Na Veronica Simba – Bahi

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, ametoa wito kwa wananchi kulinda miundombinu ya umeme ili isihujumiwe hivyo kurudisha nyuma jitihada za Serikali katika kuhakikisha Tanzania nzima inakuwa na umeme wa uhakika.

Aliyasema hayo jana, Novemba 1, 2017 akiwa katika ziara ya kazi kijijini Kigwe, Wilaya ya Bahi, Mkoa wa Dodoma.

“Naomba mlinde miundombinu ya umeme kwani gharama zake ni kubwa sana. Msichome moto wala kuiharibu kwa namna yoyote ile, kwa kuwa uhujumu wake siyo tu utarudisha nyuma jitihada za Serikali za kuhakikisha wananchi wote wanapata nishati hii muhimu bali pia ninyi wenyewe mtapata hasara kwa kuukosa umeme.”

Aidha, aliwahakikishia wananchi wa Kigwe kuwa watapata umeme ndani ya mwezi huu wa Novemba kwani, Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kwa dhati na imejipanga kuwaletea wananchi wake maendeleo.

“Hakuna kitakachotukwamisha kwani pesa zipo za kutosha na zimeshatengwa maalum kwa ajili ya kazi hii ya usambazaji umeme.”

Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Elizabeth Kitundu (katikati), akizungumza wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (kushoto), katika Kijiji cha Kigwe wilayani Bahi, kukagua maendeleo ya Mradi wa kusambaza umeme.

Alimtaka Mkandarasi anayetekeleza Mradi huo wa kusambaza umeme katika Wilaya ya Bahi ikiwemo Kijiji cha Kigwe kuhakikisha anatimiza ahadi aliyoitoa mbele yake kuwa umeme utawaka eneo hilo ndani ya mwezi huu wa Novemba.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Elizabeth Kitundu, alitoa pongezi kwa Serikali kutokana na jitihada inazofanya katika kuwaletea wananchi wake maendeleo.

Kwa niaba ya wananchi wake, Mkuu wa Wilaya aliahidi kutoa ushirikiano kwa Mkandarasi husika ili aweze kukamilisha kazi yake kwa ufanisi na ndani ya wakati kama ilivyopangwa.

Naye Mbunge wa Bahi, Omary Baduel, pamoja na kutoa pongezi kwa Serikali kutokana na jitihada zake za kuwapelekea wananchi umeme, aliomba maeneo muhimu ya huduma za kijamii kama vile Hospitali na Shule yapewe kipaumbele wakati wa zoezi la kuunganisha umeme.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa ziara hiyo, mbele ya Naibu Waziri, Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Dodoma, Zakayo Temu na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga, waliwahakikishia wananchi kuwa maeneo ya huduma za kijamii yatapewa kipaumbele katika kuunganishiwa umeme.

Aidha, waliwataka wananchi kufanya maandalizi yote muhimu katika makazi yao na majengo ya biashara ili waweze kuunganishiwa umeme wakati utakapofika katika maeneo yao.