Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amezindua huduma ya upatikanaji umeme wa Gridi ya Taifa katika Wilaya ya  Muleba,   mkoani Kagera,  na  kuifanya Wilaya  hiyo kuacha kutumia umeme kutoka nchini Uganda.

Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani akizindua huduma ya upatikanaji umeme katika Kijiji cha Nundu wilayani Muleba.

Uzinduzi umefanyika tarehe  29 Julai, 2018  katika  Kijiji cha Nyakabango, Kitongoji cha Nyamagojo wilayani Muleba na kuhudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Mhandisi Richard Ruyango ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kagera,  watendaji wa Wizara ya Nishati, Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO)  na viongozi wa Kijiji na Kitongoji.

Dkt. Kalemani alisema kuwa, umeme wa Gridi utawazesha wananchi katika Wilaya Muleba kupata umeme wa uhakika, unaotabirika,  nchi itapunguza utegemezi katika upatikanaji wa nishati, pia kutakuwa na urahisi wa ufuatiliaji endapo kutajitokeza changamoto ya upatikanaji umeme.

Alisema kuwa, unganishaji wa Wilaya ya Muleba na Gridi ya Taifa unahusisha ujenzi wa line ya kV 33 yenye urefu wa kilomita 24 kutokea wilayani Chato ambapo  Wilaya za Ngara na Biharamulo nazo zitafaidika na umeme huo wa Gridi kwa kupata umeme kupitia wilaya ya Chato.

“ Nimshukuru sana Rais,  Dkt.  John Pombe Magufuli kwa kutoa fedha za kutekeleza kazi hii kwani  gharama zilizotumika kwa kazi husika ni shilingi milioni 778 ambazo zimetolewa na Serikali ya Tanzania kwa asilimia 100,” alisema Dkt. Kalemani.

Aliongeza kuwa, agizo la kuunganisha Wilaya hiyo na Gridi  alilitoa  tarehe 2 Juni, 2018 kwa  kuwaagiza TANESCO kukamilisha kazi ndani ya miezi miwili hivyo aliwapongeza  TANESCO na mafundi kwa kukamilisha kazi hiyo kabla ya muda uliopangwa.

Aidha,  alitoa agizo kwa TANESCO kuhakikisha kuwa,  vijana waliofanya kazi ya kujenga miundombinu ya usafirishaji umeme huo,  wapewe mafunzo ya miezi miwili na TANESCO ili kuwajengea uwezo na kufanya kazi kisasa.

Kuhusu usambazaji  umeme vijijini alisema kuwa,  kazi hiyo  ifanyike kwa kasi kwa kuwa maeneo mengi ya Mkoa wa Kagera sasa yanapata umeme wa Gridi ambao unatabirika na hivyo kuwezesha wananchi pia kuanzisha viwanda.

Alisema kuwa, kati ya Vijiji 663 mkoani Kagera, vijiji 413 tayari  vimeunganishwa na huduma ya umeme na kazi ya usambazaji bado inaendelea kupitia Mradi wa REA III ( mzunguko wa kwanza) utakaokamilika Juni 2019.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, akizindua huduma ya upatikanaji umeme katika Kijiji cha Nyamagojo wilayani Muleba.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Muleba  alisema kuwa,  Wilaya ya Muleba imeshatenga maeneo kwa ajili ya ujenzi wa Viwanda hivyo umeme huo utawezesha azma ya Serikali ya kuwa na Viwanda vya kutosha.

Alisema kuwa,  Wananchi sasa wataweza kuanzisha biashara na kufanya ufundi wa aina mbalimbali unaotegemea uwepo wa nishati ya umeme.

Mbali na kuwasha umeme wa Gridi ya Taifa wilayani Muleba, Waziri wa Nishati pia alizindua huduma ya upatikanaji wa umeme katika Vijiji vya Nyamagojo na Nundu.

Na Teresia Mhagama, Kagera