Lengo
Kusimamia Uundwaji wa mazingira wezeshi kwa ajili ya kutoa huduma za nishati za kisasa ambazo ni salama, madhubuti, za gharama nafuu, zenye ufanisi, na rafiki wa mazingira.
Majukumu
(i) Kuandaa sera, mipango na programu zinazohusiana na umeme, nishati mbadala na matumizi bora ya nishati, ili kuhakikisha ufanisi, gharama sahihi, huduma bora na za uhakika, katika mazingira rafiki.
(ii) Kukuza ufanisi na matumizi endelevu ya rasilimali za nishati.
(iii) Kutambua uwezo wa nishati nchini na kutengeneza mazingira bora ya kuvutia uwekezaji katika ukuzaji, utoaji na utumiaji wa rasilimali za nishati;
(iv) Kubuni mazingira wezeshi ili kuvutia ushiriki wa sekta binafsi na kuwezesha usambazaji wa uhakika wa nishati ya umeme;
(v) Kutengeneza mazingira bora ya uagizaji na uuzaji wa umeme;
(vi) Kuongoza uchunguzi wa ajali na majanga na kutoa mapendekezo;
(vii) Kupanga, kukuza, kuratibu na kusimamia mipango ya upatikanaji wa huduma ya nishati ya kisasa katika maeneo ya vijijini;
Kitengo hiki kitaongozwa na Kamishna na kitakuwa na sehemu tatu (3) kama ifutavyo:-
(i) Umeme;
(ii) Nishati Mbadala
(iii) Maendeleo ya Nishati.
Umeme
Majukumu ya sehemu ya Umeme ni kama ifuatavyo:-
(i) Kusimamia utendaji wa sekta ya umeme na taasisi zinazojishughulisha na ufuaji, usafirishaji, na usambazaji wa umeme;
(ii) Kusimamia na kuratibu maendeleo na matumizi ya rasilimali za umeme;
(iii) Kuanzisha na kutekeleza miradi ya ukuzaji sekta ya umeme nchini;
(iv) Kuunda na kusimamia utaratibu wa marekebisho katika sekta ya umeme;
(v) Kufanya tafiti zinazohusiana na usambazaji wa umeme na kutoa ushauri;
(vi) Kukadiria na kuchanganua athari zitokanazo na ajali au majanga yatokanayo na shughuli za usambazaji umeme kwa kushirikiana na mamlaka husika;
(vii) Kuratibu biashara ya umeme katika mkoa na kutekeleza miradi ya usafirishaji umeme pamoja na miradi ya uzalishaji.
Sehemu hii itakuwa chini ya Kamishna Msaidizi.
Nishati Mbadala
Sehemu hii itakuwa na majukumu yafuatayo:-
(i) Kutoa ushauri katika sera sahihi na miongozo muhimu ya kufwatwa kwa matumizi sahihi na maendeleo ya rasilimali za nishati mbadala;
(ii) Kukuza na kuratibu nishati mbadala, na kufwata hatua sahihi katika shughuli zote kwenye ngazi ya Taifa, Mkoa, na Kimataifa;
(iii) Kuwezesha hatua na utekelezaji wa mipango na mikakati ya nishati mbadala na ufanisi wa nishati hiyo;
(iv) Kuwezesha ukuaji wa vyanzo vipya vya uzalishaji umeme kama mini hydro, biomasi na umeme wa jua kwa ajili ya mifumo iliyoko nje ya gridi;
(v) Kufanya tathmini ya rasilimali za nishati mbadala na kuandaa, na kuainisha maeneo ya rasilimali za nishati mbadala;
(vi) Kuwezesha ukuaji, kukuza na kusimamia viwango na kanuni kwa matumizi bora zaidi ya nishati katika sekta zote za kiuchumi
(vii) Kukuza na kusimamia, matumizi ya nishati, ufwatiliaji,uhakiki, taratibu na mbinu za utoaji taarifa;
(viii) Kufanikisha ushindani wa biashara kwa kukuza ufanisi wa nishati katika viwanda ili kupunguza gharama za uendeshaji;
(ix) Kuendesha tafiti zinazohusu nishati mbadala, na ufanisi wa nishati pamoja na kutoa ushauri pale unapohitajika;
(x) Kukuza uzalishaji na matumizi endelevu ya biomasi.
Sehemu hii itakuwa chini ya Kamishna msaidizi.
Maendeleo ya Nishati
Sehemu hii itakuwa na majukumu yafuatayo:-
(i) Kuandaa na kupitia sera , sheria, kanuni, miongozo, viwango vya kiufundi, na vigezo kulingana na muundo wa udhibiti wa Umeme na Nishati mbadala;
(ii) Kutengeneza mpango mkakati ili kuongeza ufanisi katika sekta ya Umeme na Nishati mbadala;
(iii) Kuratibu maandalizi ya mpango mkuu wa Mfumo wa nishati kwa ajili ya sekta ya Umeme ikiwa ni pamoja na kuainisha mahitaji, njia za usambazaji, kwa kuzingatia mifumo ya uwekezaji na fedha.
(iv) Kuratibu mapitio ya mipango ya taasisi zilizopo katika sekta ya umeme ili kukuza njia za ushirikiano katika kuandaaa na kutekeleza Sera ya Taifa ya nishati inayohusiana na umeme;
(v) Kutambua madhaifu na kupendekeza hatua stahiki ili kuhakikisha usambazaji wa umeme wa uhakika, dhabiti, na wa gharama stahiki kwa ajili ya kuboresha utendajiwa sekta ya Umeme;
(vi)Kufanya tafiti za rasilimali za nishati ya umeme ikiwa ni pamoja na uzalishaji umeme kwa nyuklia, na pia kutoa mwongozo wa kutoa maamuzi yanayohusu mwelekeo wa sekta ya Umeme na Nishati mbadala;
(vii) Kukuza na kuwezesha ushiriki wa mashirika binafsi katika sekta ya umeme kupitia Sheria ya ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP), pia kuboresha muundo wa udhibiti ili kukuza uwekezaji wa kasi katika miradi ya umeme na nishati mbadala.
(viii) Kuandaa na kuweka taarifa mpya katika kanzidata ya nishati ya umeme na kutoa ripoti zenye taarifa na takwimu kuhusu umeme na Nishati mbadala
(ix) Kukusanya, kupitia, na kuchanganua takwimu zinazohitajika katika uundaji na utekelezaji wa sera, mipango na makisio ya bajeti.
Sehemu hii itakuwa chini ya Kamishna msaidizi.