Makatibu Wakuu na Wataalam wa Wizara mbalimbali kutoka nchi zinazounda Jumuiya ya Afrika Mashariki ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda Burundi, Rwanda na Sudan ya Kusini wamekutana nchini Uganda ili kujadili masuala mbalimbali yanayohusu Jumuiya hiyo.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Edith Mwanje ambaye pia ni Mwenyekiti wa kikao cha Makatibu Wakuu na Watalaam kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki akizungumza katika kikao hicho.

Katika kikao kilichofanyika Kampala nchini Uganda, Makatibu Wakuu hao na wataalam walijadili ripoti kuhusu masuala ya Biashara, Fedha, Ushuru, Siasa, Miundombinu na Afya iliyokabidhiwa katika kikao cha Mawaziri wa Jumuiya hiyo kilichofanyika kuanzia tarehe 19 na kitahitimishwa tarehe 21 Februari, 2018.

Wizara kutoka Tanzania zilizohudhuria kikao hicho ni Wizara ya Nishati, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Wizara ya Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano,  Wizara ya Katiba na Sheria, Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Wizara ya Afya, Wazee Jinsia na Watoto na Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Zanzibar.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. Hamisi Mwinyimvua (wa kwanza kulia waliokaa) akiwa katika kikao cha Makatibu Wakuu na Wataalam ambao wamehudhuria Mkutano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki nchini Uganda, wa pili kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Sheria na Katiba, Amon Mpanju, wa tatu kutoka kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Siasa, Ulinzi na Usalama Stephen Mbundi katika Wizara ya Mambo ya Nje, wa nne kutoka kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, na wa kwanza kushoto ni Katibu Mkuu wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Joseph Nyamhanga.

Wizara ya Nishati iliwakilishwa na Katibu Mkuu, Dkt Hamis Mwinyimvua aliyeambatana na Kaimu Kamishna wa Nishati, Mhandisi Innocent Luoga, Mjiolojia Mkuu, Adam Zuberi pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dkt. Tito Mwinuka.