Mkutano wa 13 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki; uliopangwa kufanyika Oktoba 19, 2018 haujafanyika kutokana na kutotimia kwa idadi (akidi) ya Mawaziri husika wanaohitajika kushiriki katika Mkutano huo.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (kulia), akizungumza wakati wa kikao kilichotangaza kuahirishwa kwa Mkutano wa 13 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki, uliokuwa ufanyike leo Oktoba 19, 2018, jijini Arusha. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara, Dkt. Hamisi Mwinyimvua.

Akizungumza jijini Arusha, katika Ukumbi wa Jengo la Afrika Mashariki (EAC) ambako Mkutano ulipangwa kufanyika, Mwenyekiti wa Baraza husika, ambaye ni Waziri wa Nishati wa Uganda, Mhandisi Irene Muloni, aliwaeleza wajumbe waliofika kushiriki katika Mkutano husika kuwa kutofika kwa baadhi ya Mawaziri, kumepelekea kuahirishwa kwa Mkutano husika mpaka wakati mwingine.

Mhandisi Muloni aliwataja Mawaziri ambao hawakufika kushiriki katika Mkutano huo kuwa ni wale wenye dhamana ya nishati kutoka nchi za Kenya, Rwanda na Sudani Kusini, ilhali waliofika ni kutoka nchi za Tanzania, Uganda na Burundi pekee.

“Ili akidi itimie, ni lazima Mawaziri wenye dhamana ya nishati kutoka nchi zote sita (6) wanachama, wawepo. Kutofika kwa Mawaziri watatu, kunatulazimu kuahirisha Mkutano huu muhimu,” alifafanua Mwenyekiti.

Hata hivyo, aliwapongeza Makatibu Wakuu na Wataalam ambao walishiriki Mkutano huo kwa ngazi zao kuanzia Oktoba 15 hadi 18 mwaka huu, na kufanikisha kupitia na kuidhinisha taarifa za utekelezaji wa miradi mbalimbali ya nishati katika nchi za Jumuiya husika.

Waziri wa Ardhi, Makazi, Maji, Nishati na Mazingira (Zanzibar) Salama Talib, akizungumza wakati wa kikao kilichotangaza kuahirishwa kwa Mkutano wa 13 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki, uliokuwa ufanyike leo Oktoba 19, 2018, jijini Arusha. Kulia kwake ni Waziri wa Nishati (Tanzania Bara), Dkt. Medard Kalemani.

Alisema kuwa, Mkutano husika Ngazi ya Mawaziri utaandaliwa tena na wakikutana, watafanya kazi ya kupitia na kuidhinisha taarifa iliyoandaliwa na wataalam na kuidhinishwa na Makatibu Wakuu, ambayo ilikuwa iwasilishwe kwao leo.

Miongoni mwa taarifa zilizoandaliwa na wataalam na kuidhinishwa na Makatibu Wakuu ni pamoja na zinazohusu sekta ndogo za nishati mbadala, uhifadhi wa nishati, ubora wa nishati. sekta ndogo ya mafuta na inayohusu sekta ndogo ya umeme.

Dhima ya taarifa hizo zote ni kuboresha sekta ya nishati katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kuinua uchumi wa nchi husika, hivyo kuboresha maisha ya wananchi wake.

Kutoka Tanzania, Waziri wa Nishati (Tanzania Bara) Dkt. Medard Kalemani na Waziri wa Ardhi, Makazi, Maji, Nishati na Mazingira (Zanzibar) Salama Talib, walikuwepo Arusha kwa nia ya kushiriki Mkutano husika.

Na Veronica Simba