Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amewasha umeme katika kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Gongolamboto chenye uwezo wa MVA 65 na hivyo kuimarisha upatikanaji wa umeme katika baadhi ya maeneo jijini Dar es Salaam.

Akizungumza jijini Dar s Salaam, Mgalu alisema Kituo hicho kinapokea umeme kutoka katika mitambo ya kuzalisha umeme ya Kinyerezi katika line ya 132 kV.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, (wa pili kushoto) akipata maelezo ya uendeshaji wa kituo cha Gongolamboto , kutoka kwa Naibu Mkurugenzi Mtendaji Uwekezaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi Khalid James,(mbele) wakati akikagua mitambo ya kituo hicho kabla ya kuwasha kwa mtambo huo.kushoto ni Kaimu Meneja Miradi , Mhandisi Emmanuel Manirabona.

Mgalu alifafanua kuwa kukamilika kwa kituo hicho kumewezesha uboreshaji wa upatikanaji wa umeme katika maeneo ya Kurasini, Kipawa, Kitunda, Chanika na Kisarawe, Ubungo, Mbagala na GongolaMboto.

“Kwa sasa hali ya kukatika kwa umeme mara kwa mara katika maeneo yaliyokuwa yakisambaziwa umeme kutoka katika kituo hiki haitakuwepo tena, hivyo Serikali itaendelea na juhudi kuwasha umeme katika vituo vingine vilivyosalia,” alisisitiza Mgalu.

Kituo cha Gongolamboto ni miongoni mwa vituo 19 vya kupoza na kusambaza umeme nchini vilivyo katika mradi wa uboreshaji wa vituo hivyo unaofadhiliwa na TEDAP  ambapo Jiji la Dar es salaam lina vituo 11,  Arusha vituo Sita (6) na Kilimanjaro vituo viwili (2).

Na Zuena Msuya, Dar es Salaam