Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, amekataa kuzindua huduma ya umeme katika Kata ya Kirando na Kate wilayani Nkasi mkoa wa Rukwa, baada ya Mkandarasi kusuasua kuunganishia umeme wananchi.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (wa pili kushoto) akikagua miundombinu ya umeme katika Gereza la Kilimo-Mollo lililopo wilayani Sumbawanga kabla ya kuzindua huduma ya umeme katika Gereza hilo. Kushoto kwa Naibu Waziri ni Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Dkt. Halfan Haule na wa kwanza kushoto ni Mkuu Gereza hilo, Jailos Mwamgunda.

Naibu Waziri alitoa uamuzi huo, baada ya kukagua miundombinu ya usambazaji umeme katika Kata hizo na kuelezwa kuwa, katika Kata ya Kirando ni wananchi wanne tu ndio wameunganishiwa umeme na katika Kata ya Kate, ni wananchi wawili tu wameunganishwa.

Naibu Waziri alieleza kusikitishwa kwake na kasi ndogo ya mkandarasi huyo, kampuni ya Nakuroi, aliyepewa kazi ya kusambaza umeme katika Vijiji 111 vya Mkoa wa Rukwa  hadi kufikia Juni 2019 ambapo mpaka sasa ameunganisha umeme katika Vijiji Saba tu.

“Tangu mpewe kazi hii mwaka jana, mpaka sasa ni Vijiji Saba tu mmewasha umeme, hili suala halikubaliki, na nitakaporudi Dodoma Mkurugenzi wa Kampuni hii na Menejimenti yake wafike wizarani Dodoma kutoa maelezo, “amesema Naibu Waziri.

Alisema kuwa, pamoja na Serikali kuanza kutoa fedha kwa wakandarasi wa umeme, baadhi ya wakandarasi bado wanasuasua kutekeleza kazi hiyo kwa visingizio vya kutokuwa na vifaa.

Alitoa onyo kuwa, kama kuna mtandao wa watu wanaojipanga ili kukwamisha juhudi za Serikali za kusambaza umeme Vijijini, Serikali itawabaini na watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.

Aidha,  aliwakumbusha wananchi kuwa, miradi ya usambazaji umeme vijijini  haina fidia na kwamba wakubali kutoa maeneo yao ili kupitisha miundombinu ya umeme na kutoa angalizo kuwa, Serikali haitawavumilia wananchi wachache wanaokwamisha juhudi za Serikali za  kuleta maendeleo nchini.

Awali, Mbuge wa Nkasi Kaskazini, Ally Kessy na Mbunge wa Nkasi Kusini, Desderius Mipata nao walitoa malalamiko kwa Naibu Waziri kuhusu kampuni ya Nakuroi kuwa na kasi ndogo katika kuwasambazia umeme wananchi.

Katika ziare yake mkoani Rukwa, Naibu Waziri pia alizindua miundombinu ya usafirishaji umeme kutoka katika Kata ya Kirando hadi katika eneo lililotengwa kwa ajili ya viwanda katika Kijiji cha Isesa wilayani Nkasi, ambayo imejengwa na wataalam wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, akibonyeza kitufe kuashiria uzinduzi wa miundombinu ya kusafirisha umeme kuelekea katika eneo la Viwanda lililopo kwenye Kijiji cha Isesa wilayani Nkasi. Wa kwanza kulia ni Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Kessy.

Vilevile, Naibu Waziri, alizindua huduma ya umeme katika Gereza la Kilimo la Mollo lililopo wilayani Sumbawanga ambapo zaidi ya nyumba 30 zimeunganishwa na huduma ya umeme.

Mkuu wa Gereza hilo, Jailos Mwamgunda, alisema kuwa, Gereza lililoanzishwa mwaka 1967, lilikuwa likitumia jenereta ambalo liliharibika mwaka1999 na hivyo kufanya Gereza hilo  kukosa nishati ya umeme.

Na Mwandishi Wetu, Rukwa