Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani amezima mashine zilizokuwa zikitumia mafuta mazito kuzalisha umeme katika kituo cha Ludewa na kukiunganisha katika umeme wa gridi ya taifa.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, akibonyeza kitufe ili kuzima umeme wa mafuta katika kituo cha Ludewa wilayani Ludewa na kukiunganisha katika gridi ya taifa.

Kuzimwa kwa kituo cha Ludewa ni matokeo chanya ya kukamilika kwa mradi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Makambako, Madaba hadi Songea mjini wenye umbali wa kilometa takribani 250.

Akizungumza wakati wa ziara yake ya kikazi katika Mkoa wa Njombe ya kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme, Dkt. Kalemani, alisema kuwa kuzimwa kwa mtambo huo katika kituo cha Ludewa kumeokoa zaidi ya shilingi milioni 75 kwa mwezi zilizokuwa zikitumika kununua mafuta mazito kuzalisha umeme.

Alifafanua zaidi kuwa, katika wilaya hiyo ya Ludewa vijiji 9, vitanufaika na mradi huo na kwamba kwa ujumla vijiji takribani 122, wateja 22,700 vitanufaika katika mradi mzima.

“Wananchi wa Ludewa pamoja na wengine wote ambao vijiji vyao vimepitiwa na mradi huu wa gridi ya taifa ongezeni kasi ya kulipia huduma ya umeme kwa kuwa ni bei rahisi ya shilingi 27,000 kama ilivyokuwa katika mradi wa kusambaza umeme vijijini (REA)” alisisitiza Dkt. Kalemani.

Umeme unaotumika katika wilaya ya Ludewa unatoka katika kituo cha Madaba ikiwa ni umbali wa kilometa 140 na umegharimu kiasi cha shilingi bilioni 13.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, (wa pili kushoto) akikata utepe kuashiria kuzima umeme unaotumia mafuta mazito wilayani Ludewa na kuungalisha Wilaya hiyo katika gridi ya taifa.

Baada ya kuunganishwa katika gridi ya taifa, Kituo hicho kwa sasa kimeongezwa uwezo na kuzalisha megawati 2, tofauti na ilivyokuwa hapo awali kilikuwa kinazalisha megawati 0.5 ambapo mahitaji ya umeme kwa wakazi wa wilaya hiyo ni chini ya megawati 1.5.

Vilevile, aliwaeleza watendaji wa TANESCO kuhakikisha kuwa umeme haukatiki katika wilaya hiyo na endapo utakatika pasipo sababu ya msingi hatasita kuwachukulia hatua watendaji hao.

Kituo cha Ludewa mkoani Njombe ni miongoni mwa vituo vilivyokuwa vikitumia mafuta mazito ana vituo vingine ni Mbinga, Madaba, Songea na Namtumbo ambavyo vimeunganishwa na umeme wa gridi wenye urefu wa kilomita 250, ambao umegharimu kiasi cha shilingi bilioni 219, ikiwa ni fedha za Serikali na wahisani.

Na Zuena Msuya

7 Novemba, 2018

cpluskey.com