Shirika la Umeme Tanzania limeagizwa kumchukulia hatua Mkandarasi ambaye ni kampuni ya wazawa ya JV State Grid Electrical & Technical Works Ltd aliyekuwa akitekeleza Mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Pili (REA II) Mikoa ya Mbeya na Songwe kwa kushindwa kukamilisha katika baadhi ya maeneo kwa mujibu wa makubaliano.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu ametoa agizo hilo Januari 5, 2018 kwenye mkutano na wananchi wa Kijiji cha Utengule Usongwe, Mbeya Vijijini alipokuwa kwenye ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi ya Umeme Vijijini hususan Miradi ya Umeme iliyo chini ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Mgalu alitoa agizo hilo kufuatia taarifa ya Meneja wa TANESCO Mkoa wa Mbeya, Mhandisi Benedict Bahati ambaye alimueleza kuhusu kampuni hiyo iliyokuwa ikitekeleza Miradi katika Wilaya za Mbarali, Rungwe, Kyela na Ileje kushindwa kukamilisha miradi yake kama ilivyopaswa kulingana na mkataba.

Alisema Serikali haitowafumbia macho Wakandarasi walioshindwa kukamilisha utekelezaji wa Miradi waliyokabidhiwa kwa mujibu wa makubaliano na aliliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuhakikisha Mkandarasi huyo anapatikana na hatua za kisheria zinachukuliwa dhidi yake kwa mujibu wa makubaliano ya awali.

Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Utengule Usongwe, Mbeya Vijijini wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza kwenye ziara yake ya kukagua utekelezaji wa Miradi ya Umeme Vijijini Mkoani Mbeya.

“Serikali haijaribiwi, tutachukua hatua kwa Wakandarasi wote walioshindwa kutekeleza miradi waliyokabidhiwa kwa mujibu wa sheria; TANESCO na REA, hakikisheni Mkandarasi huyu anapatikana na hatua stahiki za kisheria zinachukuliwa dhidi yake,” alisema Mgalu.

Mgalu aliagiza Mkandarasi huyo apatikane ndani ya Siku Saba ili aeleze sababu za kushindwa kutekeleza mradi huo kwa kiwango kilichokubaliwa na kwa muda wa makubaliano. “Nataka ndani ya Siku Saba tukutane nae aeleze kwanini hajakamilisha mradi kwa mujibu wa mkataba wake,” alisema.

Aliongeza kuwa Serikali imedhamiria kuwainua Wakandarasi wazawa hata hivyo katika utekelezaji wa miradi hiyo ya REA, imedhihirika kwamba walio wengi wameshindwa kutekeleza miradi waliyokabidhiwa kwa mujibu wa makubaliano.

Mgalu aliwaasa Wakandarasi wazawa waliopewa jukumu la kutekeleza baadhi ya miradi kuhakikisha wanafanya shughuli zao kwa uadilifu na kwa mujibu wa makubaliano na kwamba Serikali itaendelea kuwapatia ushirikiano unaohitajika.

Naibu Waziri Mgalu yupo Mkoani Mbeya kwa ziara ya siku Tatu ya kukagua na kujiridhisha utekelezaji wa Miradi ya Umeme Vijijini hususan ya REA pamoja na kuzungumza na Wananchi na Wakandarasi kuhusiana na utekelezaji wake.