Wakandarasi waliopewa jukumu la kutekeleza Miradi ya Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA III) Nchini, wametakiwa kuhakikisha wanatekeleza kwa mujibu wa mikataba na kwamba Serikali haitomvumilia Mkandarasi atakayekwenda kinyume.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu ametoa agizo hilo Januari 5, 2018 katika Kijiji cha Utengule, Mbeya Vijijini kwenye ziara yake ya kukagua utekelezaji wa Mradi wa Nishati Vijijini (REA) Mkoani Mbeya.

Mgalu alisema kumekuwepo na aina ya uzembe kwenye utekelezaji wa Mradi wa REA Awamu ya Pili kwenye baadhi ya maeneo uliosababishwa na baadhi ya Wakandarasi jambo ambalo alilikemea na kuagiza lisijirudie tena kwenye utekelezaji wa miradi ya Awamu ya Tatu.

“Wakandarasi mnaotekeleza mradi wa REA III; anayeona hawezi kazi atupishe; hatutomvumilia Mkandarasi anayeharibu kazi,” alionya Naibu Waziri Mgalu.

Aliongeza kuwa utekelezaji wa Mradi wa REA II ulikuwa na mapungufu ikiwemo ya kuruka baadhi ya maeneo jambo ambalo alisema halitojirudia kwenye utekelezaji wa Awamu ya Tatu ya mradi huo.

“REA II ilikuwa na mapungufu ya kuruka baadhi ya maeneo, tena muhimu; hili nawahakikishia halitojirudia tena, Wanambeya msiwe na mashaka,” alisema Mgalu.

Aidha, aliwaasa wananchi kuchangamkia fursa ya kuunganishiwa huduma ya umeme ili kujiletea maendeleo na alisisitiza kuwa gharama ya kuunganishiwa umeme kupitia Mradi wa Umeme Vijijini ni Shilingi 27,000 ambayo alisema hakuna mwanachi atakayeshindwa kumudu.

Alisema dhamira ya Serikali ni kuhakikisha Mradi wa Umeme Vijijini unakamilika kwa kiwango kinachokubalika na kwa wakati kama inavyoelekezwa kwenye mikataba waliyoingia na Serikali.

Vilevile aliliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuacha kufanya kazi kwa mazoea na kuhakikisha linatoa taarifa kwa wananchi kama kutakuwa na ukataji wa umeme.

Na Mohamed Saif