Imeelezwa kuwa, kazi mbalimbali za maandalizi ya ujenzi wa mradi wa umeme wa Rufiji ( MW 2115) zinazofanywa na Mkandarasi kampuni ya ubia ya Arab Contractors na Elsewedy Electric  zimefikia zaidi ya asilimia 4O.

Moja ya nyumba inayojengwa na mkandarasi anayetekeleza mradi wa umeme wa Rufiji ambapo katika eneo hilo kunajengwa  kambi ya muda ya Wafanyakazi wa mradi huo.

Hayo yalielezwa na Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani wakati alipokuwa akitoa taarifa ya mradi huo kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ambao walitembelea eneo la mradi lililopo wilayani Rufiji, Mkoa wa Pwani.

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, pamoja na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (wa nne kutoka mbele) wakiwa  katika eneo ambalo litatumika kutekeleza mradi wa umeme wa Rufiji (MW 2115) mara baada ya kufanya  ziara katika eneo la mradi huo.

Kamati hiyo ya Bunge pia ilikagua miundombinu wezeshi iliyotekelezwa na Serikali ikiwemo  Barabara, umeme, nyumba za Wafanyakazi na sehemu maalum ya kushushia mizigo katika Stesheni ya Tazara katika Kituo cha Fuga.

Dkt. Kalemani, alisema kuwa,  Mkandarasi huyo ameanza kazi za maandalizi mara baada ya kukabidhiwa eneo hilo la mradi mwezi wa Pili mwaka huu. 

Alisema kuwa, miongoni mwa kazi ambazo Mkandarasi  anaendelea kutekeleza kwa sasa ni ujenzi wa kambi ya muda ya Wafanyakazi, uletaji wa vifaa na mitambo itakayotumika wakati wa ujenzi pamoja na kazi za kuchukua sampuli za udongo na maji kwa ajili ya utafiti.

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani, (katikati), akizungumza na Wataalam wanaosimamia na wanaotekeleza mradi wa umeme wa Rufiji (MW 2115) mara baada ya kufika katika eneo la mradi huo akiwa ameambatana na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.

Aliongeza kuwa, mara baada ya kukamilisha kazi hizo za maandalizi Mkandarasi huyo anatakiwa kumaliza kazi ya ujenzi ndani ya miezi 36.

Alieleza kuwa, pamoja na kuridhishwa na hatua hiyo ya maandalizi, bado Serikali kupitia Wizara ya Nishati itaendelea kumsimania mkandarasi ili amalize kazi ndani ya muda uliopangwa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, Dunstan Kitandula,  baada ya kukagua miundombinu iliyotekelezwa na Serikali pamoja na kazi za maandalizi zinazofanywa na Mkandarasi, aliipongeza Serikali kwa kuamua kuutekeleza mradi huo na kuusimamia kikamilifu.

Alisema kuwa, Kamati hiyo pia inafuatilia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo ili uweze kukamilika kwa wakati kutokana na umuhimu wake nchini ambapo pia alitoa wito kwa Wizara kutorudi nyuma katika usimamizi wa mradi.

Pia, alitoa wito kwa wafanyabiashara hapa nchini kuchangamkia fursa zinazopatikana katika mradi kwani Serikali itatumia takribani shilingi Trilioni 6.5 kutekeleza mradi huo hivyo ni muhimu watanzania wafaidike na fedha hizo.

Katika ziara hiyo, viongozi mbalimbali waliambatana na Kamati hiyo akiwemo Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dkt Tito Mwinuka pamoja na wataalam kutoka kampuni inayotekeleza mradi huo.

Na Teresia Mhagama

14/3/2019