Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amekutana na wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini, awamu ya tatu, mzunguko wa kwanza na kujadiliana maendeleo ya mradi huo unaotekelezwa nchini kote.

Kikao hicho kilichofanyika leo, Mei 21, 2020 jijini Dodoma kimehudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu, Katibu Mkuu Mhandisi Zena Said, Naibu Katibu Mkuu Mhandisi Leonard Masanja, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Wakili Julius Kalolo pamoja na Wajumbe wa Bodi hiyo.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akizungumza na Wakandarasi wanaotekeleza Mradi wa Umeme Vijijini, Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Kwanza (hawapo pichani) wakati wa kikao cha Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani) na Wakandarasi hao kilichofanyika jijini Dodoma, Mei 21, 2020 kujadili maendeleo ya Mradi huo.

Wengine ni Kaimu Kamishna wa Nishati Edward Ishengoma, Kamishna Msaidizi wa Umeme Mhandisi Innocent Luoga, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Dkt. Tito Mwinuka, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa REA Mhandisi Amos Maganga na Menejimenti yake, Mameneja wa TANESCO wa Kanda pamoja na Wasimamizi wa Mradi husika kutoka Wizarani.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Zena Said (wa pili kushoto) akizungumza na Wakandarasi wanaotekeleza Mradi wa Umeme Vijijini, Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Kwanza (hawapo pichani), wakati wa kikao cha Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani) na Wakandarasi hao kilichofanyika jijini Dodoma, Mei 21, 2020 kujadili maendeleo ya Mradi huo. Kushoto kwake ni Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu na kulia kwake ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Wakala wa Nishati Vijijini REA, Wakili Julius Kalolo.

Akifungua kikao husika, Dkt Kalemani amewapongeza Wakandarasi hao kutokana na kazi wanayoifanya ya kusambaza umeme vijijini lakini amebainisha msimamo wa Wizara kuwa haitarajii kuongeza muda wa kukamilisha kazi husika, hivyo amewataka kuongeza bidii na ubunifu ili waweze kukamilisha kazi ifikapo Juni 30, mwaka huu kama ilivyoainishwa katika Mkataba.

Kutoka kulia ni Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Mbadala Edward Ishengoma, Kamishna Msaidizi wa Umeme Mhandisi Innocent Luoga na Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Jones Olotu, wakifuatilia kikao kati cha Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani) na Wakandarasi wanaotekeleza Mradi wa Umeme Vijijini, Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Kwanza (hawapo pichani), kilichofanyika jijini Dodoma, Mei 21, 2020 kujadili maendeleo ya Mradi huo.

“Pamoja na kwamba wengi wenu mnafanya kazi nzuri lakini wapo wachache ambao wanasuasua. Ninawataka mjipime kutokana na utendaji wenu kama mtastahili kuendelea na kazi nyingine zitakazofuata,” ameasa Waziri.

Akifafanua zaidi, amesema Wizara kamwe haitaingia mikataba mipya ya kazi na wakandarasi wababaishaji huku akisisitiza kuwa ni wale tu wanaofanya vizuri katika miradi ya sasa ndiyo watakuwa na nafasi ya kupewa kazi nyingine.

Katika hatua nyingine, Waziri amewataka wakandarasi hao kutambua kuwa wao ni watumishi wa umma hivyo amewataka kufanya kazi kwa weledi na uzalendo huku wakizingatia maslahi ya wananchi na Taifa kwa ujumla kwani ndivyo watumishi wa umma wanavyopaswa kuwa.

Amefafanua kuwa, mtumishi wa umma ni yeyote aliyeajiriwa au kuingia mkataba na Serikali kufanya kazi fulani na ataendelea kuwa na sifa hiyo hadi pale mkataba wake unapokoma.

Aidha, Waziri ametoa pongezi za pekee kwa wakandarasi ambao hadi sasa wamekamilisha kazi kwa asilimia nyingi huku wakiwa na uelekeo wa kukamilisha kazi husika muda mfupi kutoka hivi sasa.

Wakandarasi hao wametajwa kuwa ni Kampuni za Steg International Ltd anayetekeleza Mradi katika mikoa ya Mbeya na Songwe, Sengerema Engineering Group Ltd (Iringa), Derm Electrics (T) Ltd  (Tanga) na Nakuroi Investment Co. Ltd (Rukwa).

Vilevile, Waziri ametoa pongezi kwa Bodi ya Wakurugenzi wa REA kwa kazi nzuri wanayoifanya katika kusimamia miradi husika. Pia, ameipongeza Menejimenti ya Wakala huo na watumishi wake wote huku akiipambanua Taasisi hiyo kwamba imetengeneza historia Tanzania.

“Tanzania sasa inasifika kwa kazi nzuri ya usambazaji umeme vijijini. Hilo limewezekana kwa uchapakazi wenu. Hongereni sana.”

Sambamba na REA, Waziri pia ameipongeza TANESCO, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu kwa utendaji wao mahiri ambao ameeleza umewezesha mafanikio ya utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika kikao hicho, Naibu Waziri Mgalu na Katibu Mkuu Mhandisi Said, pamoja na kuunga mkono pongezi alizotoa Waziri kwa REA, TANESCO na Wakandarasi, pia wametoa nasaha kwao.

Naibu Waziri amesema, miradi ya REA ili itekelezwe kwa ufanisi, inahitaji ushirikiano baina ya pande zote ambazo ni mwajiri, mwajiriwa na wadau wote wanaohusika.

“Serikali tunathamini na tunaahidi kuendelea kuwajengea mazingira mazuri ili muweze kukamilisha kazi zenu kwa wakati na viwango.”

Naye Katibu Mkuu amewaasa wakandarasi kujenga mahusiano mazuri na viongozi pamoja na wananchi wote katika maeneo wanakotekeleza miradi, ili iwasaidie kupata ushirikiano katika utekelezaji wa kazi zao.

“Unapoaminiwa, basi jitahidi ili nawe ufanye ile kazi kwa kiwango kinachostahili ili uendelee kuaminiwa,” amesisitiza Katibu Mkuu.

Wizara ya Nishati imejijengea utamaduni wa kufanya mikutano ya aina hii mara kwa mara ili kutoa fursa ya majadiliano baina ya pande zote, kwa lengo la kuboresha utendaji kazi kwa manufaa ya Watanzania na Taifa kwa ujumla.

Na Veronica Simba – Dodoma