Na Asteria Muhozya, DSM

Meneja wa TANESCO Mkoa wa TEMEKE, Mhandisi Jahulula Jahulula (aliyenyoosha mkono) akimweleza jambo Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu. Wengine ni Wataalam kutoka TANESCO na Wizara ya Nishati.

Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu ametembelea Miradi ya Umeme inayotekelezwa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) katika maeneo tofauti eneo la Mbagala jijini Dar es Salaam na kueleza kuwa ameridhishwa na utekelezaji wa miradi hiyo.

Naibu Waziri ameyasema hayo leo tarehe 5 Oktoba, 2017, alipotembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa na shirika hilo eneo la Mbagala, ikiwemo uwekaji wa line mpya, na ufungaji wa Transfoma.

Aidha, ameitaka TANESCO kubuni njia zitakazowezesha kuwaunganisha wananchi na nishati ya umeme kutokana na mahitaji ya nishati hiyo kuwa kubwa katika eneo la Mbagala na maeneo mbalimbali nchini.

“Kadri miradi inavyotekelezwa ni vema wakafanya  makisio kuendana na uongezeko la wateja lakini wazingatie  ubunifu. Mfano zipo nyumba ambazo zimejengwa baada ya mradi kutekelezwa. Ni vema TANESCO ikajipanga kuona namna ya kuwahudumia wateja wapya,”amesisitiza Naibu Waziri.

Pia, Naibu Waziri amewataka wananchi ambao bado hawajafikiwa na huduma hiyo, kuanza kujipanga ili pindi miundombinu ya umeme inapofika katika maeneo yao waweze kuunganishwa na nishati hiyo.

Aidha, Mgalu ameeleza kuridhishwa na namna shirika hilo linavyotumia mapato yake kutelekeza miradi mbalimbali, lengo likiwa ni kuhakikisha kwamba, wananchi wanaunganishwa na nishati hiyo.

Miradi hiyo ya ujenzi wa njia za umeme za msongo wa kilovolti 11 kila eneo, inatekelezwa katika maeneo tofauti ya Chamazi Dovya 1- 3, Mbande kwa Masista 1-3, kwa Mzala na Chamazi Vigoa.