Mawaziri wanaohusika na utekelezaji wa mradi wa umeme wa maji wa Rusumo (MW 80)  kutoka Tanzania, Rwanda na Burundi wamekagua kazi ya ujenzi wa mradi huo wilayani Ngara mkoa wa Kagera na kutoa maelekezo mbalimbali yatakayowezesha kasi ya utekelezaji wa mradi huo kuongezeka.

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (katikati), Waziri wa Nishati na Migodi wa Burundi, Come Manirakiza (kushoto kwa Dkt. Kalemani) na Waziri wa Miundombinu wa Rwanda, Claver Gatete (kulia kwa Dkt Kalemani) wakiwa katika kikao chao na wataalam mbalimbali wanaosimamia mradi wa umeme wa Rusumo kilichofanyika Rusumo mkoani Kagera.

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani ndiye aliyewaongoza, Waziri wa Nishati na Migodi wa Burundi, Come Manirakiza na Waziri wa Miundombinu wa Rwanda, Claver Gatete katika kukagua kazi mbalimbali zinazoendelea kufanyika ikiwemo ujenzi wa eneo itakapojengwa mitambo ya kuzalishia umeme na ujenzi nyumba za wafanyakazi.

Baada ya kukagua kazi zinazoendelea kufanyika, Mawaziri hao walifanya kikao chini ya uenyekiti wa Dkt Medard Kalemani na kuiagiza Bodi ya Wakurugenzi ya mradi huo kusimamia ipasavyo kazi mbalimbali za ujenzi ili mradi huo ukamilike mwaka 2020 kama ilivyo katika makubaliano.

Dkt. Kalemani alisema kuwa, kazi ya ujenzi wa mradi huo ilianza mwezi Februari mwaka 2017 na inapaswa kukamilika ndani ya miezi 36 hivyo Bodi hiyo yenye wajumbe kutoka nchi zote Tatu ihakikishe kuwa mkandarasi anakamilisha kazi kwa wakati.

“Pia tumeiagiza Bodi na wataalam walioko katika mradi huu, wahakikishe kuwa wanashirikisha Mamlaka na Taasisi mbalimbali zilizopo katika maeneo ya mradi katika nchi zote Tatu hasa katika masuala yanayohusu jamii zinazozunguka mradi na stahili za wafanyakazi ili kutokuwa na vikwazo katika utekelezaji,” alisema Dkt Kalemani.

Kuhusu faida za mradi huo, alisema kuwa, kila nchi itapata megawati 27 na kujenga miundombinu ya usafirishaji umeme wa kV 220 ambapo kwa upande wa Tanzania, itajengwa miundombinu hiyo kutoka Rusumo kwenda Nyakanazi  kwa umbali wa kilometa 98.

Aliongeza kuwa, miundombinu hiyo ya usafirishaji umeme, kwa upande wa Tanzania, itaingiza umeme katika gridi ya Taifa kupitia njia  ya umeme inayotoka Geita na kwamba, vijiji  13 vinavyopitiwa na mradi wa Rusumo vitasambaziwa nishati hiyo.

Maporomoko ya maji ya Mto Kagera, yatakayotumika kuzalisha umeme wa megawati 80 kwa ajili ya nchi za Tanzania, Rwanda na Burundi.

Kuhusu gharama za mradi, alisema kuwa, kila nchi imegharamia mradi huo kupitia wadau wa maendeleo ambao ni Benki ya Maendeleo Afrika (AfdB) na Benki ya Dunia (WB) ambapo kwa ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme kila nchi imechangia takribani Dola za Marekani milioni 113.

Kwa upande wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme, alisema kuwa kila nchi imechangia kiasi cha Dola za Marekani milioni 36.7.

Kwa ujumla, alisema kuwa, Mawaziri wa nchi hizo Tatu wameazimia kuwa, mradi huo utekelezwe kwa kasi usiku na mchana bila kuwa na visingizio na kama kuna muda uliopotezwa na mkandarasi wa mradi, ufidiwe kwa njia mbalimbali ikiwemo kuongeza nguvu kazi.

Aidha, ili kuongeza usimamizi katika mradi huo, Mawaziri hao  ambao kwa kawaida hukutana kila baada ya miezi Sita, wameamua kufanya vikao vya dharura kila itakapohitajika ili kuhakikisha kuwa yale wanayoaagiza yanatekelezwa kwa ufanisi.

Na Teresia Mhagama.