• Wajadili miradi ya nishati inayofadhiliwa na Sweden

Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu amekutana na Balozi wa Sweden nchini, Katarina Rangnitt na kujadili miradi mbalimbali ya nishati inayofadhiliwa na Sweden.

Kamishna wa Nishati, Mhandisi Innocent Luoga (wa kwanza kushoto), akifafanua jambo wakati wa kikao cha Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu (wa kwanza kulia) na Balozi wa Sweden nchini, Katarina Rangnitt (wa pili kutoka kulia). Kikao hicho kilifanyika Juni 12, 2018 Makao Makuu ya Wizara jijini Dodoma. Wengine pichani ni Afisa kutoka Ubalozi wa Sweden nchini, Jargen Eriksson (katikati) na Mkurugenzi wa Masuala ya Kiufundi kutoka Wakala wa Nishati Tanzania (REA), Mhandisi Bengiel Msofe.

Katika mazungumzo yao yaliyofanyika jana, Juni 12, 2018 Makao Makuu ya Wizara Dodoma, Balozi Rangnitt alisema kuwa nchi yake bado ina nia ya kuendelea kufadhili miradi ya kupeleka umeme vijijini inayotekelezwa sehemu mbalimbali nchini.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Mgalu alimhakikishia Balozi huyo kuwa, Serikali ya Tanzania itaendelea kutoa ushirikiano kwa Sweden katika kuhakikisha miradi husika inatekelezwa kama ilivyopangwa.

Aidha, Naibu Waziri aliuagiza uongozi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kupitia mapendekezo ya kuongeza uzalishaji wa umeme nchini kwa kutumia gesi na kupitia ufadhili wa Benki ya Sweden, yaliyowasilishwa na Kampuni za Siemens na EKN, ambazo viongozi wake waliambatana na Balozi.

“Nawaagiza TANESCO kupitia mapendekezo yaliyowasilishwa ili tuone namna bora ya kuitekeleza miradi husika.”

Miradi ya nishati nchini inayofadhiliwa na Sweden ni pamoja na Mradi wa kupeleka umeme vijijini (REA) pamoja na miradi mbalimbali ya kuzalisha umeme inayotekelezwa kupitia TANESCO.

Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Wakurugenzi kutoka REA na TANESCO pamoja na baadhi ya maafisa waandamizi kutoka Wizara ya Nishati.

Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu (katikati) akiongoza kikao na Ujumbe kutoka Sweden (kushoto), ulioongozwa na Balozi wake hapa nchini, Katarina Rangnitt. Kikao hicho kilifanyika Juni 12, 2018 Makao Makuu ya Wizara jijini Dodoma. Kulia ni Wakurugenzi kutoka REA na TANESCO pamoja na baadhi ya maafisa waandamizi kutoka Wizara ya Nishati.

Na Veronica Simba – Dodoma