Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Medard kalemani ameliagiza Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kukamilisha ufungaji wa mitambo ya kusindika Gesi Asilia (Compressed Natural Gas – CNG) kwa matumizi ya magari ndani ya miezi sita.

Waziri Kalemani ametoa maagizo hayo kwa TPDC tarehe 23 Januari, 2021 wakati alipokuwa akikagua mradi wa Usindikaji wa Gesi Asilia (Compressed Natural Gas-CNG) itakayotumika kwenye mabasi yaendeyo kasi yaliyozoeleka kama mwendokasi (Dar es Salaam Bus Rapid Transit – DART) katika kituo kinachoendelea kujengwa cha magari yaendayo kasi cha DART kilichopo Ubungo jijini Dar-es-Salaam ambacho awali kilikuwa ni kituo kikuu cha mabasi yaendayo mikoani katika jiji la Dar-es-salaam.

Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Medard Kalemani mara baada ya kuwasili kwenye eneo la mradi wa usindikaji wa Gesi asilia (Compressed Natural Gas-CNG) itakayotumika kwenye mabasi yaendeyo kasi yaliyozoeleka kama mwendokasi (Dar es Salaam Bus Rapid Transit – DART) katika kituo kinachoendelea kujengwa cha magari yaendayo kasi cha DART kilichopo Ubungo jijini Dar-es-salaam ambacho awali kilikuwa ni kituo kikuu cha mabasi yaendayo mikoani cha Dar-es-Salaam, tarehe 23 Januari, 2021 kwa ajili ya kujionea maendeleo ya Mradi wa DART unaotarajiwa kutumia gesi asilia (CNG) itakayosambazwa na TPDC.

Waziri Kalemani ameiagiza TPDC kutoa huduma hiyo si tu kwa magari 300 yaendayo kasi, bali pia kwa watumiaji binafsi ili kuongeza kipato kwa Serikali,  kuipunguzia DART gharama za uendeshaji na hivyo kuleta unafuu wa gharama za nauli ya mabasi kwa wananchi.

‘’Sitakuja kuzindua matumizi ya gesi asilia kwa magari 300 tu. Ongezeni wigo wa watumiaji wa gesi asilia kwa magari mengine yakiwemo ya watu binafsi.” Amesema Dkt. Kalemani

Aidha, Waziri huyo wa Nishati, ameongeza kuwa, matumizi ya gesi asilia kwenye magari ya watu binafsi yataleta unafuu mkubwa wa gharama ikilingalishwa na matumizi ya Petroli na dizeli kwa zaidi ya asilimia 45.

Vilevile, Waziri Kalemani amewashauri wananchi kufunga mfumo utakaowawezesha kutumia gesi asilia kwenye magari yao ambao utawapa unafuu mkubwa katika matumizi ya magari yao.

Dkt. Kalemani amesema, kwa sasa kuna magari takriban 800 yanayotumia gesi, hivyo amewashauri wananchi wenye magari na vyombo vingine vya moto waongeze mfumo utakaowawezesha kutumia gesi asilia, na kwamba, huduma hiyo ya kufunga mfumo kwa ajili ya kutumia gesi asilia inapatikana katika Chuo Kikuu cha Dar-es-salaaam na Taasisi ya Teknolojia ya Dar-es-salaam (DIT).

Waziri Kalemani amesema, Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni kumi kwa ajili ya kukamilisha mradi huo.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dkt. James Mataragio, alimueleza Waziri Kalemani kuwa,  mradi huo ulipangwa kuanza kutumiwa na mabasi 300 yaendayo kasi na ulipangwa kukamilika ndani ya miezi Sita.

Alisema,  kwa kuanzia, vituo vingine vinne vya usindikaji wa Gesi asilia vitajengwa katika maeneo ya Chuo Kikuu – Mlimani City, Eneo la Feri, Muhimbili na Kibaha na ujenzi wa vituo hivyo unakwenda sambamba na ujenzi wa kituo cha magari yaendayo kasi cha DART kilichopo Ubungo jijini Dar-es-salaam.

Dkt. Mataragio amebainisha kuwa, TPDC imepanga kujenga vituo vitano vya CNG ambapo kati ya hivyo, viwili vitakuwa vituo vikuu (CNG mother stations) na vitatu vitakuwa vituo vidogo (CNG daughter Stations) ambapo Kituo Kikuu kimoja kitajengwa eneo la Ubungo linalomilikiwa na DART maalum kwa mabasi ya mradi wa BRT uliozoeleka kama mwendokasi ambapo kitakuwa na uwezo wa kujaza gesi katika mabasi zadi ya 300 kwa siku.

Aidha,  ameeleza kuwa, kituo Kikuu cha pili kitajengwa pembezoni mwa barabara ya Sam Nujoma katika eneo la Chuo Kikuu cha Dar es salaam ambapo kituo hiki kwa kuanzia kitakuwa na uwezo wa kujaza gesi katika magari zaidi ya 200 kwa siku na pia kitatumika kuhudumia vituo vidogo (CNG daughter stations) vitakavyojengwa katika maeneo mbalimbali.

Akizungumzia ujenzi wa vituo vidogo, Dkt. Mataragio amesema, vituo hivyo vitajengwa eneo la Soko kuu la samaki Feri, Hospitali ya Muhimbili, pamoja na Galagaza-Kibaha katika eneo la ukanda wa viwanda.

Amesema, Kituo cha Muhimbili pamoja na Soko Kuu la samaki Feri vitakuwa na uwezo wa kuhudumia magari zaidi ya 200 kwa siku.

Dkt. James Mataragio, amemuahidi Waziri Kalemani kuwa, atahakikisha wanatekeleza maagizo yote aliyowapatia.