Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amesema Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuwafikishia huduma ya umeme watanzania wote bila kubagua aina ya makazi yao na kwamba itaendelea kutekeleza jukumu hilo pasipo kukatishwa tamaa na yeyote.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akiwa ameshika taa ya Chemli na Kibatari, alizokabidhiwa na mkazi wa kijiji cha Misongeni wilayani Muheza (kulia kwa Naibu Waziri); baada ya kumuwashia rasmi umeme katika nyumba yake, Machi 29, 2019 akiwa katika ziara ya kazi.

Aliyasema hayo jana, Machi 29, 2019 akiwa katika ziara ya kazi wilayani Muheza, ambapo aliwasha umeme katika vijiji vya Mamboleo-Lusanga, Mamboleo-Nkumba na Misongeni. Vilevile, alikagua genge la Mkandarasi anayetekeleza miradi ya umeme vijijini wilayani humo pamoja na kuzungumza na wananchi.

Naibu Waziri alisema kumekuwepo na maneno ya baadhi ya watu kubeza jitihada zinazofanywa na Serikali kuwaunganishia umeme watanzania wote hususani waishio vijijini pasipo ubaguzi, wakitoa sababu kwamba wenye nyumba za nyasi hawastahili kupatiwa huduma hiyo.

Akifafanua, alisema kuwa, wataalamu wa serikali wamekuwa wakihakikisha taratibu za usalama zinafuatwa wakati wa kuunganisha umeme katika nyumba za vijijini, hususani zilizoezekwa kwa makuti au nyasi.

Aliwataka wananchi kuondoa hofu kuwa madhara yanaweza kutokea katika nyumba za aina hiyo ambazo zimeunganishiwa umeme na badala yake wawapuuze watu wanaobeza jitihada hizo, na zaidi wautumie umeme kujiletea manufaa katika maisha yao.

Pia, Naibu Waziri alieleza kuwa, kazi ya kuwapelekea wananchi wa vijijini umeme inafanyika sambamba na zoezi la uhamasishaji wa kujenga makazi bora. Alisema, mwananchi mwenye makazi duni akiunganishiwa umeme, anapata hamasa ya kuboresha zaidi makazi yake na hilo limekuwa likifanyika sehemu mbalimbali nchini kote.

“Maelekezo yetu kwa wakandarasi ni kutobagua nyumba ya aina yoyote. Watanzania wote wanahitaji umeme pasipo ubaguzi wa aina yoyote. Hakuna sababu ya mtu aliye karibu na miundombinu, halafu asiunganishiwe umeme,” alisisitiza.

Baadhi ya wananchi wenye nyumba zilizoezekwa kwa makuti wilayani Muheza na ambao wameunganishiwa umeme, akiwemo Musa Rashidi, mkazi wa kijiji cha Mamboleo, waliipongeza Serikali na kutoa shukrani nyingi kwa kuwapatia huduma ya umeme pasipo kuwabagua. Waliahidi kuboresha zaidi makazi yao.

“Naishukuru sana Serikali kwa kuniunganishia umeme katika nyumba yangu, maana kabla ya huduma hii, hali haikuwa nzuri hapa nyumbani. Nimefarijika sana,” alisema Musa.

Awali, akizungumza na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo, ofisini kwa Mkuu wa Wilaya, Naibu Waziri alisema suala la kukatika-katika kwa umeme wilayani humo linatokana na njia inayotumika kusafirisha umeme, yenye msongo wa kilovoti 132 kuzidiwa nguvu kutokana na matumizi kuongezeka.

“Ndiyo maana serikali ikaja na mpango wa kujenga njia nyingine ya umeme yenye uwezo wa kilovoti 400 kutoka Kinyerezi – Kibaha – Chalinze – Segera hadi Tanga ili kuboresha hali ya upatikanaji umeme mkoani humu,” alisema Naibu Waziri.

Aidha, Naibu Waziri aliuagiza uongozi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), mkoani Tanga na nchi nzima kwa ujumla, kuboresha utoaji taarifa kwa viongozi na wananchi.

Aliwataka kutoa taarifa kwa wakati kunapokuwa na ratiba ya kukatika kwa umeme, ikiwa ni pamoja na kueleza umeme utakatika muda gani, kwa sababu gani, maeneo yatakayoathirika pamoja na hatua zinazochukuliwa kutatua tatizo husika.

Vilevile, aliwataka wananchi wa Mkoa wa Tanga, ambao wana utamaduni wa kuchoma moto maeneo mbalimbali kwa ajili ya kilimo, kuchukua tahadhari ili kutoathiri miundombinu ya umeme.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (wa pili-kulia) akimpa mkono wa pongezi mkazi wa kijiji cha Mamboleo-Nkumba, wilayani Muheza, Musa Rajabu, baada ya kumuwashia rasmi umeme katika nyumba yake, Machi 29, 2019 akiwa katika ziara ya kazi. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Mhandisi Mwanaasha Tumbo na wa pili-kushoto ni Mbunge wa Muheza, Adadi Rajabu.

“Natoa rai kwa wananchi, unapohujumu miundombinu ya umeme ni kosa kisheria maana ni uhujumu uchumi. Na mkumbuke, serikali inatumia gharama kubwa kuwekeza katika miundombinu husika.”

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Mhandisi Mwanaasha Tumbo, alimweleza Naibu Waziri kuwa Wilaya hiyo imekuwa ikipata matatizo ya kukatika umeme mara kwa mara.

Naye Mbunge wa Jimbo la Muheza, Adadi Rajabu (CCM), alisema umeme wa REA umekuwa ni jambo la kufurahisha kiasi kwamba wale ambao hawajafikiwa na huduma hiyo wanalalamika. Hivyo, alimwomba Naibu Waziri kusimamia suala hilo ili vijiji na vitongoji ambavyo havijafikiwa, vipelekewe umeme mapema.

Taarifa ya TANESCO wilayani Muheza inabainisha kuwa; vijiji 87 kati ya 135 vya Wilaya hiyo tayari vina umeme ambapo ni sawa na asilimia 64. Mradi wa REA III Mzunguko wa I ukikamilika mwishoni mwa Juni mwaka huu, asilimia 75 ya vijiji vya wilaya husika vitakuwa na umeme.

Na Veronica Simba – Muheza