Dkt. Kalemani Awaomba Radhi Watanzania. Aeleza Jitihada Za Serikali Na Kutoa Maagizo Kwa Tanesco

Na Mwandishi Wetu

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (wa kwanza kulia) akiwa katika eneo la Kinyerezi I linalozalisha Umeme wa kiasi cha megawati 150.

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani amewaomba radhi watanzania kufuatia kukatika kwa Umeme kulikosababishwa na hitilafu katika Gridi ya Taifa tarehe 25 na 26 Oktoba, 2017 na hivyo kusababisha mikoa inayopata Umeme kupitia gridi hiyo kukosa Umeme.

Dkt Kalemani alisema hayo, tarehe 26 Oktoba, 2017 katika ofisi za Wizara jijini Dar es Salaam alipofanya mkutano na waandishi wa habari.

Akitokea mkoani Dodoma, Dkt Kalemani alifanya ziara ya kukagua Kituo  cha kuzalisha Umeme cha Kinyerezi I na kituo cha kudhibiti mifumo ya Umeme cha Ubungo ili kupata picha halisi ya tatizo hilo.

Dkt Kalemani alieleza kuwa chanzo cha kutokea kwa hitilafu hiyo ya Umeme kilikuwa ni kukatika kwa waya (Cable) wa kupeleka Umeme kwenye Geti la kufungulia Maji katika Bwawa la Kidatu linalozalisha Umeme wa kiasi cha megawati  204.

Alisema kuwa, hitilafu hiyo ilisababisha mtambo wa Kidatu pamoja na mitambo mingine ya kuzalisha Umeme katika sehemu mbalimbali nchini kutoka kwenye Gridi ya Taifa na hivyo kusababisha mikoa yote iliyounganishwa kwenye mfumo wa Gridi hiyo kukosa Umeme.

Aliongeza kuwa,  baada ya kutokea kwa tatizo hilo Serikali kupitia TANESCO ilifanya juhudi mbalimbali ambapo hadi kufikia tarehe 26 Oktoba, 2017 Gridi hiyo ilirejea katika hali yake ya kawaida na baadhi ya maeneo nchini yanapata Umeme isipokuwa sehemu chache ambazo zitapata Umeme baada ya mtambo wa Umeme wa  Ubungo  II (MW 129)  utakapoanza kufanya kazi tarehe 27 Oktoba, 2017 kuanzia Saa Tano asubuhi.

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (wa tatu kushoto) akiwa katika chumba cha kuongozea mitambo katika eneo la Kinyerezi I linalozalisha Umeme wa kiasi cha megawati 150. wa pili kulia ni Kaimu Kamishna wa Nishati, Mhandisi Innocent Luoga. Wengine katika picha ni watendaji wa TANESCO na Wizara ya Nishati.

Aidha alisema kuwa, ameagiza wataalam kufanya kazi usiku na mchana ili mtambo huo uanze kufanya kazi na  huduma ya Umeme irejee katika hali yake ya kawaida.

Vilevile aliagiza Meneja wa Mtambo wa Kidatu kuondolewa katika kituo hicho baada ya kuchelewa kutoa taarifa kuhusu hali ya hitilafu ya Umeme, “ Nimemwelekeza Mkuu wake amuondoe katika kituo hicho mara moja leo Ili tuwe na wafanyakazi wachache wenye weledi,”.

Kuhusu mitambo yote ya kuzalisha Umeme ambayo haifanyi kazi kutokana na kuhitaji ukarabati, alimuagiza Naibu Mkurugenzi TANESCO anayeshughulikia Uzalishaji kuhakikisha mitambo hiyo inakarabatiwa ndani ya kipindi cha wiki mbili.

Kwa upande wa udhibiti wa mfumo wa Umeme ambao unapaswa kutambua tatizo la Umeme mara linapotokea, alimtaka Meneja wa TANESCO, anayeshughulikia Mfumo huo na Usambazaji Umeme kuhakikisha mfumo husika unafanya kazi mara moja.

Pata taarifa zaidi katika ukurasa wa 10.