Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu amefanya ziara katika Wilaya ya Kigamboni, mkoani Dar es Salaam na kuwaelezea wananchi wa eneo hilo watakavyonufaika na Mradi mpya wa umeme unaoitwa Peri-Urban.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (mbele-katikati) akiwa ameambatana na viongozi mbalimbali wa Serikali wilayani Kigamboni na maafisa kutoka wizarani, TANESCO na REA; wakati wa ziara yake wilayani humo Julai 3, 2018 kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme pamoja na kuzungumza na wananchi.

Alifanya ziara hiyo jana, Julai 3, 2018 akiwa ameambatana na maafisa mbalimbali kutoka wizarani, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Akizungumzia Mradi huo mpya; Naibu Waziri alisema kuwa Serikali imeuanzisha mahsusi kwa lengo la kupeleka umeme katika maeneo yanayokua kwa kasi.

“Kutokana na kasi ya ukuaji wa maeneo mbalimbali, ikiwemo Kigamboni, kumekuwepo na ongezeko la uhitaji wa viwanda pamoja na mahitaji mengine ya wananchi. Hivyo Serikali imeonelea vema kuanzisha Mradi huu mpya maalum kwa ajili ya maeneo hayo na utatekelezwa sambamba na miradi mingine ya umeme inayoendelea.”

Akifafanua zaidi, alisema kuwa, Mradi huo mpya utazinduliwa hivi karibuni ambapo kazi ya kusambaza umeme itaanza kutekelezwa mwezi Agosti mwaka huu.

“Kinachoendelea kwa sasa ni mchakato wa kufanya tathmini. Mpaka mwishoni mwa mwezi Julai mwaka huu, tutakuwa tumeshamteua Mkandarasi wa kutekeleza miradi hiyo,” alisema.

Naibu Waziri aliwataka wananchi kujiandaa ipasavyo ili Mradi utakapoanza kutekelezwa katika maeneo yao, waweze kuunganishiwa.

Aidha, aliwaasa kuwa makini na matapeli wanaojinadi kufanya kazi TANESCO na kuwatoza malipo zaidi ya yale yaliyoainishwa na Serikali.

Awali, akitoa taarifa ya hali ya umeme katika eneo la Kigamboni, kwa Naibu Waziri, Meneja husika wa TANESCO, Mhandisi Hadija AbdalaHemed, alibainisha kuwa, katika kipindi cha mwaka huu wa bajeti, Shirika hilo linatarajia kutekeleza miradi 23 ya kusambaza umeme katika Wilaya ya Kigamboni. Aidha, alisema kuwa, jumla ya vijiji 35 vitapatiwa umeme kupitia Mradi wa Peri-Urban.

Baadhi ya wananchi wa maeneo mbalimbali ya Kigamboni, wakiuliza maswali na kutoa maoni kwa Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (hayupo pichani), wakati wa ziara yake kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme wilayani humo, Julai 3, 2018.

Mradi huo wa kusambaza umeme wa Peri-Urban unatekelezwa katika Mkoa wote wa Pwani pamoja na baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Dar es Salaam, ikiwemo Kigamboni.

Katika ziara yake Kigamboni, Naibu Waziri alitembelea na kukagua maendeleo ya Kituo cha kupooza umeme cha Dege, kutembelea na kuzungumza na wananchi wa Mtaa wa Minondo, Gorani, Mwasonga pamoja na Mtaa wa Pemba Mnazi.

Na Veronica Simba – Dar es Salaam