Mahakama ya Mwanzo katika Kata ya Somanda wilayani Bariadi Mkoa wa Simiyu, imeanza kupata huduma ya umeme kupitia Mradi wa usambazaji Umeme Vijijini wa Awamu ya Tatu (REA III).

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (wa nne kulia, waliokaa) akiwa katika eneo la Mahakama ya Mwanzo ya Somanda wilayani Bariadi baada ya kuwasha umeme katika Mahakama hiyo. Wa Tatu kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka na wengine katika picha ni Wafanyakazi kutoka Taasisi mbalimbali za Serikali.

Uzinduzi wa huduma hiyo, ulifanywa na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, Agosti 15, 2018 katika eneo la Mahakama ya Mwanzo ya Somanda akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Simiyu.

“Mahakama nyingi zilikuwa hazina umeme, na hii ni mojawapo ya changamoto ambayo inapekea kesi nyingi mahakamani  kuchelewa, hivyo kuwepo kwa huduma ya umeme kutasaidia shughuli mbalimbali zitakazosadia uharakishaji wa kutoa hukumu za kesi kwa wananchi, ” alisema Waziri Kalemani.

Dkt. Kalemani alisema kuwa, kipaumbele cha Serikali ni kupeleka nishati ya umeme katika Taasisi zote Umma ili ziweze kutoa huduma kwa wananchi kwa ufanisi.

Katika uzinduzi huo, Waziri Kalemani aliwakumbusha watendaji wa Mahakama hiyo kulipia bili zao za umeme kwa wakati ili kuepuka kukatiwa umeme na kusababisha usumbufu kwa wananchi.

Pia, aliliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuweka Transforma moja itakayohudumia mahakama hiyo pekee ili kuepuka changamoto ya kukosa umeme endapo itatokea hitilafu katika maeneo mengine.

“Wekeni Transfoma ya Mahakama kwa ajili ya Mahakama hii tu, ili ikitokea umeme umekatika katika maeneo mengine, hawa wasipate usumbufu ili wafanye kazi yao kwa ufanisi,” alisema Dkt. Kalemani.

Viongozi Waandamizi kutoka Wizara ya Nishati, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Wakala wa Nishati Vijijni (REA), Mahakama ya mwanzo ya Masonda wilayani Bariadi pamoja na Wananchi wakimsikiliza Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani)

Aidha, Dkt. Kalemani alikabidhi Vifaa cha Umeme Tayari (UMETA) 20 kwa Mahakama hiyo lengo likiwa ni kuhamasisha matumizi ya vifaa hivyo vya UMETA katika Taasisi za umma ambavyo havihitaji mteja kuingia gharama kubwa kusuka nyaya za umeme ndani ya nyumba.

Katika ziara yake mkoani Simiyu, Dkt. Kalemani pia, aliwasha umeme katika kijiji cha Songambele kata ya Ipililo wilayani Maswa.