• Kiwanda kikubwa cha kusanifu Mabomba kujengwa Isaka, Kahama

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amesema kuwa kiwanda kikubwa cha kusanifu mabomba yatakayotumika katika mradi wa ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi katika Bandari ya Tanga nchini Tanzania kitajengwa katika mji wa Isaka wilayani Kahama mkoani Shinyanga.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (wa pili), Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wiliam Lukuvi na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainabu Tellack wakati Warsha ya Wadau wa Bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima Uganda hadi Bandari ya Tanga Tanzania iliyofanyika mkoani Shinyanga.

Vile vile alieleza kuwa Wilaya ya Kahama ni miongoni mwa Wilaya 24 nchini zitakazopitiwa na Mradi wa Ujenzi wa Bomba hilo la kusafirisha mafuta ghafi kutoka nchini Uganda hadi Tanzania.

Kufuatia ujenzi wa kiwanda hicho pamoja na utekelezaji wa mradi wa Bomba, Dkt Kalemani aliwataka wakazi wa Mkoa wa Shinyanga kuchangamkia fursa za ajira kwa kuwa zitatoa kipaumbele kwa watanzania.

Dkt. Kalemani alisema hayo wakati wa Warsha ya Wadau wa Bomba la Kusafirisha  Mafuta ghafi Afrika Mashariki iliyofanyika tarehe 26 Aprili, 2018 wilayani Kahama mkoani Shinyanga, kwa lengo la kutoa elimu na kueleza hatua iliyofikiwa katika maendeleo ya utekelezaji wa mradi.

Akizungumzia suala la ajira, Dkt. Kalemani alifafanua kuwa zaidi ya ajira elfu kumi (10,000) zitapatikana wakati wa utekelezaji wa mradi wa  ujenzi wa Bomba hilo ambazo zitatoa kipaumbele kwa watanzania wenye sifa na taaluma husika pia kwa wale wasio na taaluma watafanya  kazi nyingine zisizohitaji taaluma.

“Wakazi wa Kahama changamkieni fursa za ajira na shughuli mbalimbali za kuwaingizia kipato, sitarajii kuona watanzania wakikosa ajira, kazi zitakuwa nyingi kwa wenye sifa na wasio na sifa, tijitume na tuwe wabunifu zaidi, mradi huu ni kwa manufaa yetu sisi,” alisisitiza Dkt. Kalemani

Aidha alisema kuwa, kuwepo kwa mradi huo kuitaingizia Serikali mapato yatokanayo shughuli mbalimbali za kibiashara zitakazo kuwa zikifanyika katika eneo hilo.

Kuhusu hatua iliyofikiwa katika maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo, Dkt. Kalemani alisema kuwa ujenzi rasmi wa Mradi wa Bomba la kusafirisha mafuta ghafi unatarajiwa kuanza mwezi Mei mwaka huu na kwa sasa kinachofanyika ni  kuchukua sampuli ya udongo sehemu ambayo Bomba litapita na kisha kufanya tathmini ya namna ya ulipaji wa fidia kwa wananchi watakaopitiwa na mradi huo.

“Tone la kwanza la mafuta litadondoka mwaka 2020, huu ni uwekezaji mkubwa sana, tuipongeze Serikali ya awamu ya Tano kwa kuhakikisha mradi huu unakuja Tanzania, nchi nyingi ziliuhitaji, wananchi tuutunze na kuulinda mradi wetu”, alisisitiza Dkt. Kalemani.

Baadhi ya wadau walioshiriki Warsha ya Wadau wa Bomba la kusafirisha Mafuta ghafi kutoka Hoima Uganda hadi Bandari ya Tanga Tanzania iliyofanyika mkoani Shinyanga

Bomba hilo lenye urefu wa kilometa 1443 litajengwa kwa kipindi cha miaka mitatu (3) na linatarajiwa kukamilika ifikapo mwaka 2020 litakuwa na uwezo wa kusafirisha mapipa 216,000 kwa siku.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu aliwataka wanawake kuchangamkia fursa ya ajira na biashara katika mradi huo wa Bomba kwa kuwa wanawake wengi wamekuwa wakibaki nyuma.

Hivyo aliwaasa viongozi hasa wanawake kutoa hamasa kwa wanawake wote katika sehemu ambazo zitapitiwa na Bomba la Mafuta ili waweze kunufaika kiuchumi kupitia mradi huo kwa kufanya shughuli mbalimbali ikiwemo biashara ndogo.

Na Zuena Msuya Kahama, Shinyanga.