katika kipindi chote hicho, licha ya kulikabidhi katika mamlaka husika.

“SACCOSSA lazima mlipe fedha mnazodaiwa kwa mujibu wa makubaliano hata kama mmerudisha jengo hili, Serikali hii ina mali nyingi sana lakini wajanja wachache wamekuwa wakizitumia kwa faida zao binafsi na serikali hainufaiki, lakini sasa hivi mali hizi zimeanza kurudishwa na tumeshaona mifano mingi,zoezi hili litaendelea nchi nzima, lazima watanzania wote wanufaike na wajivunie mali za serikali yao, na sio kwa mikono ya watu walio wachache tu”,alisisitiza Mhandisi Zena.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Dkt. James Mataragio,akionyeha hati ya makabidhiano ya kurudishwa kwa maghala matatu ya shirika hilo, yaliyokuwa yametwaaliwa na Kampuni SACCOSSA kwa zaidi ya miaka 10, tangu 2006.tukio hilo lilifanyika Juni 02,2020.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dkt. James Mataragio, alisema kuwa urudishwaji wa majengo hayo ni matokeo ya maagizo na maelekezo ya rais dkt. John Magufuli ya kutaka mali zote za serikali ambazo umiliki wake haufahamiki au kuhamishiwa kwa watu wengine bila kufuata taratibu zihakikiwe na kurudishwa serikalini katika mamlaka husika.

Dkt. Mataragio alisema kuwa baada ya maagizo hayo iliundwa timu ya ndani ya kuhakiki mali zote za shirika hilo na kufanya kazi nzuri iliyotoa taarifa/ripoti iliyoanisha mali za shirika hilo inazozimili kisheria, zisizomilikiwa kisheria pamoja na zile zenye migogoro na kuanza kuzishughulikia.

“Tume hii iliyoundwa imefanya kazi nzuri sana, tunaendelea kufanyia kazi taarifa/ripoti ya iliyoletwa na tume hiyo kwa utekelezaji wenye manufaa kwa shirika na Taifa kwa ujumla, nawahakikishia kuwa mali zote za TPDC zitaendelea kuwa salama na katika umiliki sahihi kwa faida yetu sote watanzania, sababu hili ni shirika letu lazima tujivunie nalo”, Alisema Dkt. Mataragio.

Naye muwakilishi wa kampuni ya SACCOSSA, Donashan Kambamba Alisema kuwa, kampuni hiyo iliridhia kuundwa kwa tume hiyo na kukubali na taarifa ya matokeo ya tume hiyo na kuriidhia kurejesha jengo hilo kwa mamlaka husika.

Kuhusu kulipa fedha wanazodaiwa kama walivyoagizwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Zena Said, Kambamba alisema kuwa watakaa na kukubaliana na TPDC kuona namna bora na kutekeleza agizo hilo.

Na Zuena Msuya DSM