Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa Majaliwa amezindua mradi wa umeme ambao umewezesha mikoa ya Lindi na Mtwara kuunganishwa katika gridi ya Taifa.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa Majaliwa (katikati) akiwa katika chumba cha kuongozea mitambo katika Kituo cha kupoza umeme cha Mahumbika mkoani Lindi baada ya kuzindua kituo hicho ambacho kimewezesha kuunganisha mikoa ya Lindi na Mtwara katika Gridi ya Taifa. Kushoto kwake ni Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani na kulia kwa Waziri Mkuu ni Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi.

Waziri Mkuu, amezindua mradi huo tarehe 21 Mei, 2018 katika kijiji cha Mahumbika mkoani Lindi ambapo uzinduzi huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani, Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Dkt. Hamisi Mwinyimvua, Wabunge wa mikoa ya Lindi na Mtwara, Wakuu wa Mikoa na Wilaya za Lindi na Mtwara, Kaimu Kamishna wa Nishati, Eng. Innocent Luoga, Wenyeviti wa Bodi na watendaji wa Taasisi zilizo chini ya Wizara.

Awali, mikoa hiyo ilikuwa ikipata umeme kutoka katika kituo cha cha kufua umeme wa Gesi Asilia cha Somanga Fungu na Mtwara lakini sasa itapata pia umeme wa Gridi kutokea katika kituo cha kupoza umeme cha Mbagala na hivyo kuimarisha hali ya upatikanaji umeme katika mikoa hiyo.

Akizungumza na Wananchi waliohudhuria hafla hiyo, Waziri Mkuu alisema kuwa mikoa ya Lindi na Mtwara ilikuwa ina changamoto ya upatikanaji wa umeme lakini kwa sasa inaanza kupata umeme wa uhakika ambao utapelekea vijiji vingi zaidi kusambaziwa huduma hiyo.

Hivyo, Waziri Mkuu, alitoa agizo kwa Wakandarasi wanaosambaza umeme vijijini, kuharakisha utekelezaji wa kazi hiyo ili wananchi waweze kufanya shughuli mbalimbali ikiwemo za kiuchumi.

Aidha, alitoa agizo kwa Wakurugenzi wa Halmashauri nchini kuhakikisha kuwa sehemu zinazotoa huduma za kijamii kama Shule, visima vya maji na vituo vya afya zinapata nishati ya umeme ili ziweze kutoa huduma ya uhakika kwa wananchi.

Vilevile, aliwaagiza wakandarasi wanaosambaza umeme nchini kuhakikisha kuwa wanaunganisha umeme bila kubagua ubora wa nyumba, lakini aliwaasa wananchi kuendelea kujenga nyumba bora.

Kuhusu uzalishaji umeme nchini, alisema kuwa, Serikali inakaribisha wawekezaji binafsi kuzalisha umeme na kueleza kuwa Serikali inaendelea kutekeleza miradi ya uzalishaji umeme ukiwemo wa Rufiji (MW 2100) na Mtwara (MW 300).

Waziri Mkuu, pia alitoa pongezi kwa Wizara ya Nishati na  Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa juhudi wanazofanya katika kuhakikisha kuwa nchi inakuwa na umeme wa kutosha na wa uhakika na kuwataka waendelee kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Kwa upande wake, Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, alisema kuwa, kukamilika kwa kituo cha kupoza umeme cha Mahumbika kumepelekea wilaya mbalimbali mkoani Lindi, kupata umeme wa uhakika ikiwemo Ruangwa, Masasi na Nachingwea.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa Majaliwa (kushoto) akisalimiana na Kaimu Kamishna wa Nishati, Mhandisi Innocent Luoga kabla kuzindua kituo cha kupoza umeme cha Mahumbika ambacho kimewezesha kuunganisha mikoa ya Lindi na Mtwara katika Gridi ya Taifa. Kulia kwa Kaimu Kamishna ni Mbunge wa Nachingwea, Hassan Masala na kushoto kwa Kaimu Kamishna ni Mbunge wa Mtwara Vijijini, Hawa Ghasia.

Aliongeza kuwa, kukamilika kwa kituo hicho kumetoa matumaini ya kuiunganisha Wilaya ya Liwale na kituo cha kupoza umeme cha Mahumbika na hivyo kuachana na matumizi ya majenereta ya mafuta yanayotumika kufua umeme.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dkt. Tito Mwinuka, alisema kuwa, kukamilika kwa kituo cha kupoza umeme cha Mahumbika, kumetoa unafuu wa megawati 2.5 kwenye mitambo ya kufua umeme ya Mtwara hivyo kuboresha hali ya umeme katika mkoa wa Mtwara.

Aliongeza kuwa, kupatikana kwa umeme wa uhakika katika Mikoa ya Lindi na Mtwara kutavutia zaidi wawekezaji hususan kwenye Sekta ya Viwanda hivyo kuboresha maisha ya wananchi na kuongeza pato la Serikali.

Na Teresia Mhagama, Lindi.