Imeelezwa kuwa, ujenzi wa Mradi wa umeme wa Rusumo (MW 80) unaotekelezwa kwa ushirikiano wa nchi za Tanzania, Rwanda na Burundi umefikia zaidi ya asilimia 47 na  matarajio ni kukamilika mwaka 2020.

Hayo yamebainika tarehe 21 Juni, 2019 wakati Mkutano wa Tatu wa  Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani, Waziri wa Miundombinu wa Rwanda, Claver Gatete na Waziri wa Nishati na Migodi wa Burundi, Come Manirakiza uliofanyika Rusumo, wilayani Ngara mpakani mwa nchi za Tanzania na Rwanda ambapo mradi huo unatekelezwa.

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (wa tatu kushoto) na Waziri wa Miundombinu wa Rwanda, Claver Gatete (wa nne kutoka kulia) na watendaji mbalimbali kutoka nchi za Tanzania, Rwanda na Burundi wakikagua ujenzi wa miundombinu katika mradi wa umeme wa Rusumo ( MW 80) wilayani Ngara.

Mwenyekiti wa Mkutano huo, Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani alisema kuwa kwa ujumla wameridhishwa na kazi zilizofanyika hadi sasa ambazo ni ujenzi wa sehemu itakaposimikwa mitambo ya umeme ambao umefikia asilimia 100 na ujenzi wa njia kwenda kwenye mgodi wa umeme ambao nao umefikia asilimia 100.

Alitaja kazi nyingine walizoridhishwa nazo kuwa ni, ujenzi wa eneo kutakapojengwa vituo vya kupoza umeme ambao umefikia asilimia 99, na ujenzi wa kambi ya wafanyakazi watakaosimamia mradi uliotekelezwa kwa asilimia 99.

Wajumbe wa Bodi ya usimamizi ya mradi wa umeme wa Rusumo wakiwa kwenye mkutano wa Tatu wa Mawaziri wanaosimamia Sekta ya Nishati/Miundombinu kutoka Tanzania, Rwanda na Burundi uliofanyika wilayani Ngara, Mkoa wa Kagera.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

“Kazi kubwa iliyobaki ni kwa upande wa upasuaji mwamba ambao kwa ujumla umefikia asilimia 47 lakini mwamba huo inabidi upasuliwe kwa mita 703, hadi wamepasua kwa mita 400 hivyo tumewataka wazingatie kanuni na taratibu ili kutoleta madhara kwa wananchi wanaoishi karibu na Mgodi.” alisema Dkt Kalemani

Aliongeza kuwa, Mkandarasi wa mradi huo, kampuni ya CP1 aliomba kuongezewa muda wa utekelezaji lakini Mawaziri hao walikataa ombi hilo na kuelekeza kuwa Mkandarasi afanye kazi usiku na mchana na kuongeza wafanyakazi ili mradi huo ukamilike kwa wakati.

Alisema kwenye mradi huo, vitajengwa vituo vitatu vya kupoza umeme ambavyo vitasafirisha umeme mkubwa wa kV 220 kwenda nchi za Rwanda, Burundi na Tanzania.

Kuhusu gharama za utekelezaji wa mradi alisema kuwa, mradi huo unafadhiliwa na Benki ya Dunia (WB), Benki ya Maendeleo ya  Afrika (AfDB) na nchi zinazofaidika na mradi husika.

Kwa upande wake, Waziri wa Miundombinu wa Rwanda, Claver Gatete alisema kuwa baada ya kutembelea mradi huo wameona kuna maendeleo yamefanyika na wamempongeza Mkandarasi kwa hatua hiyo na wanategemea mradi utakamilika mwezi Februari mwaka 2020.

Alisema kuwa, kazi ya upasuaji mwamba ambayo Mkandarasi anapaswa kufanya tayari imeshatengewa fedha hivyo haitahitaji fedha ya ziada, lakini walichomsisitiza Mkandarasi huyo ni kufanya kazi hiyo kwa mujibu wa kanuni na taratibu za nchi.

Na Teresia Mhagama