Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani ameuagiza uongozi wa juu wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuteua na kupeleka Meneja atakayesimamia Halmashauri ya Nanyamba wilayani Mtwara, ili pamoja na mambo mengine aharakishe zoezi la uunganishaji umeme kwa wananchi.

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani akizungumza na wananchi wa eneo la Namamba wilayani Mtwara, alipopita kukagua zoezi linaloendelea la uunganishaji umeme, Desemba 5, 2018.

Alitoa agizo hilo jana, Desemba 5 akiwa katika ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme pamoja na kuzungumza na wananchi.

Akizungumza na wananchi wa Mtaa wa Kilimanjaro, Waziri Kalemani alisema ukosefu wa Ofisi ya TANESCO katika eneo hilo, ni mojawapo ya sababu zinazochelewesha zoezi la kuwaunganishia umeme wananchi.

“Najua hapa hakuna Ofisi ya TANESCO. Mtu wa kuwahudumia anatoka Tandahimba. Hivyo naagiza, kuanzia kesho awepo Meneja hapa ambaye atasimamia Nanyamba peke yake.”

Miongoni mwa majukumu makuu ambayo Waziri alielekeza yatekelezwe na Meneja atakayeteuliwa ni pamoja na kuhakikisha ndani ya siku 20 kuanzia kutolewa kwa agizo, wananchi wote waliolipia wawe wameunganishiwa huduma ya umeme.

Pia, alisema Meneja husika atawajibika kumsimamia mkandarasi anayeunganisha umeme katika eneo hilo kuongeza kasi ya kazi ili kushawishi wananchi wengi zaidi kulipia na kuunganishwa.

Aliagiza Meneja husika kuhakikisha anawafuata wananchi mahala walipo badala ya kukaa ofisini akisubiri wao wamfuate ili kupatiwa huduma.

Aidha, Waziri Kalemani aliwaahidi wananchi wa Mtaa wa Kilimanjaro kuwa watapatiwa umeme kupitia mpango wa umeme vijijini unaotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kutokana na uhalisia wa eneo hilo kuwa na sifa za kijiji zaidi badala ya mtaa kama ulivyoainishwa.

Umati wa wananchi wa Mtaa wa Kilimanjaro, Manispaa ya Nanyamba, wilayani Mtwara wakishuhudia Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (hayupo pichani) akiwasha umeme katika nyumba ya mmojawao ambaye amekwishaunganishiwa huduma hiyo, Desemba 5, 2018.

“Mtaa wa Kilimanjaro na vitongoji vyake mtaunganishiwa umeme wa REA ambao gharama yake ni shilingi 27,000 tu,” alisisitiza.

Waziri Kalemani aliwasisitiza wananchi kuandaa makazi yao kwa ajili ya kuunganishiwa umeme ikiwa ni pamoja na kutandaza nyaya za umeme.

Aidha, aliwashauri wale wasio na uwezo wa kugharamia utandazaji wa nyaya za umeme katika nyumba zao, kutumia kifaa mbadala cha Umeme Tayari (UMETA), ambacho huuzwa kwa bei rahisi ya shilingi 36,000 tu.

Hata hivyo, Waziri alibainisha kuwa Serikali imetoa vifaa hivyo 200 bure kwa ajili ya wananchi watakaowahi kujitokeza ili kuunganishiwa umeme.

Katika ziara hiyo, Waziri Kalemani aliwasha umeme katika moja ya nyumba ya mwananchi aliyeunganishiwa. Pia, alitembelea na kukagua miradi ya umeme, kuzungumza na wananchi na kuwasha umeme katika maeneo mengine kadhaa ikiwemo Namambi.

Na Veronica Simba – Mtwara.

kaspersky kaufen