Naibu wa Nishati, Subira Mgalu amesema kuwa ujenzi wa mradi mkubwa wa uzalishaji umeme kwa kutumia maporomoko ya maji ya Bonde la mto Rufiji (MW 2100) hautakuwa na athari katika ujenzi wa gati la Nyamisati litakalotumiwa na vyombo vya usafiri kusafirisha abiria na mizigo yao kwenda Kisiwa cha Mafia ambapo ujenzi huo umetengewa kiasi cha shilingi bilioni 14.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (katikati) akitoa maelekezo kwa Meneja wa ujenzi wa Gati ya Nyamisati kutoka Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) Erick Madinda (kushoto) wakati Naibu waziri huyo alipotembelea eneo hilo.

Mgalu alisema hayo katika Kijiji cha Nyamisati wilayani Kibiti alipokuwa akizungumza na wananchi mara baada ya kutembelea ujenzi wa gati hilo.

Alisema  mradi wa ujenzi kuzalisha umeme katika bonde la mto Rufiji, umefanyiwa utafiti wa kina na kubaini  kuwa hautakuwa na athari zozote za kimazingira, tofauti na baadhi ya watu waliokuwa wakidai kuwa mara baada ya ujenzi huo, kina cha maji katika eneo litakalojengwa  gati kitapungua.

“Hakutakuwa  na athari za kimazingira kama baadhi ya watu wanavyosema kwani wataalam walifanya upembuzi yakinifu na haukuonyesha kuwa kutakuwa na athari yoyote ya kimazingira,” alisema Mgalu.

Alibainisha kuwa, maji kwenye eneo la gati siyo ya mto pekee bali ni pamoja na yale ya bahari kwakuwa hapo ndipo maji yanapoungana kati ya maji ya bahari na yale ya mto .

Aidha alisema kuwa, miradi yote ina faida kubwa kwa wananchi na Taifa kwa ujumla na kwamba Serikali imetumia wataalam kufanya utafiti na kujiridhisha katika kutekeleza  mradi huo.

Mgalu alifafanua kuwa, miradi yote ni ya manufaa hivyo wananchi wawe tayari kuipokea muda wote pale ambapo Serikali inataka kuitekeleza na pia wasidanganywe ama kupotoshwa na watu wachache kwa lengo la kukwamisha ama kuchelewesha mradi hiyo.

Vilevile watumie fursa ya miradi hiyo hiyo, katika kujiletea maendeleo na kuongeza kipato kwa kufanyakazi na biashara mbalimbali zitakazokuwa zinajitokeza wakati huo na hata baada.

Naye Meneja wa ujenzi wa mradi wa gati la Nyamisati kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Mhandisi Erick Madinda,  alisema kuwa maji hayawezi kupungua mara litakapojengwa bwawa kubwa la kuzalishia umeme katika bonde la mto Rufiji.

Madinda alisema kuwa,  eneo hilo ni sehemu ambapo kuna mwingiliano wa mto na bahari hivyo maji hayawezi kupungua na kuleta athari kwenye gati na kuwataka wakazi wa Nyamisati kuwa na subira kusubiri utekelezaji wa mradi huo.

Kwa wake Mbunge wa Kibiti, Ally Ungando aliomba TPA kuongeza kasi katika ujenzi wa gati hilo kwa kuwa wananchi wamekuwa wakilisubiri kwa muda mrefu ili kurahisisha huduma za usafiri ambao wameukosa kwa siku nyingi.

Na Zuena Msuya