Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, ameendelea na ziara  ya ukaguzi wa miradi ya umeme mkoani Ruvuma ambapo leo amewasha umeme Kijiji cha Palangu na Mang’ua pamoja mtaa wa Luhila Seko katika Wilaya ya Songea ambavyo vimepata umeme kupitia mradi wa usambazaji umeme vijijini wa Awamu ya Tatu (REA III) mzunguko wa kwanza na mradi wa Makambako – Songea.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (wa pili kulia) akikagua mitambo ya umeme katika kituo cha kupoza umeme cha Songea ambacho kimejengwa kupitia mradi wa umeme wa Makambako-Songea na kimeanza kusambaza umeme wa gridi kuanzia mwezi wa Tisa mwaka huu.

Huo ni muendelezo wa kazi ya ukaguzi na uzinduzi wa miradi ya umeme vijijini mkoani Ruvuma aliyoianza tarehe17 Disemba, 2018 kwa kuwasha umeme katika Vijiji Saba vilivyopo katika Wilaya ya Tunduru na Namtumbo ambapo wateja zaidi ya 200 wameunganishwa na huduma ya umeme.

Aidha, kuunganishwa kwa umeme katika Vijiji Palangu, Mang’ua pamoja na Mtaa wa Luhila Seko, wilayani Songea kumewezesha wateja zaidi ya 230 kuunganishwa na huduma hiyo huku wengine wakitumia umeme huo kwa shughuli za kiuchumi kama kusaga na kukoboa nafaka.

Pamoja na kuwasha umeme katika Vijiji hivyo, Naibu Waziri alikagua kazi ya usambazaji umeme katika Vijiji vya Liula, Mpangula na Litapwasi na kumsisitiza mkandarasi, kampuni ya Namis kufanya kazi kwa kasi na umakini ili kuondoa malalamiko ya wananchi ya kucheleweshewa huduma ya umeme.

Kuhusu Mkandarasi huyo, Naibu Waziri alisema kuwa, Serikali inaangalia kasi yake katika utekelezaji wa mradi wa umeme vijijini mkoani Ruvuma na endapo atasua sua hadi kufikia mwezi ujao, atanyang’anywa kazi hiyo.

“ Serikali inatoa vipaumbele kwa wakandarasi wazawa kufanya kazi hizi za usambazaji umeme vijijini, lakini na sisi tunataka mfanye kazi kwa kasi na umakini ili kutorudisha nyuma juhudi za Serikali za kuwapelekea umeme wananchi,” alisema Mgalu.

Akiwa wilayani Songea, Naibu Waziri pia alifanya mazungumzo na  Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme ambapo walijadiliana  masuala mbalimbali kuhusu nishati ya umeme mkoani Ruvuma na baadaye alikagua  kituo cha kupoza umeme cha Songea kilichojengwa kupitia mradi wa Makambako-Songea na kinasambaza umeme wa gridi katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Ruvuma.

Moja ya nyumba zilizounganishiwa umeme katika Kijiji cha Palangu wilayani Songea, Mkoa wa Ruvuma kupitia mradi wa usambazaji umeme vijijini wa Awamu ya Tatu (REA III) mzunguko wa kwanza.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma,  alimshukuru Naibu Waziri kwa kazi anazofanya ikiwemo ukaguzi wa miradi ya umeme katika sehemu za pembezoni mwa nchi na kueleza kuwa Mkoa wa Ruvuma sasa unapata nishati ya umeme ya kutosha na uhakika mara baada ya kukamilika kwa mradi wa umeme wa Makambako- Songea.

Alisema kuwa Mkoa huo unapata umeme wa kiasi cha megawati 139, hata hivyo nyakati za mchana kiasi cha umeme kinachotumika ni megawati 11 na usiku umeme unaotumika ni megawati 3 hivyo alitoa wito kwa wakazi wa Mkoa wa Ruvuma kuutumia umeme huo usiku na mchana kwa shughuli mbalimbali ikiwemo za maendeleo kwani umeme upo wa kutosha.

Kuhusu kiwango  hicho cha matumizi  ya umeme mkoani Ruvuma, Naibu Waziri alisema kuwa, kiwango hicho kitaendelea kuongezeka kwani  kazi ya uunganishaji  umeme kwa wananchi  inaendelea na wataitumia nishati hiyo kwa shughuli za maendeleo ambapo pia alitoa wito kwa wawekezaji  mbalimbali kuendelea kuwekeza mkoani humo.

Na Teresia Mhagama, Ruvuma.

office 2016 kaufen