Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amekutana na Mawaziri mbalimbali akiwemo Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, January Makamba, Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu na Makatibu wakuu kutoka wizara mbalimbali ili kujadili maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa kufua umeme wa mto Rufiji.

Waziri wa Nishati, Dkt. Merdard Kalemani akizungumza katika kikao cha Mawaziri na Makatibu Wakuu wa Wizara mbalimbali zinazoshiriki katika utekelezaji wa ujenzi wa Mradi wa Uzalishaji umeme wa maji wa Rufiji mkoani Morogoro. Kutoka kulia ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maeendeleo ya Makazi, William Lukuvi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, January Makamba na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Ujenzi, Mhandisi Josaeph Nyamhanga akimwakilisha Waziri wa Wizara hiyo.

Akielezea madhumuni ya mkutano huo, Dkt. Kalemani alisema ni kujadili hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa masuala mbalimbali yatakayopelekea katika kuanza utekelezaji wa mradi Kuzalisha umeme wa Rufiji wa Mw 2100 kwa wakati.

Aliongeza kuwa, “Wizara imejipanga kutekeleza mradi huu kwa hatua mbalimbali ikiwemo ujenzi wa mazingira wezeshi katika kuutekeleza mradi huu ili Mkandarasi atakayepatikana aweze kuukamilisha mradi huo kwa muda mfupi”, alisema Waziri Kalemani.

Aidha, Dkt. Kalemani alisema jambo jingine lililowakutanisha wajumbe hao ni kupeana taarifa kwa kila mmoja kwa hatua aliyofikia, kujadili changamoto anazokutana nazo, kutembelea eneo la ujenzi ili kuwa na uelewa wa pamoja, kubuni mkakati wa pamoja na kutatua changamoto zinazoukabili mradi huo kwa pamoja ili kuwezesha kuupeleka mradi kwa kasi na kutimiza azma ya Serikali katika kukamilisha mradi kwa wakati.

Akizungumzia faida za Mradi wa Umeme wa Mto Rufiji Dkt. Kalemani alisema utaongeza upatikanaji wa Umeme nchini ambapo kiasi cha MW 2100 zitazalishwa na kuingizwa kwenye gridi ya Taifa.

Akizungumzia kiasi cha umeme kinachozalishwa kwa sasa kutoka katika vyanzo mbalimbali nchini alisema ni MW 1582 ziada ya umeme ni MW 200 -250 na kwamba kiasi hicho hakitoshelezi katika kupelekea uchumi wa viwanda nchini.

Dkt. Kalemani alibainisha kuwa taratibu za upatikanaji wa Mkandaarasi zinaendelea na wapo katika hatua za mwisho za upatikanaji wa Mkandarasi, na hivyo mradi haurudi nyuma, hautachelewa wala kucheleweshwa.

“tutachukua hatua kali sana kwa yeyote atakayechelewesha mradi huu,” alionya Waziri Kalemani.

Waziri Kalemani alielezea kanuni anazozitumia katika utendaji wake ikiwa ni Wepesi, Usahihi na Nidhamu na kuhaidi kuwa atahakikishia watanzania kwa ujumla wanafaidika na  mradi huu na kusema kuwa mradi huu utakamilika kwa wakati na wananchi watapata umeme wa kutosha.

Katibu Mkuu wa Nishati, Dkt. Hamisi Mnyimvua akiwakaribisha wadau mbalimbali (hawapo pichani) kwenye Mkutano wa Mawaziri wa kujadili maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa kufua umeme wa mto Rufiji ulifanyika tarehe 1 Agosti, 2018 Morogoro.

Kwa Upande wake, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, alisema kuwa, anamshukuru Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani kwa kuwashirikisha mawaziri wanaohusika na mradi huu kwa namna moja au nyingine na akatoa wito kwa Waziri Kalemani kuwashirikisha Mawaziri wote kwa ukamilifu ili wauelewe mradi huu kwa kina na waweze kutekeleza Azma ya Serikali kikamilifu.

Pia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, January Makamba alisema kuwa, atashirikiana na Mawaziri wote katika kuutekeleza mradi huu na kuhakikisha kuwa azma ya serikali ya viwanda nchini inatekelezeka.

Mkutano wa aina hii ni wa pili kufanyika ambapo mkutano wa kwanza ulifanyika mwezi Januari, 2018 na huu wa pili umefanyika tarehe 1 mwezi Agosti, 2018 katika ukumbi wa Umwema JKT uliopo mjini Morogoro.

Na Rhoda James- Morogoro