Mkuu wa Mkoa wa Pwani,  Evarist Ndikilo, amewataka watanzania kuziba masikio na kushirikiana kwa pamoja  ili kufanikisha ujenzi wa Mradi wa kuzalisha umeme wa megawati 2,100 kwa kutumia maporomoko ya maji katika Bonde la Mto Rufiji mkoani Pwani unaotarajiwa kuanza hivi karibuni.

Ndikilo alisema hayo wakati wa Warsha ya Wadau wa  Mradi wa kuzalisha umeme Rufiji wa iliyoandaliwa na Wizara ya Nishati na kuongozwa na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani na Naibu wa Waziri wa Nishati, Subira Mgalu iliyofanyika Ikwiriri mkoani Pwani, Machi 6,2018.

Warsha ya Wadau wa Mradi wa kuzalisha umeme Rufiji wa megawati 2100 iliyoandaliwa na Wizara ya Nishati na kuongozwa na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani na Naibu wa Waziri wa Nishati, Subira Mgalu iliyofanyika Ikwiriri mkoani Pwani.

Warsha hiyo iliwashirikisha wadau mbalimbali wakiwemo Wakuu wa Wilaya, Wabunge, Viongozi wa Serikali za Mitaa na Vijiji ili kupata Elimu kuhusu faida na umuhimu wa mradi huu na utunzaji wa mazingira yanayozunguka bonde la Mto Rufiji.

” Mradi huu umechelewa sana kujengwa, sisi tunauhitaji mno, kuna maneno mengi yanazungumzwa juu ya mradi huu tangu miaka ya 80, yote haya ni kutukatisha tamaa sisi watanzania na kuturudisha nyuma, lakini tusikubal, mradi huu ni lazima ujengwe kwa manufaa yetu sisi, kwao wamejenga na wananufaika na miradi kama hii, sasa kwanini Tanzania ipingwe?, ” alisisitiza Ndikilo.

Aliweka wazi kuwa, mradi huo una manufaa makubwa hasa kwa Mkoa wa Pwani ambao baada ya muda mfupi kuanzia sasa utahitaji kiasi kikubwa sana cha umeme kutokana na kuwepo kwa viwanda vingi mkoani humo.

Hata hivyo,  aliiomba Wizara ya Nishati kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ili kuimarisha hali ya usalama katika eneo hilo na ikiwezekana eneo hilo lijengwe kituo maalum cha Polisi na nyumba za Askari pamoja na Mkuu wa Kituo ili kuimarisha ulinzi.

Kwa upande wake, Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, aliwahakikishia wakazi wa Mkoa wa Pwani kuwa watanufaika zaidi na mradi huo kwa kuwa fusra nyingi za maendeleo zitajitokeza katika maeno yao tofauti na ilivyo sasa zikiwemo Ajira, Biashara, kilimo chenye manufaa na miundombinu ya usafirishaji.

Kuhusu Kilimo, Dkt. Kalemani alisema kuwa kupitia wataalam wa ujenzi wa mradi huo wameweka miundombinu thabiti ambayo itarahisisha uwepo wa kilimo bora cha umwagiliaji katika eneo lililo chini ya Bwawa litakalojengwa pamoja na kuimarisha shughli za uvuvi.

Pia Mradi huo utawezesha kuwepo kwa upatikanaji wa maji ya kutosha kwa matumizi ya wakazi wa Mkoa wa Pwani na Dar es salaam pamoja na umeme wa kutosha,  wa uhakika na wa bei nafuu utakaosaidia kukuza maendeleo ya ustawi wa jamii.

Sambamba na hilo, alisema kuwa mradi huo utazalisha ajira za kudumu na za muda mfupi zaidi ya 10,000 wakati wa kazi za ujenzi pamoja na kuimarisha shughuli za Utalii ndani ya Mbuga ya Selous.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Evarist Ndikilo (aliyesimama) akizungumza wakati Warsha ya Wadau wa Mradi wa kuzalisha umeme Rufiji wa megawati 2,100 iliyoandaliwa na Wizara ya Nishati na kuongozwa na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani na Naibu wa Waziri wa Nishati, Subira Mgalu iliyofanyika Ikwiriri mkoani Pwani.

Aliweka wazi kuwa ujenzi wa mradi huo, utahusisha ujenzi wa kituo kikubwa cha kuhifadhi mizigo katika eneo la Chalinze kwa kuwa eneo hilo limeonekana kuwa na aina tofauti ya miundombinu iliwemo Reli na Barabara ili kurahisisha usafirishaji.

Katika hatua nyingine Wabunge wote wa mkoa wa Pwani walisema wanaunga mkono juhudi za Serikali katika hatua iliyofikiwa ya kujenga mradi huo na kwamba watatoa elimu kwa wananchi ili waelewe umuhimu wake na waweze kuchangamkia fursa za maendeo katika maeneo yao.

Na Zuena Msuya Pwani.