Imeelezwa kuwa, jumla ya wananchi 10,000 watalipwa fidia kutokana na kupisha mradi wa ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi linalotoka Uganda hadi Tanzania (EACOP),  lenye urefu wa kilometa 1445.

Hayo yelisemwa tarehe 1 Juni, 2019 na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani  wakati akifungua  Kongamano la Wadau wa Mkoa wa Kagera lililohusu mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki lililofanyika wilayani Bukoba, Mkoa wa Kagera.

Kongamano hilo lilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiongozwa na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Dkt Hamisi Mwinyimvua, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati ya Nishati na Madini, Dunstan Kitandula, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Brigedia Jenerali Marco Gaguti,  Kaimu Kamishna wa Petroli na Gesi, Mwanamani Kidaya, Wakuu wa Wilaya, Wenyeviti wa Halmashauri, Wabunge na wawakilishi wengine wa wananchi.

“Katika mwaka huu wa fedha tumetenga zaidi ya shilingi Bilioni 50.7 kwa ajili ya kazi za fidia na hatua inayofuata ni kuwataarifu wananchi waliofanyiwa tathmini na kuwaonesha stahili zao ni zipi kabla ya kuanza kulipa.” alisema Dkt. Kalemani

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (wa kwanza kushoto), Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati, Dkt.Hamisi Mwinyimvua (wa kwanza kulia) na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini, Dunstan Kitandula, wakiwa katika kikao cha wadau wa mradi wa Bomba la Mafuta mkoani Kagera.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Kuhusu ujenzi wa Bomba hilo, Dkt Kalemani alisema kuwa, matarajio ni kuanza ujenzi mwezi Septemba mwaka huu, mara majadiliano baina ya pande zinazohusika na mradi huo kukamilika na mradi unatarajiwa kukamilika baada ya miaka mitatu.

Kuhusu mradi huo, Dkt Kalemani amesema kuwa, utaajiri watanzania takribani 10,000 wakati wa ujenzi na baada ya ujenzi watanzania zaidi ya 200 wataajiriwa na kwamba Bomba litakalojengwa litakuwa na uwezo wa kusafirisha mapipa 216,000 kwa siku na kila pipa litalipiwa Dola 12.2  kama ushuru.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, akizungumza wakati wa kikao cha wadau wa mradi wa Bomba la Mafuta kilichofanyika mkoani Kagera.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Alisema kuwa, gharama za mradi ni USD bilioni 3.5 na kwa upande wa Tanzania Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) ndilo litakashiriki katika ujenzi wa mradi huo kwa niaba ya Serikali.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, aliwapongeza wataalam kutoka Tanzania walioshiriki katika majadiliano ya mradi huo ambayo kwa sasa yamefikia zaidi ya asilimia 80 hali itakayowezesha pande zinazohusika na mradi huo kuanza utekelezaji wa mradi.

Pia alieleza lengo la Serikali la kufikisha umeme katika vijiji vinavyopitiwa na mradi ili kuwezesha pia kazi za ujenzi wa Bomba hilo kufanyika wakati wote bila ya kuwa na changamoto ya umeme.

Vilevile, aliahidi wananchi wa Mkoa wa Kagera kuwa, Serikali itaendelea kushirikiana nao katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya nishati ukiwemo wa Bomba la Mafuta ili kuweza kufanikisha miradi hiyo kwa ufanisi.

Katika Mkutano huo, wadau mbalimbali wakiwemo Wabunge wa Mkoa huo, walitoa maoni mbalimbali yatakayoboresha utekelezaji wa mradi na baadhi ya masuala waliyogusia ni pamoja na ajira kwa wazawa, fidia ya wananchi wanaopisha mradi, ulinzi wa Bomba na upatikanaji wa fursa wakati wa utekelezaji wa mradi.

Na Teresia Mhagama