Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amwataka wazalishaji umeme wa sekta binafsi kuangalia namna ya kupunguza tozo za kuunganisha na kununua umeme, ili kumfikishia mwananchi wa kijijini kwa gharama nafuu.

Mgalu ametoa rai hiyo jana, Novemba 26, alipotembelea kampuni ya kuzalisha umeme ya Mwenga inayotoa huduma ya umeme Mufindi Kaskazini wilayani Mufindi mkoani Iringa.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akicheza na wananchi wa kijiji cha Ikondosi wilayani Mufindi akiwa katika ziara ya kazi kukagua miradi ya umeme.

Alisema Serikali ililazimika kufanya marekebisho ya sheria mbalimbali ili kuruhusu sekta binafsi kuzalisha na kusambaza umeme kwa nia ya kufanya maeneo mengi yapate huduma ya umeme.

“Ili kufikia lengo hilo, Serikali ilitoa ruzuku kwa baadhi ya kampuni binafsi ikiwa ni kuweka mazingira wezeshi ya kusaidia katika uzalishaji wa umeme.

“Mpaka sasa bado Serikali imeendelea kuweka mazingira na kushirikiana na wadau wa sekta binafsi wanaozalisha umeme kwa kutumia njia mbalimbali za umeme jua, upepo, makaa ya mawe, lengo likiwa ni kuzalisha umeme kwa wingi na uwafikie watu wengi, wakati wote na kwa gharama nafuu.

Alisema Serikali inapokuwa inatoa takwimu za vijiji vilivyofikiwa na umeme kwa njia moja au nyingine inahusisha pia vile vya wawekezaji binafsi.

”Ndiyo maana katika siku za hivi karibuni tulikutana na wazalishaji umeme chini ya megawati 10 husani wale waliopata ruzuku kupitia upelekaji wa nishati vijijini, na kushauriana nao kuhusiana na tozo, hasa baada ya kupokea malalamiko ya kuwapo gharama kubwa za kuunganisha na kulipia umeme.

“Kwa sasa Serikali ina viwango maalumu vya kuunganisha wateja ikiwa ni Sh 27,000 kwa kuunganisha, na tukawaomba walifanyie kazi ili gharama hizo zisiwe kubwa hivyo kumuumiza mwananchi wa kijijini.

Alisema ili hilo lifanikiwe, tayari Wizara yake imeiagiza Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati, Maji na Mafuta (EWURA) kufanya mapitio ya tozo za sekta binafsi katika kuunganisha na kuuza umeme ili kutimiza lengo la Serikali la kuwafikia wananchi wengi na kwa gharama nafuu.

Alisema kwa sasa umeme unaozalishwa nchini ni takribani megawati 1,600 na kuwa taarifa za hivi karibuni za matumizi ya juu ya nchi ni megawati 1,092 hivyo kufanya kuwa na ziada ya megawati zaidi ya 200 hivi.

“Ziada hii ni ndogo kwa wananchi wote walioomba na viwanda vinavyojengwa, hivyo kama Serikali tuna jukumu la kuondoa pengo lililopo kati ya mahitaji, uzalishaji na matumizi.”

“Ndiyo maana nawapongeza ninyi Mwenga kwa kushiriki kikamilifu katika kupunguza pengo hilo kwa kuanzisha miradi mingine ya kuzalisha umeme ikiwamo ule wa upepo.

Alisema kwa sasa wastani wa asilimia 50 ya megawati zinazozalishwa zinatokana na umeme unaozalishwa kwa gesi na kuongeza kuwa uchumi wa viwanda unahitaji umeme wa uhakika unaotegemea vyanzo mbalimbali vya uzalishaji umeme.

Aliipongeza kampuni hiyo ya Mwenga ambayo ni kampuni tanzu ya Rift Valley kwa kuweza kuviunganishia vijiji 32 huku ikiwa na wateja takribani 3,000.

Akizungumzia suala la utunzaji mazingira, Mgalu amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Mufindi na Kamati ya Ulinzi ya Wilaya hiyo kutokuwa na huruma kwa waharibifu wa mazingira.

“Mkuu wa Wilaya (Jamhuri William) na Kamati ya Ulinzi mmesikia taarifa ya Mwenga ya kuwapo matumizi ya shughuli za kibinadamu ambayo yanaharibu vyanzo vya maji, zuieni hili na msiwe na huruma na waharibifu na muwaondoe maeneo hayo. Pia shirikisheni vijiji 32 vinavyonufaika na uwekezaji huu wa umeme kuhakikisha wanalinda na kuzuia uharibifu wa mto Mwenga ili shughuli za uzalishaji wa umeme ziweze kufanyika kama ilivyokusudiwa.”

Pia, aliitaka Kampuni ya Mwenga kuhakikisha inatumia fungu za jamii katika kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na uharibifu wa mazingira na ikiwezekana kuanzisha shughuli mbadala.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akikagua kituo binafsi cha kuzalisha umeme cha Mwenga ambacho kinazalisha megawati 4 na kuunganishwa katika vijiji 32 vya Wilaya ya Mufindi.

Awali, Meneja wa Kampuni ya uzalishaji Umeme ya Mwenga, Joel Gomba alisema kwa sasa Mradi umekuwa ukikabiliwa na upungufu wa kina cha maji cha Mto Mwenga ambao wanautumia kuzalisha nishati hiyo ambayo imetokana na shughuli za kibinadamu.

Alisema kutokana na hali hiyo, kampuni yake ambayo kwa sasa inazalisha megawati 4 imechukua hatua ya kuanzisha Mradi wa kuzalisha umeme kwa njia ya upepo ili kuondoa upungufu wa umeme nyakati za kiangazi, na kuwa umeme huo utaanza kuzalishwa mwakani.

Pia aliishukuru Serikali kwa kuunga mkono kazi zinazofanywa na kampuni yake na kusisitiza kuwa Serikali imekuwa ikiwaunga mkono hata kwa fedha ili kufikia dhana ya kuzalisha umeme.

windows 8.1 pro kaufen