Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amewaonya wakandarasi wa miradi ya umeme vijijini nchi nzima kuwa serikali itahakikisha inafanya ukaguzi maalumu na wa kina ili kubaini kama mita za Umeme Tayari (UMETA) zimetolewa kwa wananchi husani wale ambao wameshindwa kumudu gharama za kutandaza nyaya katika nyumba zao.

Aidha, amebainisha kutoridhishwa na namna Kampuni ya Sengerema inavyotekeleza miradi ya REA awamu ya tatu mzunguko wa kwanza na kuiagiza hadi ifikapo Desemba 15 kuwepo na mabadiliko ya kazi walizofanya.

Mgalu aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Uwominyi kilichopo Kata ya Image wilayani Kilolo kuhusiana na mikakati ya serikali ya kuwafikishia wananchi huduma ya umeme.

Alisema pamoja na serikali kupeleka huduma ya nishati ya umeme kwa wananchi na kutakiwa kuunginisha kwa Sh 27,000 tu, bado kuna malalamiko kwa baadhi ya wananchi kushindwa kuunganishwa na huduma hiyo kutokana na gharama kubwa za kutandaza nyaya.

“Tumebaini kuwa baadhi ya wananchi wanashindwa kuunganisha kutokana na kushindwa gharama za kutandaza nyaya kwenye nyumba ambazo ni gharama za mwenye nyumba. Lakini kila mkandarasi amepewa vifaa vya UMETA ambavyo havihitaji utandazaji wa nyaya.

“Wakandarasi wote wa umeme vijijini nawataarifu kuwa baada ya kukamilika kwa miradi yenu serikali itafanya ukaguzi wa kina wa matumizi ya mita za UMETA, maana upo ujanja ujanja miradi ikikamilika mkandarasi anabaki navyo na hususani maeneo ambako wananchi hawajaunganishwa. Tutafanya ukaguzi wa kina na hatuna masihara katika hili jambo, kwa hiyo msijisahau.

Mita za UMETA ambazo hazihitaji utandazaji wa nyaya katika nyumba inauzwa kwa Sh 36,000 na kila mkandarasai anayetekeleza usambazaji wa umeme vijijini amekabidhiwa vifaa 250.

Aidha, Mgalu aliwakumbusha wakandarasai wote nchini kuhakikisha wanatekeleza matakwa ya mikataba yao ikiwamo na maelekezo ya kila transfoma kuweka taa na kusisitiza kuwa serikali itafanya ukaguzi wa kazi hatua kwa hatua kabla ya kutoa fedha kwa hatua inayofuata.

Pia Mgalu aliitaka kampuni ya Segerema ambayo imepewa kazi katika vijiji 145 kuhakikisha inaongeza kasi ya upelekaji wa umeme na kusisitiza kuwa hawatakuwa na msamaha na kuongeza muda wa utekelezaji wa miradi hiyo.

Alipopewa nafasi ya kujieleza, msimamizi wa miradi hiyo kutoka kampuni ya Sengerema, Btyson Chengula alisema hali ya hewa na mvua zinazonyesha zimekuwa kikwazo kwa utekelezaji na kuahidi baada ya mvua hizo kupungua wataongeza kasi ya kazi.

Hata hivyo maelezo hayo hayakuonesha kukubaliwa na Naibu Waziri na wananchi ambao walipinga kauli hiyo kwa kelele wakidai barabara zinapitika.

“Umebakiwa na miezi sita, mkandarasi, vijiji hivi 44 vya Kilolo unawasha lini? Kasi ni ndogo, Sengerema jipange sababu hizi sizikubali, mkataba unataka kazi zote mlizopewa kwenda sambamba. Hivyo nawapa mpaka Desemba 15 nione mabadiliko ya miradi ya REA Awamu ya Tatu,” alisema Mgalu.

Alisema Serikali ilishatoa maelekezo kwa wakandarasi waliopewa miradi ya umeme vijijini kuhakikisha kila wiki wanawasha vijiji 3 na kuwa kasi ya mkandarasi huyo aliyepewa vijiji 145 katika wilaya kadhaa za Mkoa wa Iringa kutokuwa ya kuridhisha.

Naye Diwani wa Kata ya Image, Joseph Mhumba aliyeiomba serikali kuongeza kasi na kuhakikisha inafikisha nishati ya umeme katika vijiji na vitongoji ambavyo havijapatiwa huduma hiyo.

“Sera inasema nishati ya umeme ni kijiji kwa kijiji na kitongoji, lakini bado maeneo ambayo umeme haujafika na pia kuna kijiji ambacho hakijapelekewa umeme ambacho kinatekeleza sera ya viwanda na hili lingefanyika lingesaidia mapato kwa Wilaya ya Kilolo.”

Naye mkazi wa kijiji cha Uwominyi Getrude Mwenda alisema ameshukuru kwa kupata umeme katika kijiji chao na kuwa hali hiyo imemuongezea wigo wa kufanya biashara yake ya saluni.

“Kabla ya umeme kutufikia, kipato changu kilitegemea kazi ya kusuka tu, lakini sasa nimeongeza huduma ya kuosha na kuwatengeneza nywele wateja wangu, hivyo hata kipato kimeongezeka,” alisema.

autocad lt kaufen