Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amewataka wakandarasi wanaojenga miundombinu ya  usambazaji wa umeme vijijini chini ya  Wakala wa Nishati  Vijijini Awamu ya  Tatu (REA III) kuongeza kasi  ili miradi yote iweze kukamilika ifikapo mwaka 2019.

Mgalu aliyasema hayo mapema leo  tarehe 15 Desemba, 2017 katika ziara yake aliyoifanya katika kijiji cha Bwitini wilayani Korogwe mkoani Tanga, lengo likiwa ni kukagua hatua  ya utekelezaji wa miradi ya  umeme vijijini iliyopo chini ya REA Awamu ya Tatu na kutorishishwa na kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo.

Msimamizi wa Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Pangani kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi Mahenda S. Mahenda (kulia) akitoa maelezo kuhusu uzalishaji wa umeme katika kituo hicho kwa Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (kushoto) katika ziara aliyoifanya mapema leo tarehe 15 Desemba, 2017 katika kituo hicho.

Katika ziara hiyo Naibu Waziri Mgalu aliambatana na watendaji kutoka Wizara ya Nishati, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Alisema kuwa, Serikali ilikwishawalipa wakandarasi wote malipo ya awali na kuwataka kuanza kazi mara moja lakini wamekuwa wakifanya katika kasi ndogo hususan katika hatua ya upembuzi yakinifu.

“Wakandarasi wengi wamekuwa wakichukua muda mrefu kutekeleza miradi kwa kisingizio cha kufanya upembuzi yakinifu wakati fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi zimekwishatolewa, nichukue fursa hii kuwatangazia wakandarasi wote nchini kuanza kazi mara moja,” alisema Mgalu

Aliendelea kusema kuwa mkandarasi yeyote atakayefanya kazi kwa kiwango kisichoridhisha atanyang’anywa kazi na kupewa mkandarasi mwingine mwenye uwezo wa kufanya kazi kulingana na kasi inayotakiwa na Serikali.

Alisema kuwa wananchi wengi kwa sasa hususan walipo katika maeneo ya vijijini wanahitaji nishati ya umeme kwa gharama nafuu, hivyo wamechoka na masuala ya michakato.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Mgalu aliwataka wakandarasi wote nchini kununua vifaa kutoka ndani ya nchi hususan transfoma na nguzo badala ya kuagiza kutoka nje ya nchi kama ilivyoagizwa awali.

Akielezea mikakati ya serikali katika uboreshaji wa upatikanaji wa umeme wa uhakika na kwa gharama nafuu, Mgalu alisema kuwa serikali kupitia REA Awamu ya Tatu  inasambaza umeme katika vijiji vyote nchini ambapo  ifikapo mwaka 2019 karibia vijiji vote vitakuwa na umeme wa uhakika.

Aliendelea kuelezea mikakati mingine kuwa ni pamoja na matumizi ya nishati  jadidifu kama vile jua hususan katika maeneo yasiyofikiwa na umeme kutoka Gridi ya Taifa, ujenzi wa  mradi  wa kuzalisha umeme  kwa kutumia maporomoko ya maji ya Mto  Rufiji wa Stieglers Gorge na mradi wa kuzalisha  umeme kwa kutumia  gesi asilia wa Kinyerezi I na Kinyerezi II.

Alisisitiza kuwa serikali imeweka mkakati wa kufufua mkoa wa Tanga kiuchumi hivyo kuwataka wawekezaji ndani ya nchi kuwekeza kwenye viwanda katika mkoa huo.

Alieleza kuwa kutokana na uwepo wa mradi mkubwa wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga nchini Tanzania katika mkoa wa Tanga, mahitaji ya umeme yatakuwa makubwa hivyo Wizara ya Nishati imejipanga katika kuhakikisha kuwa nishati ya uhakika inapatikana.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (wa pili kulia) akitoa maelekezo kwa watendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) katika ziara hiyo.

Wakati huo huo Naibu Waziri Mgalu aliwataka wananchi wa Tanga kutoharibu vyanzo vya maji katika Bonde la Mto Pangani yanayotumiwa katika uzalishaji wa umeme katika kituo cha kufua umeme cha Hale ili kutoathiri uzalishaji wa umeme katika mkoa huo.

Alisisitiza kuwa serikali haitasita kuwachukulia hatua hali za kisheria wananchi watakaobainika wanaharibu mazingira.

Na Greyson Mwase, Tanga