• Mkandarasi atakiwa kuwasha umeme kijiji cha Mdunku kabla ya Eid al-Fitr

Kampuni inayojihusisha na ujenzi wa miundombinu ya umeme katika Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara kupitia Wakala wa Nishati Vijijini Awamu ya Tatu (REA III) ya Angelique International Limited imetakiwa kuhakikisha inakamilisha kazi yake na kuhakikisha umeme unawaka katika kijiji cha Mdunku kilichopo  wilayani Kiteto mkoani Manyara kabla ya sikukuu ya Eid al-Fitr inayotarajiwa kusheherekewa mwezi Juni.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (katikati), Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Tumaini Magessa (kushoto) Mbunge wa Kiteto, Emmanuel Papian (kulia) pamoja na wananchi wengine wakishangilia mara baada ya uzinduzi wa uwashaji wa umeme katika kijiji cha Lesoit kilichopo wilayani Kiteto mkoani Manyara.

Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu katika ziara yake ya ukaguzi wa utekelezaji  wa kazi ya usambazaji wa miundombinu ya umeme katika wilaya ya Kiteto kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) iliyoenda sambamba na uwashaji wa umeme katika kijiji cha Lesoit kilichopo wilayani humo.

Mgalu alisema wananchi wa kijiji cha Mdunku  wamekuwa wakihitaji  huduma ya  umeme kwa muda mrefu na kwa kuwa kijiji chao kipo katika orodha ya vijiji vitakavyopatiwa huduma ya umeme kupitia  REA Awamu ya Tatu, kampuni  ya Angelique International Limited inatakiwa kuhakikisha inafanya kazi usiku na mchana ili wananchi waunganishiwe huduma ya umeme mara moja.

Aliendelea kusema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano kupitia Wizara ya Nishati, imeweka mikakati  ya usambazaji wa umeme nchini ili kuhakikisha karibia vijiji vyote nchini vinafikiwa na huduma ya umeme kabla ya mwezi Juni, 2021.

Sambamba na mikakati ya usambazaji wa umeme vijijini kupitia REA, Mgalu alitaja mikakati mingine ya muda mrefu kuwa ni pamoja na ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko ya maji ya mto Rufiji wa Stieglers Gorge ambapo mara baada ya kukamilika kwake utakuwa na uwezo wa kuzalisha Megawati 2100 na kuondoa kabisa changamoto ya upungufu wa umeme nchini.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Mgalu alimtaka mkandarasi kutoa ajira kwa vijana wa wilaya ya Kiteto hususan katika kazi zisizohitaji utaalam badala ya kutoa ajira kwa vijana walio mbali na wilaya ya Kiteto.

Aidha, alimtaka mkandarasi kuhakikisha kuwa taasisi zote zinazotoa huduma za jamii kama vile shule, vituo vya afya na zahanati zinaunganishiwa na huduma  ya umeme  wakati wote wa utekelezaji wa mradi.

Wakati huohuo, Naibu Waziri Mgalu aliwataka wananchi kuchangamkia huduma ya umeme kwa kuchukua fomu zinazotolewa bure na  kulipia shilingi 27,000 tu ili kuunganishiwa na huduma ya umeme.

Aliwataka wananchi kuepuka vishoka na matapeli wanaopita kwenye nyumba za watu na kujifanya ni wafanyakazi wa REA na kuwatoza fedha na kuwataka kutoa taarifa kwenye vyombo vya usalama ili wachukuliwe hatua kali za kisheria.

“Ninaelekeza akitokea mtu yeyote ambaye ni tapeli anayepita katika nyumba za watu na kutoza gharama bila kufahamika mtoe taarifa katika vyombo vya ulinzi na usalama ili hatua kali za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yake,” alisisitiza Mgalu.

Sehemu ya wananchi wa kijiji cha Lesoit kilichopo wilayani Kiteto mkoani Manyara wakisikiliza hotuba ya uzinduzi iliyokuwa inatolewa na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (hayupo pichani) kwenye uzinduzi huo.

Akizungumza na wananchi wa katika kijiji cha Lesoit kilichopo wilayani Kiteto mkoani Manyara mara baada ya kuwasha umeme katika kijiji hicho, Mgalu aliwataka kujiandaa na huduma ya umeme kwa kutandaza mfumo wa umeme (wiring)

Alieleza kuwa, kwa wananchi wenye nyumba ndogo hawana haja ya kutandaza mfumo wa umeme badala yake watumie kifaa maalum kijulikanacho kama UMETA yaani Umeme Tayari kinachopatikana kwa gharama ya shilingi 36,000 kuunganishiwa na huduma ya  umeme hapo hapo.

Alilitaka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuhakikisha linakagua vifaa vya mkandarasi mapema iwezekanavyo ili kazi ya ujenzi wa miundombinu ya umeme katika vijiji vilivyobaki iweze kuanza na kukamilika kwa wakati.

Na Greyson Mwase, Manyara