Waziri wa Nishati, Dkt. Medard kalemani  amefungua mkutano wa 51 wa nchi 12 washirika wa Muungano wa Mfumo wa Usafirishaji Umeme Kusini mwa Bara la Afrika (SAPP) uliofanyika mjini Arusha Septemba 6, 2018.

Mkutano huo ulikutanisha nchi washirika kwa lengo la kujadili masuala muhimu kuhusu sekta ya Nishati katika bara la Afrika.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akizungumza wakati wa Uzinduzi wa mkutano wa 51 wa nchi 12 washirika wa muungano wa mfumo wa usafirishaji umeme Kusini mwa Bara la Afrika (SAPP) uliofanyika Arusha.

Akizungumzia mkutano huo, Dkt Kalemani alisema kuwa mkutano ulijadili malengo makuu matatu ambayo ni kuimarisha na kuboresha miundombinu ya  usafirishaji umeme mkubwa wa  kV 400 kwa nchi wanachama ambapo kwa sasa Tanzania ipo katika utekelezaji wake.

Malengo mengine ni kuweka mipango madhubuti ya namna ya kushirikiana katika sekta ya Nishati kwa nchi hizo pamoja na kuimarisha uzalishaji na upatikanaji wa umeme na kuuziana kwa bei nafuu na kwa masharti nafuu kwa kuwa miundombinu imejengwa kwa kushirikiana.

” SAPP imefanyika wakati muafaka nchini kwetu, sababu tunatekeleza miradi mikubwa ya kusambaza umeme wa kV 400 hii ni fursa nzuri kwetu, pia kwa Malawi na Angola ambao pia wanajenga miundombinu na hawajalamilisha hivyo tutapata uzoefu kwa waliotangulia, ” alisema Kalemani.

Alisema kuwa Tanzania inajenga mradi mkubwa wa kusafirisha umeme wa kV 400 kutoka Iringa, Singida, Manyara, unakwenda mpaka Namanga-Kenya hadi Zambia (Zambia-Tanzania-Kenya interconnector)  ambao utaunganisha umeme kati ya nchi za Kusini mwa Afrika na Kaskazini mwa Afrika.

Akitolea mfano nchi kuuziana umeme, Dkt.Kalemani alisema kuwa Tanzania ikimaliza miradi yake yote mikubwa ya kuzalisha umeme ukiwemo wa Rufiji, Somanga Fungu na Mtwara itawauzia nchi wanachama endapo watahitaji umeme na ikitokea yenyewe ina uhaba pia ni rahisi kununua umeme kwa gharama nafuu kutoka nchini nyingine kupitia miundombinu ya usafirishaji umeme iliyojengwa kwa ushirikiano.

Alitaja nchi 12 wanachama waliohudhuria mkutano huo kuwa ni  Tanzania, Kenya, Zambia, Zimbabwe, Afrika Kusini, Namibia, Angola, Botswana, Swaziland, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Msumbiji na  Malawi.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, (katikati) akisikiliza majadiliano wakati wa mkutano wa 51 wa nchi 12 washirika wa muungano wa mfumo wa usafirishaji umeme kusini mwa Bara la Afrika, uliofanyika Arusha.

Kwa upande wake,  Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Dkt. Tito Mwinuka alisema kuwa kwa sasa Tanzania ipo katika hatua nzuri za kuunganisha miundombinu ya kusafirisha umeme na nchi za Kusini  mwa Afrika kupitia mradi mkubwa wa kV 400 kutokea Iringa, Mbeya, Tunduma hadi nchini Zambia.

Alisema mradi huo utasaidia kupata umeme kutoka nchi jirani pale itakapohitajika na kwamba utapatikana kwa bei nzuri kutokana na kuwepo kwa ushindani wa bei kutoka kwa nchi wanachama.

Aliongeza kuwa  TANESCO inaendelea kuboresha na kuimarisha upatikanaji wa huduma ya umeme nchini kwa kufanya matengenezo ya miundombinu, kubadilisha na kuondoa ile iliyoharibika ili kuondoa adha ya kukatika kwa umeme inayotokana na changamoto za miundombinu kwa kuwa kwa sasa Tanzania ina umeme wa kutosheleza mahitaji.

Na Zuena Msuya