Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu amewataka Wakuu wa Mikoa kuingiza Agenda ya   Nishati katika vikao vya Maendeleo vya mikoa kwa kuwa sekta hiyo ni kichocheo kikuu cha sekta nyingine kiuchumi na kimaendeleo.

Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu akimweleza jambo Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Zainab Taleck (katikati) alipomtembelea ofisini kwake wakati wa ziara yake mkoani humo. Wanaofuatilia ni watendaji walioambatana na Naibu Waziri kutoka Wizara ya Nishati, TANESCO na REA na Watumishi wa Mkoa wa Shinyanga.

Aliyasema hayo wakati alipomtebelea Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga ofisini kwake wakati wa ziara ya kukagua  utekelezaji wa Mradi wa Usambazaji Nishati vijijini unaotekelezwa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) mkoani humo.

Aliongeza kuwa, ili sekta zote ziweze kuendelea zinahitaji nishati ya umeme hivyo imefika hatua ambayo masuala ya nishati ni muhimu yakapewa nafasi katika vikao hivyo vya maendeleo kwa kuwa ikiwa haitapewa nafasi inaweza kuchangia kupUnguza kasi ya maendeleo tarajiwa.

Aidha, akizungumza kwa nyakati tofauti katika mikutano ya hadhara katika vijiji vya Itwangi na Nyambui, Mgalu amesisitiza kuhusu Wakandarasi wanaotekeleza miradi hiyo kuhakikisha kuwa wanaripoti katika ofisi za Serikali kuanzia ngazi za Vijiji, Wilaya na Mikoa ili kuweka mazingira bora na rafiki ya utekelezaji ka wa miradi husika.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Zainabu Taleck, amelitaka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoani humo kuwasilikiza wateja na kuhakikisha linasambaza nishati hiyo kwa wananchi wengi zaidi ikizingatia kuwa, mahitaji ya umeme hususani maeneo ya mijini yamekuwa makubwa.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Josphine Matiro aliiomba wizara kuwafikiria wananchi ambao wako tayari kuchangia ili kupata huduma ya nishati hususan kwa walio katika maeneo ya pembezoni.

Msimamizi wa Mradi wa REA Hussein Shemdasi, (kulia) akimtambulisha Mkandarasi wa Mradi wa REA Mkoa wa Shinyanga kutoka kampuni ya Angelic (kushoto).

Naye Msimamizi wa Mradi wa REA Hussein Shemdasi, amewataka wananchi watakaounganishwa na huduma ya umeme kuutumia kwa uzalishaji ili kujiongezea kipato. Pia, alisisitiza kuhusu wakandarasi kushirikiana na viongozi wa Serikali ili kuwezesha mradi huo kutekelezwa kikamilifu.

Kwa upande wake, Meneja wa Tanesco Kanda ya Magharibi Macline Mbonile aliwataka wananchi kufanya maandalizi kipindi cha mradi ili wanapofikiwa wakati wa utekelezaji waweze kuunganishwa na huduma hiyo.