Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, amefanya ziara katika Kituo cha kupoza na kusambaza umeme kilichopo eneo la Zuzu mjini Dodoma, leo Oktoba 28, 2017.

Akiwa amefuatana na Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Dodoma, Zakayo Temu, Naibu Waziri Mgalu, ametembelea Kituo hicho ili kujionea utendaji kazi wake.

Akitoa malelezo kwa Naibu Waziri, Kaimu Mkuu wa Kituo hicho, Bosco Mgina amesema kuwa, Kituo hupokea msongo wa umeme wa kilivolti 220 katika njia tatu ambazo ni Mtera, Iringa One na Iringa Two.

Aidha, ameongeza kuwa, Kituo kina transfoma mbili za kupoza umeme ambapo kila moja ina uwezo wa kutoa megawati 24 za umeme hivyo kufanya jumla yake kuwa megawati 48.

Akizungumzia hali ya upatikanaji wa umeme kwa Mkoa wa Dodoma, Meneja Temu ameeleza kuwa kwa sasa huduma ya nishati hiyo muhimu imerejea katika maeneo yote baada ya jitihada za Shirika hilo katika kutatua matatizo yaliyojitokeza hivi karibuni.

Akihitimisha ziara yake katika Kituo hicho, Naibu Waziri Mgalu amewasisitiza viongozi wa TANESCO kuhakikisha huduma ya umeme wa uhakika inaendelea kutolewa kwa wateja katika maeneo yote.