Wizara ya Nishati imefanya ukaguzi wa kuangalia hali ya usalama katika maghala ya kuhifadhi na kupakua mafuta na Gesi yaliopo jijini Dar es salaam pamoja na kujionea tahadhali zinazochukuliwa katika maghala hayo ili kukabiliana na janga la moto pindi litakapotokea.

Ukaguzi huo ulifanyika kwa muda wa wiki nzima kunzia Mei 26 hadi Juni 3, 2020 ukiongozwa na Kamishna wa Mafuta na Gesi na kutoka Wizara ya Nishati pamoja maafisa wengine kutoka wizara hiyo, kwa kushirikiana na maafisa kutoka Mamlaka ya Uthibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), na Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa pamoja ( PBPA).

Kamishna wa Petroli na Gesi wa Wizara ya Nishati, Adam Zuberi( wa pili kulia) akiwa pamoja na ujumbe wake wakati wa ziara ya kukagua usalama wa maghala ya kuhifadhi na kupakua mafuta pindi moto utakapotokea, kuanzia Mei, 26 hadi Juni 3, 2020.

Wizara ya Nishati ilifanya ukaguzi huo ili kutathmini mwenendo wa utekelezaji wa mapendekezo ya kamati iliyounda na Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni kuchunguza chanzo cha ajali ya moto uliotokea katika ghala la kuhifadhia mafuta na gesi mali ya kampuni ya Lake Oil katika eneo la Kigamboni mwanzoni mwa Mwezi Januari 2020, pamoja na kubaini mapungufu yaliopo katika baadhi ya Kampuni mbalimbali katika kukabiliana na majanga kama hayo.

Baada ya kufanya ukaguzi huo, Wizara pamoja na ujumbe walioambata nao walibaini changamoto mbalimbali hivyo walizitaka mamlaka husika kuruhusu kampuni hizo kuunganisha maji kutoka baharini pamoja na kuwa na muongozo wa pamoja kuunganisha miundombinu ya maji na viwanda vilivyopo jirani ili kuweza kupata msaada kutoka kwa majirani wanaowazunguka ili kukabiliana na janga la moto pindi litakapotokea. Aidha, ujumbe huo ulishauri kuwepo na vikao vya pamoja baina ya makampuni kwa lengo la kujadili masuala ya usalama na kuweka mikakati ya pamoja katika kukabiliana na majanga ya moto na mengine.

Kwa upande wao wamiliki wa maghala wameomba Wizara kwa  kushirikiana na mamlaka husika kuona namna bora ya kuboresha mfumo wa gharama kubwa za kufanya tathmini ya athari kwa mazingira na kuwa rafiki kwa wawekezaji ili waweze kujenga kwa utaratibu unaotakiwa, tofauti na sasa mchakato huo umekuwa mrefu na wa gharama kubwa jambo linalowafanya wawekezaji wengi kujenga bila kufanya tathmini ya athari ya mazingira na baadaye kujikuta wamekosa ushauri wa kitaalam unaohitajika kuzingatia kabla ya kujenga: Hata hivyo, kwasasa NEMC iboreshe utoaji wa vibali vya tathmini ya athari za kimazingira ili kuvutia uwekezaji.

Wizara ilishauri Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kuratibu mazoezi ya pamoja na makampuni ya mafuta na gesi ya kujiandaa kupambana na majanga ya moto (walau mara moja kila baada ya miezi sita) pia kuweka kituo cha zimamoto kikubwa kwa upande wa Kigamboni.

Sambamba na hilo EWURA ilishauriwa kuratibu vikao vya Usalama vitakavyofanyika kila mwezi vya kujumuisha Kampuni zote za mafuta na gesi pamoja na kufupisha muda wa upatikanaji wa leseni na kuhuisha leseni na kuvutia uwekezaji.

Kamishna wa Petroli na Gesi wa Wizara ya Nishati, Adam Zuberi( katikati) akikagua moja ya pampu za maji zitakazotumika kuzima moto katika maghala ya kuhifadhi na kupakua mafuta, Kamishna wa Mafuta na Gesi pamoja na ujumbe wake walifanya ziara ya kukagua usalama wa maghala hayo pindi ajali ya moto itakapotokea kuanzia Mei, 26 hadi Juni 3, 2020.

Vilevile kampinu hizo zimeshauriwa  kuwa na maeneo maalumu na yakutosha ya maegesho ya magari yanayosubiri kujaza mafuta ili kupunguza msongamano. Aidha, mamlaka husika zimeshauriwa kuweke muongozo wa bei elekezi ya serikali kwa ajili ya fidia za makazi yaliopo jirani na maghala ya kuhifadhi mafuta na gesi ili waondolewe katika maeneo hayo kupunguza athari zinazoweza kutokea endapo janga la moto litatokea.

Ujumbe huo wa Wizara umezishauri kampuni zote hususan za wazawa kuajiri maafisa wa Afya na Usalama kazini ili pamoja na kusimamia shughuli za usalama kazini kuweka mpango mkakati wa mafunzo yanayohusu namna bora ya kukabiliana na majanga na kundaa mpango shiriki wa kufanya mazoezi ya dharula ili kujiandaa wakati wa dharura.

Pia Kampuni hizo kuwa na utaratibu wa kufanya matengenezo ya kudumu ya miundombinu na ukaguzi wa kiufundi wa mara kwa mara katika maghala yao ili kuwezesha miundombinu hiyo kudumu na imara wakati wote.  .

Aidha, kamati hiyo ilitembelea kampuni zifuatazo, Lake Oil Limited, TIPER, World Oil Limited, Sahara Tanzania Limited, GBP, PUMA, Total, Manjis Gas, Afroil Investment Limited, TAZAMA, Camel Gas, Oryx Gas Limited pamoja na Hass Petroleum (T) Limited.

 Na Zuena Msuya DSM,