Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amekagua mitambo miwili ya umeme yenye uwezo wa kuzalisha megawati 2 kila mmoja itakayofungwa katika kituo cha kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia cha Mtwara.

Watendaji kutoka Wizara ya Nishati, kampuni ya Mantrac na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wakiwa katika kikao kilichoongozwa na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu kilichofanyika jijini Dar es Salaam.

Amekagua mitambo hiyo tarehe 21 Februari, 2018 katika eneo la Mkandarasi, jijini Dar es Salaam ambapo kampuni ya Mantrac ndiyo iliyopewa kazi ya kufunga mitambo hiyo.

Baada ya kukagua mitambo hiyo, Naibu Waziri alisisitiza kuwa, Serikali inafuatilia kwa karibu utekelezaji wa  kazi  hiyo lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa  mitambo hiyo inafikishwa na kusimikwa mkoani Mtwara mapema iwezekanavyo ili kuboresha hali ya upatikanaji wa umeme katika mkoa wa Mtwara pamoja na Lindi.

Kabla ya kukagua mitambo hiyo, Naibu Waziri Mgalu alifanya kikao na watendaji wa kampuni hiyo ya Mantrac pamoja na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) lengo likiwa ni kufahamu maendeleo ya kazi hiyo.

Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa Mantrac, Ahmed Saleh alimweleza Naibu Waziri kuwa mpaka sasa mitambo hiyo tayari imewasili jijini Dar es Salaam na kinachosubiriwa kwa sasa ni kuwasili kwa kontena maalum zitakazotumika kuwekea mitambo hiyo kabla ya kusafirishwa kuelekea mkoani Mtwara.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Khalid James akimpa taarifa Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu kuhusu utekelezaji wa kazi ya ufungaji wa mitambo mipya ya umeme katika kituo cha Mtwara. Kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya TANESCO, Dkt. Alexander Kyaruzi.

Aliongeza kuwa, kazi ya usafirishaji wa mitambo hiyo kwenda mkoani Mtwara itafanyika mwanzoni mwa mwezi Aprili mwaka huu na kwamba kazi ya kufunga mitambo hiyo, majaribio na makabidhiano itafanyika tarehe 9 hadi 30 mwezi Aprili mwaka huu.

Kituo cha kuzalisha umeme kwa Gesi asilia mkoani Mtwara kina mitambo Tisa yenye uwezo wa kuzalisha megawati 2 kila mmoja. Kituo kwa sasa kinazalisha umeme wa kiasi cha megawati 16 kufuatia mtambo namba Tisa kuwa nje kwa matengenezo.

Kuongezeka kwa mashine hizo mbili mpya (4 MW) kutafanya uwezo wa kituo hicho kuongezeka na kufikia megawati 22 na hivyo kuboresha hali ya upatikanaji wa umeme katika mikoa ya Lindi na Mtwara.

Na Teresia Mhagama