Mawaziri kutoka Wizara Tano zinazohusika na utekelezaji wa mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanzania, wamekutana na wataalam wa Tanzania walio katika Timu ya Kitaifa ya Majadiliano ya mradi ili kupata taarifa ya  utekelezaji wa mradi huo unaotarajiwa kukamilika mwaka 2020.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ( katikati), Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba (kulia kwa Waziri wa Nishati), Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula (kushoto kwa Waziri wa Nishati), Naibu Waziri wa Kazi, Vijana na Ajira, Antony Mavunde (haonekani pichani) na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji (haonekani pichani) wakiwa katika kikao kilichokuwa kikijadili mradi wa Bomba la Mafuta jijini Dodoma. Wengine ni Watendaji kutoka Wizara ya Nishati na Taasisi mbalimbali za Serikali.

Kikao hicho  kilichoongozwa na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani kimefanyika katika Ofisi za Wizara ya Nishati jijini Dodoma ambapo Mawaziri waliohudhuria kikao hicho ni  Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba,  Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,  Dkt. Angeline Mabula,  Naibu Waziri wa Kazi, Vijana na Ajira,  Antony Mavunde na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango,  Dkt. Ashatu Kijaji.

Viongozi wengine  waliohudhuria ni  Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. Hamisi Mwinyimvua,  Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Charles Kichere na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya  Usimamizi wa Bandari, Mhandisi Karim Mataka na  Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo  ya Petroli Tanzania (TPDC),Mhandisi Kapuulya Musomba.

Pamoja na  kupata taarifa ya utekelezaji wa mradi wa Bomba la Mafuta kutoka katika Timu hiyo ya Taifa ya Majadiliano (GNT), Mawaziri hao pamoja na wataalam mbalimbali walijadili changamoto  mbalimbali pamoja na utatuzi wake lengo likiwa ni kutekeleza mradi huo kwa ufanisi ndani ya muda uliopangwa.

Kwa ujumla Mawaziri hao walipongeza wataalam katika Timu hiyo ya majadiliano kwa kutekeleza masuala mbalimbali yanayohusu mradi na kutanguliza maslahi ya nchi katika majadiliano yao na wawekezaji wa mradi huo.

Aidha, walitoa maelekezo mbalimbali yanayopaswa kufanyiwa kazi na wataalam ili kuboresha mchakato wa utekelezaji wa mradi  ikiwemo masuala ya ulipaji fidia wananchi watakaopisha mradi, upatikanaji  wa ardhi litakapopita Bomba la Mafuta ghafi na suala la Hisa.

Kwa upande wake, Waziri wa Nishati, aliwaagiza wataalam hao kuhakikisha kuwa, makubalino mbalimbali kati ya Tanzania na pande nyingine zinazohusika na mradi huo yanakamilika ifikapo mwezi Septemba mwaka huu.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ( katikati), Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba (kulia kwa Waziri wa Nishati), Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula (kushoto kwa Waziri wa Nishati), Naibu Waziri wa Kazi, Vijana na Ajira, Antony Mavunde (haonekani pichani) na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji (haonekani pichani) wakiwa katika kikao kilichokuwa kikijadili mradi wa Bomba la Mafuta jijini Dodoma. Wengine ni Watendaji kutoka Wizara ya Nishati na Taasisi mbalimbali za Serikali.

Aidha alisema kuwa, kama kuna marekebisho mbalimbali ya kisheria yanayohitajika ili kutekeleza mradi kwa ufanisi, yaainishwe mapema ili yaweze kufanyiwa kazi.

Wawekezaji katika mradi huo ni Kampuni za Total E&P ya Ufaransa, Tullow Oil ya Uingereza, China National Offshore Oil Company (CNOOC) na kampuni za Mafuta za Taifa za Tanzania na Uganda.

Na Teresia Mhagama-Dodoma.