Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga amesema kuwashwa kwa umeme katika vijiji mbalimbali vya wilaya hiyo, kumeongeza ufaulu wa wanafunzi wa kidato cha nne na cha pili katika shule za sekondari.

Aliyasema hayo Februari 12, 2020 mbele ya Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani, kwenye hafla ya uwashaji umeme katika Zahanati ya Kijiji cha Mpenda, Halmashauri ya Mtama, wilayani Lindi.

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani akiwasha umeme katika Zahanati ya Kijiji cha Mpenda, Halmashauri ya Mtama, mkoani Lindi, Februari 12, 2020.

“Mheshimiwa Waziri, naomba nikuhakikishie kuwa ahadi aliyoitoa Mkuu wa Shule ya Sekondari Namangale, siku ulipokuwa unawasha umeme katika shule hiyo, imetimia. Shule hiyo na nyingine tisa (9) ambazo umeziwashia umeme hazina tena division 0,” alisema.

Mkuu huyo wa Wilaya aliishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa kutekeleza ahadi zake ambazo alisema zimekuwa zikiboresha maisha ya wananchi katika nyanja mbalimbali ikiwemo kiuchumi.

Akieleza zaidi kuhusu manufaa ambayo wananchi wamekuwa wakiyapata kutokana na nishati ya umeme, alisema mbali na kuboresha elimu, uwepo wa umeme pia umeboresha huduma katika sekta mbalimbali zikiwemo afya na maji.

“Hapa Mpenda, baada ya wewe kusema unawasha umeme, watu wa maji nao wamejitokeza na kusema wanaleta maji, maana sasa wamekuwa na uhakika kuwa umeme upo.”

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Kalemani alikiri kufurahishwa na taarifa ya Mkuu wa Wilaya kuwa umeme umeleta matokeo chanya katika elimu na sekta nyingine mbalimbali wilayani humo.

Alimwagiza Mkandarasi anayetekeleza Mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Kwanza (REA III, Phase 1), kuhakikisha anaongeza idadi ya magenge ili kusambaza umeme katika vitongoji mbalimbali ambavyo havijafikiwa.

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (kushoto), akikabidhi kifaa cha Umeme Tayari (UMETA) kwa wananchi wakati wa hafla ya kuwasha umeme katika Zahanati ya Kijiji cha Ng’au, Kata ya Mnacho, wilayani Ruangwa, Mkoa wa Lindi, Februari 12, 2020. Waziri alisisitiza vifaa hivyo vitumike kuunganisha umeme katika taasisi za umma.

Aidha, Waziri alimtaka Mkandarasi huyo ambaye ni Kampuni ya State Grid Electrical & Technical Works Ltd, kuhakikisha anakamilisha kazi yote katika wigo aliopewa ifikapo mwishoni mwa mwezi Aprili mwaka huu na kuikabidhi kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), ambapo Mkandarasi husika aliahidi kutekeleza agizo hilo.

Katika ziara hiyo mkoani Lindi, Waziri Kalemani pia aliwasha umeme katika Zahanati ya Kijiji cha Ng’au, Kata ya Mnacho wilayani Ruangwa pamoja na kukagua hali ya upatikanaji umeme na kuzungumza na wananchi wa Kijiji cha Nandagala wilayani Ruangwa.

Akiwa Ruangwa, Waziri alipokea salamu za shukrani kwa Rais John Magufuli kutoka kwa wananchi ambazo ziliwasilishwa na Mkuu wa Wilaya Hashim Mgandilwa, zikieleza kuridhishwa na utendaji kazi mahiri ambao umewapatia maendeleo hususan katika sekta ya umeme.

Kwa nyakati tofauti alitoa pongezi kwa wabunge wa maeneo hayo ambao ni Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (Ruangwa) na Nape Nnauye (Mtama) kwa kazi nzuri wanazofanya katika kuhakikisha wananchi wao wanapata umeme.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka TANESCO Lindi, maendeleo ya Mradi wa REA III – 1 kwa ujumla katika mkoa huo, hadi kufikia Februari 2020, ni asilimia 99 ambapo kazi mbalimbali zimetekelezwa.

Na Veronica Simba