Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amewataka watendaji wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kujitathmini katika kazi ya upangaji wa Vijiji vinavyosambaziwa umeme nchini ili kuepusha migogoro kati ya Serikali na wananchi.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, akikata utepe kuashiria uzinduzi wa umeme katika Kijiji cha Mwazye wilayani Kalambo mkoa wa Rukwa, wa Tatu kushoto ni Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Josephat Kandege na wa kwanza kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, Julieth Binyura.

Naibu Waziri aliyasema hayo katika Kijiji cha Matai, wilayani Kalambo mkoa wa Rukwa wakati alipofika kukagua kazi ya usambazaji umeme akiwa ameambatana na Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Josephat Kandege ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Kalambo.

Naibu Waziri alitoa agizo hilo, baada ya kufanya ziara katika maeneo mbalimbali mkoani Rukwa na kuona kuwa, vijiji vingi vimepitiwa na miundombinu ya umeme lakini havijaunganishwa na huduma hiyo na Vijiji vingine vipo kilomita chache kutoka ilipo miundombinu ya umeme lakini havina umeme.

Aidha, akiwa katika Kata ya Mtowisa na Kipeta wilayani Sumbawanga alieleza kusikitishwa kwake na kata hizo kutowekwa katika miradi ya awali ya usambazaji umeme vijijini kwani wananchi katika maeneo hayo yaliyo katika Bonde la Ziwa Rukwa ni wazalishaji wakubwa wa mazao ya mahindi na mpunga ambayo yanaweza kuongezewa thamani kukiwa na nishati ya umeme.

Alisema kuwa, katika Kata ya Mtowisa, Serikali tayari imeshatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ambayo inahitaji nishati ya umeme, pia kuna sehemu zinazotoa huduma kwa jamii kama Mahakama, Polisi, Vituo vya Afya na Shule ambazo zinahitaji umeme ili kufanya kazi kwa ufanisi.

Alisisitiza kuwa, Serikali haitavumilia mapungufu yanayojitokeza ya urukaji wa Vijiji huku vikiwa na vigezo vyote vya kupatiwa umeme, ikiwemo kupitiwa na miundombinu ya umeme.

“Serikali imedhamiria kupeleka umeme katika Vijiji vyote nchini hadi kufikia mwaka 2021 lakini miradi hii inafanyika kwa awamu tofauti, hivyo mnapofanya uchaguzi wa Vijiji katika Awamu hizo ni lazima mshirikishe viongozi mbalimbali kama wa Mikoa na Wilaya kwani ndio wanaofahamu mahitaji ya umeme katika Vijiji,” alisema Mgalu.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (wa pili kushoto) akisalimiana na viongozi wa Kijiji cha Matai wilayani Kalambo wakati alipofika kijijini hapo kukagua kazi ya usambazaji umeme.

Katiza ziara yake ya kikazi wilayani Kalambo, Naibu Waziri wa Nishati pia alizindua huduma ya umeme katika Kijiji cha Mwazye ambapo wananchi mbalimbali walieleza kufurahia huduma hiyo ambayo itawawezesha kufanya shughuli mbalimbali kama kufunga mashine za kukoboa nafaka badala ya kusafirisha zikiwa ghafi.