Tarehe 23 Agosti 2018,  Tanzania na Uganda zilitia saini Mikataba mbalimbali ya ushirikiano ikiwa pamoja na Mkataba wa Uendelezaji wa Bomba la Kusafirisha Gesi Asilia kutoka Tanzania kwenda Uganda na mwingine ni Mkataba wa Utekelezaji wa Mradi wa Kupeleka Umeme katika Vijiji vya Mpakani mwa Tanzania na Uganda.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akishuhudia utiaji saini wa Mikataba ya Makubaliano (MoU) inayohusu utekelezaji wa Miradi ya Umeme na Gesi asilia, kati ya Tanzania na Uganda. Kulia kwake ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga.

Uwekaji saini huo ulifanyika katika Mkutano wa Pili wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Uganda uliofanyika Kampala Uganda kwa siku tatu kuanzia tarehe 21 Agosti 2018.

Miradi mingine iliyojadiliwa katika Mkutano huo ni pamoja na Mradi wa Ujenzi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi kutoka Uganda kuja Tanzania (EACOP), Mradi wa Utafutaji wa Mafuta katika Kitalu cha Eyasi Wembere, Mradi wa Ujenzi wa Kituo cha kuzalisha Umeme cha Murongo Kikagati (14MW) na Mradi wa Kituo cha kuzalisha Umeme cha Nsongezi (MW 35).

Mkutano huo pamoja na mambo mengine ulifanya tathmini ya utekelezaji wa masuala yaliyokubalika wakati wa mkutano wa kwanza wa JPC uliofanyika Arusha mwezi Aprili 2017 na kuweka mikakati ya utekelezaji kwa masuala ambayo hayajakamilika.

Aidha, ulijadili mikakati ya kuondoa vikwazo vya kibiashara kwa nchi hizo mbili.

Katika Mkutano huo ujumbe wa Wizara ya Nishati uliongozwa na Naibu Waziri, Subira Mgalu, pamoja na Maafisa Waandamizi kutoka Wizarani, TANESCO na Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC).

Watendaji mbalimbali wa Serikali za Uganda na Tanzania wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kumaliza Mkutano wa Pili wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Uganda uliofanyika Kampala Uganda kwa siku tatu kuanzia tarehe 21 Agosti 2018.