Vijana zaidi ya 200 wamepata ajira ya kufanya  utafiti  wa athari za kijamii na kiuchumi katika njia ya Bomba la Mafuta Ghafi la  Afrika Mashariki kutoka Hoima Nchini  Uganda hadi katika Bandari ya Tanga nchini Tanzania.

Vijana hao tayari wamepata mafunzo ya kazi  yaliyotolewa jijini Dar es Salaam na kampuni ya Digby Wells Consortium (DWC) kwa kushirikiana kampuni nyingine  za kitanzania na za  kimataifa kama  Digby Wells Environmental ( kampuni ya kimataifa yenye makao makao makuu nchini Afrika ya Kusini na Uingereza) na Paulsam Geo-Engineering Ltd (Kampuni ya Kitanzania inayotoa huduma za ushirikishwaji wadau, upimaji wa ardhi na  watakwimu wa mambo ya kijamii na uchumi).

Kampuni nyingine zilizotoa mafunzo kwa vjana hao ni Whiteknights Real Estate Investment Analysts Ltd (kampuni ya Kitanzania inayotoa huduma za uthamini) na STCL (kampumi ya Kitanzania  inayotoa huduma za Afya na usalama na usafiri kwa makampuni ya  DWC).

Lengo la mafunzo hayo lilikuwa ni kuwapa wahusika uelewa wa kufanya  tathmini  ya athari mbalimbambali za  kiuchumi na kimazingira katika maeneo yatakayopitiwa na Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki.

Pichani ni vijana waliopata ajira wakiwa katika mafunzo hayo.

Mara baada ya kumalizika kwa mafunzo  husika, vijana  wataanza kazi  tarehe 16 Mei, 2018 chini ya kampuni ya kizalendo ya Paulsam ambayo ni mkandarasi  anayetekeleza kazi hiyo kwa kushirikiana na kampuni nyingine.

Zoezi hili litatekelezwa na Makundi 9 yatakayogawanyika katika Mikoa 8 bomba linapopita, Wilaya 25, kata 132 na Vijiji Zaidi ya 280. Aidha, zoezi litahusisha  kubaini athari za utwaaji ardhi  kwa ajili ya  Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), na kutengeneza mifumo ya kuzuia, kupunguza na kudhibiti athari mbaya kwa watakaoguswa na mradi, na kutengeneza mpango wa uhamishaji makazi kupisha Mradi wa Ujenzi wa Boma la Mafuta

Kazi hii inajumuisha  ukusanyaji wa  taarifa za  ardhi na  rasilimali  kwa ajili ya uthamini na hatimaye  utwaaji wa ardhi ambayo itahitajika kwa ajili ya ujenzi wa njia ya bomba la mafuta  kabla  ya muda wa kuanza ujenzi.

Zoezi hili litahusisha pia, uorodheshaji wa mali zote zisizohamishika na makaburi ndani ya eneo lililochaguliwa na mradi.

Zoezi litatekelezwa kwa kutumia teknolojia ya vifaa vya kisasa (tablets)  kuchukua na kutunza takwimu. Mwisho fomu yenye rekodi itatolewa na kusainiwa na wahusika wote na nakala atapewa mhusika na kusaidia kubaini namna wahusika watakavyokuwa wameathirika.

Katika zoezi hilo vijana watafanya kazi kwa kushirikiana na wataalam kutoka Wizara ya Nishati, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC).